< Mwanzo 4 >

1 Mwanume akalala na Hawa mke wake. Akabeba mimba na akamzaa Kaini. Akasema, “nimezaa mwanaume kwa msaada wa Yahwe.”
Adamu akakutana kimwili na mkewe Eva, naye akapata mimba, akamzaa Kaini. Eva akasema, “Kwa msaada wa Bwana nimemzaa mwanaume.”
2 Kisha akazaa ndugu yake Habili. Sasa Habili akawa mchungaji, lakini Kaini alilima udongo.
Baadaye akamzaa Abeli ndugu yake. Basi Abeli akawa mfugaji, na Kaini akawa mkulima.
3 Ikawa kwamba baada ya muda Kaini alileta sehemu ya mazao ya ardhi kama sadaka kwa Yahwe.
Baada ya muda Kaini akaleta baadhi ya mazao ya shamba kama sadaka kwa Bwana.
4 Habili pia, alileta sehemu ya wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona. Yahwe akamkubali Habili pamoja na sadaka yake,
Lakini Abeli akaleta fungu nono kutoka baadhi ya wazaliwa wa kwanza wa mifugo yake. Bwana akamkubali Abeli pamoja na sadaka yake,
5 lakini Kaini pamoja na sadaka yake Mungu hakuikubali. Kwa hiyo Kaini alikasirika sana, na uso wake ukakunjamana.
lakini Mungu hakumkubali Kaini pamoja na sadaka yake. Kwa hiyo Kaini akakasirika sana, uso wake ukawa na huzuni.
6 Yahwe akamwambia Kaini, “kwa nini umekasirika na kwa nini uso wako umekunjamana?
Kisha Bwana akamwambia Kaini, “Kwa nini umekasirika? Kwa nini uso wako una huzuni?
7 Kama ukifanya vema, je hutapata kibali? lakini kama hutafanya lilio jema, dhambi iko inakuotea mlangoni na inatamani kukutawala, lakini inakupasa uishinde.
Ukifanya lililo sawa, je, hutakubalika? Lakini usipofanya lililo sawa, dhambi inakuvizia mlangoni mwako, inakutamani wewe, lakini inakupasa uishinde.”
8 Kaini akamwambia Habili ndugu yake. Hata wakati walipokuwa shambani, Kaini aliinuka dhidi ya Habili ndugu yake na akamuua. (Katika tafsiri za kale zinasema, Kaini alimwambia Habili ndugu yake, “twende mashambani.” Na wakati walipokuwa shambani, Kaini alimuinukia Habili ndugu yake na kumuua).
Basi Kaini akamwambia ndugu yake Abeli, “Twende shambani.” Walipokuwa shambani, Kaini akamshambulia Abeli ndugu yake, akamuua.
9 Kisha Yahwe akamuuliza Kaini, “Ndugu yako Habili yuko wapi?” Akasema, “sijui. Je mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?”
Kisha Bwana akamuuliza Kaini, “Ndugu yako Abeli yuko wapi?” Akamjibu, “Sijui, je, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?”
10 Yahwe akasema, “umefanya nini? damu ya ndugu yako inaniita mimi kutokea ardhini.
Bwana akasema, “Umefanya nini? Sikiliza! Damu ya ndugu yako inanililia mimi kutoka ardhini.
11 Na sasa umelaaniwa wewe kutoka ardhi ambayo imefungua kinywa chake kupokea damu ya ndugu yako kutoka mikononi mwako.
Sasa umelaaniwa na umehamishwa kutoka ardhi, ambayo imefungua kinywa chake na kupokea damu ya ndugu yako kutoka mkononi mwako.
12 Utakapo ilima ardhi, kuanzia sasa na kuendelea haita kuzalia wewe nguvu yake. Utakuwa mkimbizi na mtu asiye na makao duniani.”
Utakapoilima ardhi, haitakupa tena mazao yake. Utakuwa mtu wa kutangatanga duniani asiye na utulivu.”
13 Kaini akamwambia Yahwe, “Adhabu yangu ni kubwa kuliko uwezo wangu wa kustahimili.
Kaini akamwambia Bwana, “Adhabu yangu ni zaidi ya niwezavyo kustahimili.
14 Kwa hakika umenifukuza siku hii ya leo kutoka kwenye ardhi hii, na sitaonekana mbele ya uso wako. Nitakuwa mkimbizi na mtu nisiye na makao katika dunia, na yeyote atakaye niona ataniua.”
Leo unanifukuza kutoka nchi, nami nitafichwa mbali na uwepo wako. Nitakuwa mtu wa kutangatanga asiyetulia duniani na yeyote anionaye ataniua.”
15 Yahwe akamwambia, “ikiwa mtuyeyote atamuua Kaini, kisasi kitakuwa juu yake mara saba.” Kisha Yahwe akaweka alama juu ya Kaini, ili kwamba kama mtu awayeyote akimuona, mtu huyo asimshambulie.
Lakini Bwana akamwambia, “La sivyo, ikiwa mtu yeyote atamuua Kaini atalipizwa kisasi mara saba zaidi.” Kisha Bwana akamwekea Kaini alama ili mtu yeyote ambaye angemwona asimuue.
16 Kwa hiyo Kaini akatoka mbele ya uwepo wa Yahwe na akaishi katika nchi ya Nodi, mashariki mwa Edeni.
Kwa hiyo Kaini akaondoka mbele za Bwana akaenda kuishi katika nchi ya Nodi, iliyoko mashariki ya Edeni.
17 Kaini akamjua mke wake na akapata mimba. Akamzaa Henoko. Akajenga mji na akauita kwa jina la mwanae Henoko.
Kaini akakutana kimwili na mkewe, naye akapata mimba na akamzaa Enoki. Wakati huo Kaini alikuwa anajenga mji, akauita Enoki jina la mtoto wake.
18 Kwa Henoko akazaliwa Iradi. Iradi akamzaa Mehuyaeli. Mehuyaeli akamzaa Methushaeli. Methushaeli akamzaa Lameki.
Enoki akamzaa Iradi, Iradi akamzaa Mehuyaeli, Mehuyaeli akamzaa Methushaeli, na Methushaeli akamzaa Lameki.
19 Lameki akajitwalia wake wawili: jinala mmoja alikuwa Ada, na jina la yule mwingine alikuwa Sila.
Lameki alioa wanawake wawili, mmoja aliitwa Ada, na mwingine Sila.
20 Ada akamzaa Yabali. Huyu ndiye alikuwa baba yao na wale walioishi hemani ambao wanafuga wanyama.
Ada akamzaa Yabali ambaye ni baba wa wale walioishi katika mahema na kufuga wanyama.
21 Ndugu yake aliitwa Yubali. Huyu alikuwa baba yao na wale wapigao kinubi na filimbi.
Kaka yake aliitwa Yubali, aliyekuwa baba wa wote wapigao zeze na filimbi.
22 Sila naye akamzaa Tubal Kaini, mfua vyombo vya shaba na chuma. Dada yake na Tubal Kaini alikuwa Naama.
Pia Sila alikuwa na mtoto wa kiume aliyeitwa Tubali-Kaini ambaye alifua vifaa vya aina mbalimbali vya shaba na chuma. Naama alikuwa dada wa Tubali-Kaini.
23 Lameki akawaambia wake zake, Ada na Sila, sikieni sauti yangu; ninyi wake wa Lameki, sikilizeni nisemacho. Kwa kuwa nimemuua mtu kwa kunijeruhi, kijana kwa kunichubua.
Lameki akawaambia wake zake, “Ada na Sila nisikilizeni mimi; wake wa Lameki sikieni maneno yangu. Nimemuua mtu kwa kunijeruhi, kijana mdogo kwa kuniumiza.
24 Ikiwa Kaini atalipiwa kisasi mara saba, ndipo Lameki atalipiwa kisasi mara sabini na saba.”
Kama Kaini atalipizwa kisasi mara saba, basi Lameki itakuwa mara sabini na saba.”
25 Adam akamjua mke wake tena, na akazaa mtoto mwanaume. Akamuita jina lake Sethi na akasema, “Mungu amenipatia mtoto mwingine wa kiume kwa nafasi ya Habili, kwa kuwa Kaini alimuuwa.”
Adamu akakutana kimwili na mke wake tena, akamzaa mwana, akamwita Sethi, akisema, “Mungu amenijalia mwana mwingine badala ya Abeli, kwa kuwa Kaini alimuua.”
26 Mtoto wa kiume alizaliwa kwa Sethi na akamuita jina lake Enoshi. Wakati huo watu walianza kuliitia jina la Yahwe.
Naye Sethi akamzaa mwana, akamwita Enoshi. Wakati huo watu wakaanza kuliitia jina la Bwana.

< Mwanzo 4 >