< Mwanzo 35 >

1 Mungu akamwambia Yakobo, “Inuka, panda kwenda Betheli, na ukae pale. Unijengee madhabahu pale, niliyekutokea pale ulipomkimbia Esau kaka yako.”
Kisha Mungu akamwambia Yakobo, “Panda uende Betheli ukakae huko na ukamjengee Mungu madhabahu huko, Yeye aliyekutokea ulipokuwa unamkimbia Esau ndugu yako.”
2 Kisha Yakobo akawambia nyumba yake na wote aliokuwa nao, “Wekeni mbali miungu yote ya kigeni iliyo kati yenu, jitakaseni wenyewe, na kubadili mavazi yenu.
Hivyo Yakobo akawaambia watu wa nyumbani mwake pamoja na wote waliokuwa naye, “Iondoeni miungu ya kigeni ile iliyoko katikati yenu, jitakaseni na mkabadilishe nguo zenu.
3 Kisha tuondoke na kwenda Betheli. Nitajenga pale madhabahu kwa Mungu, aliyenijibu katika siku ya shida yangu, naye amekuwa pamoja nami kila nilikokwenda.
Kisha njooni, twende Betheli, mahali nitakapomjengea Mungu madhabahu, aliyenijibu katika siku ya shida yangu, ambaye amekuwa pamoja nami popote nilipokwenda.”
4 Hivyo wakampa Yakobo miungu yote ya kigeni iliyokuwa mikononi mwao, na heleni zilizokuwa katika masikio yao. Yakobo akazifukia chini ya mwaloni uliokuwa karibu na Shekemu.
Kwa hiyo wakampa Yakobo miungu yote ya kigeni waliyokuwa nayo, pamoja na pete zilizokuwa masikioni mwao. Yakobo akavizika chini ya mti wa mwaloni huko Shekemu.
5 Kwa kadili walivyo safiri, Mungu akaifanya miji yote iliyokuwa karibu nao kuhofu, hivyo watu hao hawakuwafuatia wana wa Yakobo.
Kisha wakaondoka, na hofu ya Mungu ikawapata miji yote iliyowazunguka. Kwa hiyo hakuna aliyewafuatia wana wa Yakobo.
6 Hivyo Yakobo akafika Luzu(ndiyo Betheli), ulioko katika nchi ya Kanaani, yeye na watu wote aliokuwa nao.
Yakobo na watu wote waliokuwa pamoja naye wakafika Luzu (ndio Betheli), katika nchi ya Kanaani.
7 Alijenge madhabahu na kuliita eneo hilo El Betheli, kwa sababu Mungu alikuwa amejifunua kwake, alipokuwa akimkimbia ndugu yake.
Huko akajenga madhabahu na akapaita mahali pale El-Betheli, kwa sababu mahali pale ndipo Mungu alipojifunua kwake alipokuwa akimkimbia ndugu yake.
8 Debora, mlezi wa Rebeka, akafa. Akazikwa chini kutoka Betheli chini ya mwaloni, hivyo ikaitwa Aloni Bakuthi.
Wakati huu Debora, mlezi wa Rebeka, akafa na akazikwa chini ya mti wa mwaloni ulioko chini ya Betheli. Kwa hiyo pakaitwa Alon-Bakuthi.
9 Yakobo alipokuja kutoka Padani Aramu, Mungu akamtokea tena na kumbariki.
Baada ya Yakobo kurudi kutoka Padan-Aramu, Mungu alimtokea tena na kumbariki.
10 Mungu akamwambia, “Jina lako ni Yakobo, lakini jina lako halitakuwa Yakobo tena. Jina lako litakuwa Israeli.” Hivyo Mungu akamwita jina lake Israeli.
Mungu akamwambia, “Jina lako ni Yakobo, lakini hutaitwa tena Yakobo, jina lako utakuwa Israeli.” Kwa hiyo akamwita Israeli.
11 Mungu akamwambia, “Mimi ni Mungu Mwenyezi, Uwe mwenye kuzaa na kuongezeka. Taifa na wingi wa mataifa watakujia, na wafalme watatoka miongoni mwa uzao wako.
Mungu akamwambia, “Mimi ndimi Mungu Mwenyezi, ukazae na kuongezeka. Taifa na jamii ya mataifa itatoka kwako, nao wafalme watatoka viunoni mwako.
12 Nchi ambayo nilimpa Ibrahimu na Isaka, nitakupa wewe. Nami nitaupa pia uzao wako baada yako nchi hii.”
Nchi niliyowapa Abrahamu na Isaki nakupa wewe pia, nami nitawapa wazao wako baada yako.”
13 Mungu akapanda kutoka mahali alipoongea naye.
Kisha Mungu akapanda juu kutoka kwake mahali pale alipozungumza naye.
14 Yakobo akaweka nguzo katika eneo ambalo Mungu alikuwa ameongea naye, nguzo ya jiwe. Akamimina juu yake sadaka ya kinywaji na akamimina mafuta juu yake.
Yakobo akasimamisha nguzo ya jiwe mahali pale Mungu alipozungumza naye, akamimina sadaka ya kinywaji juu yake, pia akamimina mafuta juu yake.
15 Yakobo akaiita sehemu Mungu aliyoongea naye, Betheli
Yakobo akapaita mahali pale Mungu alipozungumza naye Betheli.
16 Wakaendelea na safari kutoka Betheli. Walipokuwa kitambo kabla ya kufika Efrathi, Raheli akashikwa na uchungu.
Kisha wakaondoka Betheli. Walipokuwa umbali fulani kabla ya kufika Efrathi, Raheli akaanza kusikia uchungu na alipata shida kuu.
17 Akawa na utungu mzito. Alipokuwa katika utungu mzito zaidi, mkunga akamwambia, “Usiogope, kwani sasa utapata mtoto mwingine wa kiume.”
Alipokuwa katika shida hii katika kujifungua, mkunga akamwambia, “Usiogope, kwa sababu umempata mwana mwingine.”
18 Hata alipokaribia kufa, kwa pumzi yake ya mwisho akamwita jina lake Benoni, lakini baba yake akamwita jina lake Benjamini.
Hapo alipopumua pumzi yake ya mwisho, kwa maana alikuwa akifa, akamwita mwanawe Benoni. Lakini babaye akamwita Benyamini.
19 Raheli akafa na kuzikwa katika njia iendayo Efrathi (ndio Bethlehemu).
Kwa hiyo Raheli akafa, akazikwa kando ya njia iendayo Efrathi (ndio Bethlehemu).
20 Yakobo akaweka nguzo katika kaburi lake. Ndiyo alama ya kaburi la Raheli hata leo.
Juu ya kaburi lake, Yakobo akasimamisha nguzo, ambayo mpaka leo inatambulisha kaburi la Raheli.
21 Israeli akaendelea na safari na akaweka hema yake kuvuka mnara wa walinzi wa kondoo.
Israeli akaendelea tena na safari yake na kupiga hema mbele mnara wa Ederi.
22 Yakobo alipokuwa akiishi katika nchi hiyo, Rubeni akalala na Bilha suria wa baba yake, na Israeli akasikia kuhusu hilo. Basi Yakobo alikuwa na wana kumi na mbili.
Wakati Israeli alipokuwa akiishi katika nchi ile, Reubeni mwanawe alikutana kimwili na suria wa baba yake aitwaye Bilha, naye Israeli akasikia jambo hili. Yakobo alikuwa na wana kumi na wawili:
23 Wanawe kwa Lea walikuwa Rubeni, mzaliwa wa kwanza wa Yakobo, na Simoni, Lawi, Yuda, Isakari, na Zabuloni.
Wana wa Lea walikuwa: Reubeni mzaliwa wa kwanza wa Yakobo, Simeoni, Lawi, Yuda, Isakari na Zabuloni.
24 Wanawe kwa Raheli walikuwa Yusufu na Benjamini.
Wana wa Raheli walikuwa: Yosefu na Benyamini.
25 Wanawe kwa Bilha, mjakazi wa Raheli walikuwa Dani na Naftali.
Wana waliozaliwa na Bilha mtumishi wa kike wa Raheli walikuwa: Dani na Naftali.
26 Wana wa Zilpa, mjakazi wa Lea, walikuwa Gadi na Asheri. Hawa wote walikuwa wana wa Yakobo waliozaliwa kwake huko Padani Aramu.
Wana waliozaliwa na Zilpa mtumishi wa kike wa Lea walikuwa: Gadi na Asheri. Hawa walikuwa wana wa Yakobo, waliozaliwa kwake akiwa Padan-Aramu.
27 Yakobo akaja kwa Isaka, baba yake, huko Mamre katika Kiriathi Arba (jina sawa na Hebroni), alipoishi Ibrahimu na Isaka.
Yakobo akarudi nyumbani kwa baba yake Isaki huko Mamre, karibu na Kiriath-Arba (yaani Hebroni), ambapo walikuwa wameishi Abrahamu na Isaki.
28 Isaka akaishi miaka mia moja na themanini.
Isaki aliishi miaka 180.
29 Isaka akapumua pumzi yake ya mwisho na akafa, na akakusanywa kwa wahenga wake, na mtu mzee amejaa siku. Esau na Yakobo, wanawe, wakamzika.
Kisha Isaki akapumua pumzi yake ya mwisho akafa, akakusanywa pamoja na watu wake akiwa mzee wa miaka mingi. Nao wanawe Esau na Yakobo wakamzika.

< Mwanzo 35 >