< Mwanzo 45 >

1 Ndipo Yusufu hakuweza kujizuia mwenyewe mbele ya watumishi waliosimama kando yake. Akasema kwa sauti, “Kila mtu aondoke.” Hivyo hakuna mtumishi aliyesimama kando yake wakati Yusufu alipojitambulisha kwa ndugu zake.
Hapo Yosefu hakuweza kujizuia zaidi mbele ya wote waliokuwa wamesimama karibu naye, akapaza sauti, akasema, “Mwondoeni kila mtu mbele yangu!” Kwa hiyo hapakuwepo mtu yeyote pamoja na Yosefu alipojitambulisha kwa ndugu zake.
2 Akalia kwa sauti, Wamisri wakasikia, na nyumba ya Farao wakasikia kuhusu hilo.
Naye akalia kwa sauti kubwa kiasi kwamba Wamisri walimsikia, hata watu wa nyumbani mwa Farao wakapata hizo habari.
3 Yusufu akawambia ndugu zake, “Mimi ni Yusufu. Je baba yangu ni mzima bado? Ndugu zake hawakuweza kumjibu, kwani walitishwa na uwepo wake.
Yosefu akawaambia ndugu zake, “Mimi ni Yosefu! Je, baba yangu angali hai bado?” Lakini ndugu zake hawakuweza kumjibu, kwa sababu walipatwa na hofu kuu mbele yake.
4 Kisha Yusufu akawambia ndugu zake, “Nikaribieni, tafadhari.” Nao wakasogea. Akawambia, “Mimi ni Yusufu ndugu yenu, mliyemwuza Misri.
Ndipo Yosefu akawaambia ndugu zake, “Sogeeni karibu nami.” Waliposogea, akasema, “Mimi ni ndugu yenu Yosefu, yule ambaye mlimuuza Misri!
5 Lakini sasa msihuzunike au kukasirika miongoni mwenu kwamba mliniuza huku, kwani Mungu alinituma mbele yenu ili kutunza uhai.
Sasa, msihuzunike wala msijichukie wenyewe kwa kuniuza huku, kwa sababu ilikuwa ni ili kuokoa maisha ya watu ndiyo sababu Mungu alinituma niwatangulie ninyi.
6 Maana ni miaka miwili njaa imekuwa katika nchi, na bado kuna miaka mitano ambayo hakutakuwa na kulima wala kuvuna.
Kwa miaka miwili sasa imekuwepo njaa katika nchi, pia kwa miaka mitano ijayo hapatakuwepo kulima wala kuvuna.
7 Mungu alinituma mbele yenu kuwahifadhi kama masalia duniani, na kuwaweka hai kwa ukombozi mkuu.
Lakini Mungu alinitanguliza mbele yenu ili kuhifadhi mabaki kwa ajili yenu katika nchi, na kuokoa maisha yenu kwa wokovu mkuu.
8 Hivyo si ninyi mlionipeleka huku bali ni Mungu, na amenifanya baba kwa Farao, bwana wa nyumba yake yote, na mtawala wa nchi yote ya Misri.
“Kwa hiyo basi, si ninyi mlionileta huku, bali ni Mungu. Alinifanya kuwa baba kwa Farao, bwana wa watu wa nyumbani mwake wote, na mtawala wa Misri yote.
9 Fanyeni haraka mwende kwa baba yangu na mmwambie, 'Hivi ndivyo asemavyo Yusufu mwanao, “Mungu amenifanya bwana kwa Wamisri wote. Shuka kwangu, usikawie.
Sasa rudini haraka kwa baba yangu na mwambieni, ‘Hili ndilo mwanao Yosefu asemalo: Mungu amenifanya mimi kuwa bwana wa Misri yote. Shuka uje kwangu, wala usikawie.
10 Utaishi katika nchi ya Gosheni, nawe utakuwa karibu nami, wewe na watoto wako na watoto wa watoto wako, na kondoo wako na mbuzi wako, na yote uliyonayo.
Nawe utaishi katika nchi ya Gosheni na kuwa karibu nami, wewe, watoto wako na wajukuu wako, makundi yako ya kondoo, mbuzi na ngʼombe, pamoja na vyote ulivyo navyo.
11 Nami nitakuhudumia pale, kwa maana bado kuna miaka mitano ya njaa, hivyo usije ukaingia katika uhitaji, wewe, nyumba yako, na yote uliyonayo.”
Nitawatunza huko, kwa sababu bado iko miaka mingine mitano inayokuja ya njaa. La sivyo, wewe na nyumba yako na wote ulio nao mtakuwa fukara.’
12 Tazama, macho yenu yanaona, na macho ya Benjamini ndugu yangu, kwamba ni kinywa changu kinachoongea nanyi.
“Mnaweza kujionea wenyewe, hata ndugu yangu Benyamini, kwamba hakika ni mimi ninayezungumza nanyi.
13 Mtamwambia baba yangu juu ya heshima yangu yote huku Misri na yote mliyoyaona. Mtaharakisha na kumleta baba yangu huku.”
Mwambieni baba yangu juu ya heshima yote niliyopewa huku Misri, na kuhusu kila kitu mlichokiona. Mleteni baba yangu huku haraka.”
14 Akaikumbatia shingo ya Benjamini ndugu yake na kulia, na Benjamini akalia shongoni mwake.
Ndipo akamkumbatia Benyamini ndugu yake na kulia, naye Benyamini akamkumbatia akilia.
15 Akawabusu ndugu zake wote na kulia kwa ajili yao. Baada ya hayo ndugu zake wakaongea naye.
Pia akawabusu ndugu zake wote, huku akilia. Baada ya hayo ndugu zake wakazungumza naye.
16 Habari ya jambo hili ikasemwa katika nyumba ya Farao: “Ndugu zake Yusufu wamekuja.” Ikampendeza sana Farao na watumishi wake.
Habari zilipofika kwenye jumba la Farao kwamba ndugu zake Yosefu wamefika, Farao na maafisa wake wote wakafurahi.
17 Farao akamwambia Yusufu, “Wambie ndugu zako, 'Fanyeni hivi: Wapakieni wanyama wenu na mwende katika nchi ya Kanaani.
Farao akamwambia Yosefu, “Waambie ndugu zako, ‘Fanyeni hivi: Pakieni wanyama wenu mrudi mpaka nchi ya Kanaani,
18 Mchukueni baba yenu na nyumba zenu mnijie. Nami nitawapa mema ya nchi ya Misri, nanyi mtakula unono wa nchi.'
mkamlete baba yenu na jamaa zenu kwangu. Nitawapa sehemu nzuri sana ya nchi ya Misri nanyi mtafurahia unono wa nchi.’
19 Basi mmeamriwa, 'Fanyeni hivi, chukueni mikokoteni kutoka Misri kwa ajili ya watoto wenu na kwa ajili ya wake zenu. Mchukueni baba yenu na kuja.
“Mnaagizwa pia kuwaambia, ‘Fanyeni hivi: Chukueni magari ya kukokotwa kutoka Misri, kwa ajili ya watoto wenu na wake zenu, mkamchukue baba yenu mje.
20 Msijari kuhusu mali zenu, kwani mema yote ya nchi ya Misri ni yenu.”
Msijali kamwe kuhusu mali zenu, kwa sababu mema yote ya Misri yatakuwa yenu.’”
21 Wana wa Israeli wakafanya hivyo. Yusufu akawapa mikokoteni, kwa kadili ya agizo la Farao, na akawapa mahitaji ya safari.
Hivyo wana wa Israeli wakafanya hivyo. Yosefu akawapa magari ya kukokotwa, kama Farao alivyoagiza, pia akawapa mahitaji kwa ajili ya safari yao.
22 Akawapa wote mavazi ya kubadilisha, lakini akampa Benjamini vipande mia tatu vya fedha na mavazi matano ya kubadilisha.
Kila mmoja mavazi mapya, lakini Benyamini akampa shekeli 300 za fedha, na jozi tano za nguo.
23 Akampelekea baba yake: punda kumi waliobeba mema ya Misri, punda majike kumi wamebeba nafaka, mikate, na mahitaji mengine kwa baba yake kwa ajili ya safari.
Hivi ndivyo vitu alivyotuma kwa baba yake: punda kumi waliochukua vitu vizuri vya Misri, punda wake kumi waliobeba nafaka, mikate na mahitaji mengine ya safari.
24 Hivyo akawaruhusu ndugu zake nao wakaondoka. Akawambia, “Angalieni msijemkagombana njiani.”
Akaagana na ndugu zake walipokuwa wakiondoka, akawaambia, “Msigombane njiani!”
25 Wakapanda kutoka Misri na kuja katika nchi ya Kanaani, kwa Yakobo baba yao.
Basi wakatoka Misri na kufika kwa baba yao Yakobo katika nchi ya Kanaani.
26 Wakamwambia “Yusufu bado yu hai, na ndiye mtawala juu ya nchi yote ya Misri.” Na moyo wake ulishikwa na ushangao, kwani hakuwaamini.
Wakamwambia baba yao, “Yosefu angali hai! Ukweli ni kwamba yeye ndiye mtawala wa Misri yote.” Yakobo akapigwa na bumbuazi; hakuwasadiki.
27 Wakamwambia maneno yote ya Yusufu aliyokuwa amewambia. Yakobo alipoona mikokoteni Yusufu aliyokuwa amepeleka kuwabeba, roho ya Yakobo baba yao ikafufuka.
Lakini walipokwisha kumweleza kila kitu ambacho Yosefu alikuwa amewaambia, na alipoona magari ya kukokotwa Yosefu aliyokuwa amempelekea ya kumchukua aende Misri, roho ya baba yao Yakobo ikahuishwa.
28 Israeli akasema, “Inatosha. Yusufu mwanangu yu hai. Nitakwenda nikamwone kabla sijafa.”
Ndipo Israeli akasema, “Nimesadiki! Mwanangu Yosefu bado yu hai. Nitakwenda nikamwone kabla sijafa.”

< Mwanzo 45 >