< Mwanzo 37 >
1 Yakobo akaishi katika nchi aliyokaa babaye, katika nchi ya Kanaani.
2 Haya ndiyo matukio yaliyomhusu Yakobo. Yusufu, aliyekuwa kijana wa miaka kumi na saba, alikuwa akilichunga kundi pamoja na ndugu zake. Alikuwa pamoja na wana wa Bilha na pamoja na wana wa Zilpa, wake wa baba yake. Yusufu akaleta taarifa yao mbaya kwa baba yao.
3 Basi Israeli akampenda Yusufu kuliko wanawe wote kwa sababu alikuwa mwana wa uzee wake. Akamshonea vazi zuri.
4 Ndugu zake wakaona kwamba baba yao alimpenda sana kuliko ndugu zake wote. Wakamchukia na hawakuongea naye vema.
5 Yusufu akaota ndoto, na akawambia ndugu zake. Wakamchukia zaidi.
6 Aliwambia, “Tafadhari sikilizeni ndoto hii niliyoiota.
7 Tazama, tulikuwa tukifunga miganda ya nafaka shambani na tazama, mganda wangu ukainuka na kusimama wima, na tazama, miganda yenu ikasogea na kuuinamia mganda wangu”
8 Ndugu zake wakamwambia, “Je ni kweli utatutawala? Je utatutawala juu yetu? Hata wakamchukia zaidi kwa ajili ya ndoto zake na maneno yake.
9 Akaota ndoto nyingine na kuwasimulia ndugu zake. Alisema, “Tazama, nimeota ndoto nyingine: Jua na mwezi na nyota kumi na moja ziliniinamia.”
10 Akamwambia baba yake vile vile alivyowambia ndugu zake, na baba yake akamkemea. Akamwambia, Je umeota ndoto ya namna gani hii? Je mama yako na mimi na ndugu zako kweli tutakuja kukuinamia mpaka chini?”
11 Ndugu zake wakamwonea wivu, lakini baba yake akaliwema jambo hilo moyoni.
12 Ndugu zake wakaenda kulichunga kundi la baba yao huko Shekemu.
13 Israeli akamwambia Yusufu, 'Je ndugu zako hawalichungi kundi huko Shekemu? Njoo, nami nitakutuma kwao.” Yusufu akamwambia, “nipo tayari.”
14 Akamwambia, “Basi nenda, uwaone ndugu zako na kundi wanaendeleaje, na uniletee neno.” Hivyo Yakobo akamtuma kutoka katika bonde la Hebroni, na Yusufu akaenda Shekemu.
15 Mtu mmoja akamwona Yusufu. Tazama, Yusufu alikuwa akizunguka kondeni. Yule mtu akamwuliza, “Unatafuta nini?”
16 Yusufu akamwambia, “Nawatafuta ndugu zangu. Tafadhari, niambie, wananalichunga wapi kundi.”
17 Yule mtu akasema, “Waliondoka mahali hapa, kwa maana niliwasikia wakisema, 'Haya twende Dothani.” Yusufu akawafuata ndugu zake na kuwaona huko Dothani.
18 Wakamwona kutokea mbali, na kabla hajawakaribia, wakapanga njama ya kumwua.
19 Ndugu zake wakaambiana wao kwa wao, “Tazama, mwotaji anakaribia.
20 Njoni sasa, na tumwue na kumtupa katika mojawapo ya mashimo haya. Nasi tutasema, 'Mnyama mkali amemrarua.' Nasi tutaona ndoto zake zitakuwaje.”
21 Rubeni alilisikia hilo na kumwokoa kutoka katika mikono yao. Alisema, “Tusiuondoe uhai wake.”
22 Rubeni aliwambia, “Msimwage damu. Mtupeni katika shimo hili lililopo nyikani, lakini msiweke mikono yenu juu yake” - ili kwamba aweze kumwokoa katika mikono yao na kumrudisha kwa baba yake.
23 Ikawa Yusufu alipowafikia ndugu zake, walimvua vazi lake zuri.
24 Wakamchukua na kumtupa shimoni. Shimo lilikuwa tupu bila maji.
25 Wakakaa chini kula mkate. Walipoinua macho yao na kuangalia, na, tazama, msafara wa Waishmaeli ulikuwa ukija kutoka Gileadi, pamoja na ngamia wao waliochukua viungo, malhamu na manemane. Walikuwa wakisafiri kuvichukua kuelekea Misri.
26 Yuda akawambia ndugu zake, “Ni faida gani kama tutamwua ndugu yetu na kufunika damu yake?
27 Haya, na tumwuze kwa Waishmaeli na wala tusiweke mikono yetu juu yake. Kwani yeye ni ndugu yetu, nyama yetu.” Ndugu zake wakamsikiliza.
28 Wafanyabiashara wa Kimidiani wakapita. Ndugu zake wakamwinua na kumtoa Yusufu shimoni. Wakamwuza Yusufu kwa Waishmaeli kwa vipande ishirini vya fedha. Waishmaeli wakamchukua Yusufu mpaka Misri.
29 Rubeni akarudi kwenye shimo, na, tazama, Yusufu hakuwemo shimoni. Akararua mavazi yake.
30 Akarudi kwa ndugu zake na kusema, “Kijana yuko wapi? Na mimi, je niende wapi?”
31 Wakachinja mbuzi na kisha wakalichukua vazi la Yusufu na kulichovya katika damu.
32 Kisha wakalipeleka kwa baba yao na kusema, “Tumeiona hii. Tafadhari angalia kwamba ni vazi la mwanao au hapana.”
33 “Yakobo akaitambua na kusema, “Ni nguo ya mwanangu. Mnyama wa mwitu amemrarua. Bila shaka Yusufu ameraruliwa katika vipande.
34 Yakobo akararua mavazi yake na kuvaa mavazi ya magunia katika viuno vyake. Akaomboleza kwa ajili ya mwanawe siku nyingi.
35 Wanawe na binti zake wote wakainuka na kumfariji, lakini alikataa kufarijiwa. Akasema, “Hakika nitashuka kuzimu nikimwombolezea mwanangu.” Babaye akamlilia. (Sheol )
36 Wamidiani wakamwuza huko Misri kwa Potifa, afisa wa Farao, kepteni wa walinzi.