< Mwanzo 43 >
1 Njaa ilikuwa kali katika nchi.
Wakati huu njaa ilikuwa bado ni kali mno katika nchi.
2 Ikawa walipokuwa wametumia chakula chote walichokitoa Misri, baba yao akawambia, “Nendeni tena; mtununulie chakula.”
Hivyo wakati walikuwa wamemaliza kula nafaka yote waliyoileta kutoka Misri, Yakobo baba yao akawaambia, “Rudini Misri mkatununulie chakula kingine zaidi.”
3 Yuda akamwambia, “Yule mtu alituonya kwa ukali, 'Hamtauona uso wangu ndugu yenu asipokuwa nanyi.'
Lakini Yuda akamwambia, “Mtu yule alituonya kwa msisitizo, ‘Hamtauona uso wangu tena mpaka mje na ndugu yenu.’
4 Ikiwa utamtuma ndugu yetu pamoja nasi, tutashuka na kuwanunulia chakula.
Kama utakubali ndugu yetu aende pamoja nasi, tutakwenda kuwanunulia chakula.
5 Lakini usipompeleka, hatutashuka. Kwa maana yule mtu alitwambia, 'Hamtauona uso wangu ndugu yenu asipokuwa nanyi.”
Lakini ikiwa hutamruhusu aende, hatutakwenda, kwa sababu mtu yule alituambia, ‘Hamtauona uso wangu tena mpaka mje pamoja na ndugu yenu.’”
6 Israeli akawambia, “Kwa nini mlinitendea mimi vibaya hivyo kwa kumwambia mtu huyo kwamba mnaye ndugu mwingine?”
Israeli akauliza, “Kwa nini mkaniletea taabu hii kwa kumwambia yule mtu mlikuwa na ndugu mwingine?”
7 Wakasema, “Yule mtu alituuliza habari zetu na familia yetu kwa kina. Akasema, 'Je baba yenu bado yuko hai? Je mnaye ndugu mwingine?'Tukamjibu kulingana na maswali haya. Tungejuaje kwamba angetwambia, 'Mleteni ndugu yenu?”
Wakamjibu, “Yule mtu alituhoji kwa undani sana habari zetu na za jamaa yetu. Alituuliza, ‘Je, baba yenu bado yungali hai? Je mnaye ndugu mwingine?’ Sisi tulimjibu maswali yake tu. Tungewezaje kujua kwamba angesema, ‘Mleteni mdogo wenu hapa’?”
8 Yuda akamwambia Israeli baba yake, “Mtume kijana pamoja nami. Tutainuka na kwenda ili kwamba tuishi tusife, wote sisi, wewe, na hata watoto wetu.
Ndipo Yuda akamwambia baba yake Israeli, “Mtume kijana pamoja nami, nasi tutaondoka mara, ili sisi na wewe pamoja na watoto wetu tuweze kuishi, wala tusife.
9 Mimi nitakuwa mdhamini wake. Utaniwajibisha mimi. Kama nisipomleta na kumweka mbele yako, basi nibebe lawama daima.
Mimi mwenyewe nitakuhakikishia usalama wake, mimi mwenyewe nitawajibika kumrudisha. Ikiwa sitamrudisha kwako na kumweka mbele yako, nitakuwa mwenye lawama mbele yako maisha yangu yote.
10 Kwani kama tusingekawia, bila shaka hata sasa tungekuwa tumekwisha rudi mara ya pili.”
Hakika, kama hatukuchelewa kuondoka, tungekuwa tumekwenda na kurudi mara mbili.”
11 Israeli baba yao akawambia, “Kama ni hivyo, basi fanyeni hivi. Chukueni baadhi ya mazao mazuri ya nchi katika mifuko yenu. Mchukulieni yule mtu zawadi: baadhi ya malhamu, asali, viungo na manemane, jozi na lozi.
Basi baba yao Israeli akawaambia, “Kama ni lazima iwe hivyo, basi fanyeni hivi: Wekeni baadhi ya mazao bora ya nchi katika mifuko yenu na mpelekeeni yule mtu kama zawadi, zeri kidogo, asali kidogo, vikolezo, manemane, kungu na lozi.
12 Chukueni pesa mara mbili mikononi mwenu. Pesa iliyorudishwa katika magunia yenu, muichukue tena katika mikono yenu. Pengine walikosea.
Chukueni fedha mara mbili, kwa kuwa mtazirudisha zile fedha zilizowekwa midomoni mwa magunia yenu. Labda ziliwekwa kwa makosa.
13 Mchukueni ndugu yenu pia. Inukeni na mwende tena kwa mtu yule.
Mchukueni ndugu yenu pia mrudi kwa huyo mtu mara moja.
14 Mungu Mwenyezi na awape kuona rehema mbele ya huyo mtu, hivyo kwamba awafungulie ndugu yenu mwingine na Benjamini. Kama nikipotelewa na watoto, nimepotelewa.”
Naye Mungu Mwenyezi awajalieni rehema mbele ya huyo mtu ili apate kumwachia yule ndugu yenu na Benyamini mweze kurudi pamoja. Kwangu mimi kama nikufiwa nimefiwa.”
15 Watu wale wakachukua zawadi hii, na katika mikono yao wakachukua mara mbili ya kiasi cha pesa, pamoja na Benjamini. Wakaamka na kushuka Misri na kusimama mbele ya Yusufu.
Basi hao watu wakazichukua zile zawadi na zile fedha mara mbili pamoja na Benyamini. Wakafanya haraka kwenda Misri na walipofika wakajionyesha kwa Yosefu.
16 Yusufu alipomwona Benjamini akiwa nao, akamwambia mtunzaji wa nyumba yake, “Walete watu hao ndani ya nyumba, chinja mnyama na umwandae, kwani watu hawa watakula chakula cha mchana pamoja nami.”
Yosefu alipomwona Benyamini pamoja nao, akamwambia msimamizi wa nyumba yake, “Wachukue watu hawa nyumbani kwangu, mchinje mnyama na kuandalia chakula kwa kuwa watakula chakula cha mchana pamoja nami.”
17 Mtunzaji wa nyumba akafanya kama Yusufu alivyosema. Akawaleta wale watu nyumbani kwa Yusufu.
Yule Msimamizi akafanya kama Yosefu alivyomwambia na akawachukua wale watu nyumbani kwa Yosefu.
18 Wale ndugu wakaogopa kwa vile walivyoletwa katika nyumba ya Yusufu. Wakasema, “Ni kwa sababu ya pesa iliyorudishwa katika magunia yetu mara ya kwanza tulipoletwa ndani, kwamba atafute nafasi kinyume chetu. Kwamba aweze kutukamata na kutuchukua kama watumwa, na kuchukua punda wetu.” Wakamsogelea mtunzaji wa nyumba ya Yusufu,
Basi watu hao wakaogopa walipopelekwa nyumbani kwa Yosefu. Wakafikiri, “Tumeletwa hapa kwa ajili ya zile fedha zilizorudishwa katika magunia yetu mara ile ya kwanza. Anataka kutushambulia na kutushinda, atuchukue sisi kama watumwa, na atwae hawa punda zetu.”
19 nao wakaongea naye mlangoni mwa nyumba,
Hivyo wakamwendea msimamizi wa nyumba wa Yosefu na kuzungumza naye kwenye ingilio la nyumbani.
20 wakisema, “Bwana wangu, tulikuja mara ya kwanza kununua chakula.
Wakasema, “Tafadhali bwana, tulikuja hapa mara ya kwanza kununua chakula.
21 Ikawa, tulipofika katika eneo la kupumzikia, tukafungua magunia yetu, na, tazama, pesa ya kila mtu ilikuwa katika gunia lake, pesa yetu kwa kiasi kamili. Tumeileta katika mikono yetu.
Lakini mahali pale tulipotua wakati wa jioni tulifungua magunia yetu, na kila mmoja wetu akakuta fedha zake, kwenye mdomo wa gunia lake kiasi kile kile tulicholeta. Kwa hiyo tumezirudisha.
22 Tumekuja na pesa nyingine pia mikonon mwetu ili kununua chakula. Hatujui aliyeziweka pesa katika magunia yetu.”
Pia tumeleta fedha nyingine kwa ajili ya kununulia chakula. Hatujui ni nani aliziweka fedha hizo katika magunia yetu.”
23 Mtunzaji wa nyumba akasema, “Amani iwe kwenu, msiogope. Mungu wenu na Mungu wa baba yenu ndiye aliyeweka pesa katika magunia yenu. Nilipokea pesa yenu.” Kisha mtunzaji wa nyumba akamleta Simoni kwao.
Akawaambia, “Vema, msiogope. Mungu wenu, Mungu wa baba yenu, amewapa ninyi hazina katika magunia yenu; mimi nilipokea fedha yenu.” Ndipo akawaletea Simeoni.
24 Msimamizi wa nyumba akawapeleka watu hao katika nyumba ya Yusufu. Akawapa maji, nao wakaosha miguu yao. Akawalisha punda wao.
Msimamizi akawapeleka wale watu katika nyumba ya Yosefu, akawapa maji ya kunawa miguu na kuwapa punda wao majani.
25 Wakaandaa zawadi kwa ajili ya Yusufu aliyekuwa akija mchana, kwani walikuwa wamesikia kwamba watakula pale.
Wakaandaa zawadi zao ili wampe Yosefu wakati atakapofika adhuhuri, kwa kuwa walikuwa wamesikia kwamba watakula chakula huko.
26 Yusufu alipokuja nyumbani, wakaleta nyumbani zawadi iliyokuwa mikononi mwao, nao wakainama mbele yake hata chini.
Yosefu alipokuja nyumbani, walimkabidhi zile zawadi walizokuwa nazo, ambazo walikuwa wamezileta mle nyumbani, nao wakamsujudia hadi nchi.
27 Akawauliza juu ya hali zao na kusema,”Je baba yenu hajambo, yule mzee mliyemnena? Je bado yu hai?”
Akawauliza kuhusu hali yao, kisha akawaambia, “Yule baba yenu mzee mliyeniambia habari zake, yu hali gani? Je, bado yu hai?”
28 Wakasema, “Mtumishi wako baba yetu hajambo. Na bado yu hai” Wakajinyenyekeza na kuinama chini.
Wakamjibu, “Mtumishi wako baba yetu bado anaishi na ni mzima.” Kisha wakainama chini kumpa heshima.
29 Alipoinua macho yake akamwona Benjamini ndugu yake, mwana wa mamaye, naye akasema, “Je huyu ndiye mdogo wenu mliyemsema?” Na kisha akasema, “Mungu na awe mwenye neema kwako, mwanangu.”
Alipotazama na kumwona Benyamini ndugu yake, mwana wa mama yake hasa, akauliza, “Je, huyu ndiye ndugu yenu wa mwisho, ambaye mlinieleza habari zake?” Ndipo akasema, “Mungu na akufadhili, mwanangu.”
30 Yusufu akaharakisha kutoka chumbani, kwani aliguswa sana kuhusu nduguye. Akatafuta mahali pa kulia. Akaingia chumbani mwake na kulia umo.
Akiwa ameguswa sana kwa kumwona ndugu yake, Yosefu akatoka nje kwa haraka na kutafuta mahali pa kulilia. Akaingia kwenye chumba chake cha pekee na kulilia humo.
31 Akaosha uso wake na kutoka nje. Akajizuia mwenyewe, akasema, “karibuni chakula.”
Baada ya kunawa uso wake, akatoka nje na huku akijizuia akasema, “Pakueni chakula.”
32 Watumishi wakamhudumia Yusufu peke yake na wale ndugu peke yao. Wamisri pale wakala pamoja naye peke yao kwa sababu Wamisri hawakuweza kula mkate na Waebrania, kwani hilo ni chukizo kwa Wamisri.
Wakampakulia Yosefu peke yake, ndugu zake peke yao na Wamisri waliokula pamoja naye peke yao, kwa sababu Wamisri wasingeweza kula pamoja na Waebrania, kwa maana ilikuwa ni chukizo kwa Wamisri.
33 Wale ndugu wakakaa mbele yake, mzaliwa wa kwanza kwa kulingana na haki yake ya uzaliwa, na mdogo kulingana na ujana wake. Wale watu wakashangaa wote.
Watu hao walikuwa wameketi mbele yake kwa mfuatano wa umri wao, kuanzia mzaliwa wa kwanza hadi mzaliwa wa mwisho, wakatazamana wao kwa wao kwa mshangao.
34 Yusufu akapeleka sehemu kwao kutoka katika chakula kilichokuwa mbele yake. Lakini sehemu ya Benjamini ilikuwa mara tano zaidi ya kila ndugu zake. Wakanywa na wakamfurahia.
Wakati walipelekewa sehemu ya chakula kutoka mezani mwa Yosefu, sehemu ya Benyamini ilikuwa mara tano zaidi ya sehemu ya wale wengine. Kwa hiyo wakanywa na kufurahi pamoja naye.