< Mwanzo 40 >

1 Ikawa baada ya mambo haya, mnyweshaji wa mfalme wa Misri na mwokaji wa mfalime walimkosa bwana wao, mfalme wa Misri.
Baada ya muda, mnyweshaji na mwokaji wa mfalme wa Misri, wakamkosea bwana wao, mfalme wa Misri.
2 Farao akawakasirikia hawa maafsa wawili, mkuu wa wanyweshaji na mkuu wa waokaji.
Farao akawakasirikia hawa maafisa wake wawili, mnyweshaji mkuu na mwokaji mkuu,
3 Akawaweka katika lindo katika nyumba ya kapteni wa walinzi, katika gereza lile Yusufu alimofungwa.
akawaweka chini ya ulinzi katika nyumba ya mkuu wa kikosi cha ulinzi katika gereza lile lile alimofungwa Yosefu.
4 Kapteni wa walinzi akamweka Yusufu kuwa mtumishi wao. Walikaa kifungoni kwa muda fulani.
Mkuu wa kikosi cha ulinzi akawakabidhi kwa Yosefu, naye akawahudumia. Walipokuwa wamekaa chini ya ulinzi kwa muda,
5 Wote wakaota ndoto - mnyweshaji na mwokaji wa mfalme wa Misri waliokuwa wamefungwa gerezani - kila mmoja akaota ndoto usiku huo huo, na kila ndoto ilikuwa na tafsiri yake.
kila mmoja wa hao wawili waliokuwa wamewekwa gerezani, yaani mnyweshaji na mwokaji wa mfalme wa Misri, waliota ndoto usiku mmoja, na kila ndoto ilikuwa na maana yake tofauti.
6 Yusufu akaja kwao asubuhi na kuwaona. Tazama, walikuwa na uzuni.
Yosefu alipowajia asubuhi yake, akawaona kwamba walikuwa na huzuni.
7 Akawauliza maafsa wa Farao waliokuwa pamoja naye kifungoni katika nyumba ya bwana wake, kusema, “Kwa nini leo mnaoneka wenye uzuni?”
Ndipo Yosefu akawauliza maafisa hao wa Farao waliokuwa chini ya ulinzi pamoja naye nyumbani mwa bwana wake, akasema, “Mbona nyuso zenu zimejaa huzuni leo?”
8 Wakamwambia, Sisi wote tumeota ndoto na hakuna wakuitafsiri.” Yusufu akawambia, “Je tafsiri haitoki kwa Mungu? Niambieni, tafadhari.”
Wakamjibu, “Sisi sote tuliota ndoto, lakini hapakuwa na mtu yeyote wa kuzifasiri.” Ndipo Yosefu akawaambia, “Je, kufasiri ndoto si kazi ya Mungu? Niambieni ndoto zenu.”
9 Mkuu wa wanyweshaji akamwambia Yusufu ndoto yake. Akamwambia, “Katika ndoto yangu, tazama, kulikuwa na mzabibu mbele yangu.
Basi mkuu wa wanyweshaji akamweleza Yosefu ndoto yake. Akamwambia, “Katika ndoto yangu niliona mzabibu mbele yangu,
10 Na kulikuwa na matawi matatu katika mzabibu huo. Ulipochipua, ukachanua maua na kuzaa vichala vya zabibu.
nao mzabibu ulikuwa na matawi matatu. Mara tu ulipoanza kuchipua, maua yalichanua na vishada vyake vikawa zabibu zilizoiva.
11 Kikombe cha Farao kilikuwa mkononi mwangu. Nikachukua zabibu na kuzikamua katika kikombe cha Farao, na kukiweka kikombe katika mkono wa Farao.”
Kikombe cha Farao kilikuwa mkononi mwangu, nikazitwaa zabibu, nikazikamua katika kikombe cha Farao, na nikaweka kikombe mkononi mwake.”
12 Yusufu akamwambia, “Tafsiri yake ni hii. Yale matawi matatu ni siku tatu.
Yosefu akamwambia, “Hii ndiyo maana yake: Matawi matatu ni siku tatu.
13 Ndani ya siku tatu Farao atakiinua kichwa chako na kukurudisha katika nafasi yako. Utakiweka kikombe cha Farao katika mkono wake, kama ulivyokuwa ulipokuwa mnyweshaji wake.
Katika siku hizi tatu, Farao atakutoa gerezani na kukuweka tena kwenye nafasi yako, nawe utaweka kikombe cha Farao mikononi mwake, kama vile ulivyokuwa unafanya ulipokuwa mnyweshaji wake.
14 Lakini unikumbuke ukifanikiwa, na unionesha wema. Unitaje kwa Farao na kuniondoa hapa gerezani.
Lakini wakati mambo yatakapokuwia mazuri, unikumbuke, unifanyie wema, useme mema juu yangu kwa Farao ili niondoke huku gerezani.
15 Maana hakika nilitekwa kutoka katika nchi ya Waebrania. Na hapa sijafanya chochote kinachonipasa niwekwe gerezani.”
Kwa maana nilichukuliwa kwa nguvu kutoka nchi ya Waebrania, na hata hapa nilipo sikufanya lolote linalostahili niwekwe gerezani.”
16 Mkuu wa waokaji alipoona kwamba tafsiri ilikuwa ya kuvutia, akamwambia Yusufu, “Mimi pia niliota ndoto, na tazama, vikapu vitatu vya mikate vilikuwa juu ya kichwa changu.
Yule mwokaji mkuu alipoona kuwa Yosefu amefasiri ikiwa na maana nzuri, akamwambia Yosefu, “Mimi pia niliota ndoto: Kichwani mwangu kulikuwepo vikapu vitatu vya mikate.
17 Katika kikapu cha juu kulikuwa na kila aina za bidhaa ya kuokwa kwa Farao, lakini ndege wakavila ndani ya kikapu juu ya kichwa changu.”
Katika kikapu cha juu kulikuwa na aina zote za vyakula vilivyookwa kwa ajili ya Farao, lakini ndege walikuwa wakivila kutoka kwenye kikapu nilichokuwa nimebeba kichwani.”
18 Yusufu akajibu na kusema, “Tafsiri ni hii. Vikapu vitatu ni siku tatu.
Yosefu akamwambia, “Hii ndiyo maana yake: Vikapu vitatu ni siku tatu.
19 Ndani ya siku tatu Fareao atakiinua kichwa chako kutoka kwako na atakutundika juu ya mtu. Ndege watakula mwili wako.”
Katika siku hizi tatu, Farao atakata kichwa chako na kukutundika juu ya mti. Nao ndege watakula nyama ya mwili wako.”
20 Ikawa siku ya tatu ambayo ilikuwa ni siku ya kuzaliwa kwa Farao. Akafanya sherehe kwa watumishi wake wote. “Akakiinua juu” kichwa cha mkuu wa wanyweshaji na kichwa cha mkuu wa waokaji, kati ya watumishi wake.
Mnamo siku ya tatu, ilikuwa kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Farao, naye akawaandalia maafisa wake wote karamu. Akawatoa gerezani mnyweshaji mkuu na mwokaji mkuu, akawaweka mbele ya maafisa wake:
21 Akamrudisha mkuu wa wanyweshaji katika majukumu yake, na akakiweka tena kikombe katika mkono wa Farao.
Ndipo akamrudisha mnyweshaji mkuu kwenye nafasi yake, ili aweke kikombe mikononi mwa Farao tena,
22 Lakini akamtundika mkuu wa waokaji, kama Yusufu alivyokuwa amewatafsiria.
lakini akamwangika yule mwokaji mkuu, sawasawa na jinsi Yosefu alivyowaambia katika tafsiri yake.
23 Hata hivyo mkuu wa wanyweshaji hakukumbuka kumsaidia Yusufu. Badala yake, alimsahau.
Pamoja na hayo, mnyweshaji mkuu hakumkumbuka Yosefu, bali alimsahau.

< Mwanzo 40 >