< Mwanzo 32 >

1 Yakobo pia akaendelea na safari yake, na malaika wa Mungu wakakutana naye.
Yakobo pia akaondoka akaenda zake, nao malaika wa Mungu wakakutana naye.
2 Yakobo alipowaona, akasema, “Hii ni kambi ya Mungu,” hivyo akapaita mahali pale Mahanaimu.
Yakobo alipowaona, akasema, “Hii ni kambi ya Mungu!” Kwa hiyo akapaita mahali pale Mahanaimu.
3 Yakobo akatuma wajumbe mbele yake waende kwa Esau ndugu yake katika nchi ya Seiri, katika eneo la Edomu.
Yakobo akatuma wajumbe kumtangulia kwa Esau ndugu yake huko Seiri, katika nchi ya Edomu.
4 Aliwaagiza, kusema, “Hivi ndivyo mtakavyosema kwa bwana wangu Esau: Hivi ndivyo mtumishi wako Yakobo asemavyo: 'Nimekuwa nikikaa na Labani, naye amekawilisha kurudi kwangu hata sasa.
Akawaagiza akisema: “Hili ndilo mtakalomwambia bwana wangu Esau: ‘Mtumishi wako Yakobo anasema, nimekuwa nikiishi pamoja na Labani na nimekuwako huko mpaka sasa.
5 Nina ng'ombe, punda, na kondoo, wajori na wajakazi. Nimetuma ujumbe huu kwa bwana wangu, ili kwamba nipate kibali mbele zako.”
Ninao ngʼombe na punda, kondoo na mbuzi, watumishi wa kiume na wa kike. Sasa ninatuma ujumbe huu kwa bwana wangu, ili nipate kibali machoni pako.’”
6 Wajumbe wakarudi kwa Yakobo na kusema, “Tulikwenda kwa Esau ndugu yako. Anakuja kukulaki, na watu mia nne pamoja naye.”
Wajumbe waliporudi kwa Yakobo, wakamwambia, “Tulikwenda kuonana na ndugu yako Esau, naye sasa anakuja kukulaki akifuatana na wanaume 400.”
7 Ndipo Yakobo alipoogopa sana na kutaabika. Hivyo akagawanya watu aliokuwa nao katika kambi mbili, na kondoo pia, mbuzi na ngamia.
Kwa hofu kuu na huzuni, Yakobo akagawanya watu aliokuwa nao katika makundi mawili, pia akagawanya makundi ya kondoo na mbuzi, na vilevile ngʼombe na ngamia.
8 Akasema, “Ikiwa Esau ataishambulia kambi moja, ndipo kambi nyingine itakaposalimika.”
Yakobo alifikiri, “Kama Esau akija na kushambulia kundi moja, kundi lililobaki litaweza likanusurika.”
9 Yakobo akasema, “Mungu wa baba yangu Ibrahimu, na Mungu wa baba yangu Isaka, Yahwe, uliyeniambia, 'Rudi katika nchi yako na kwa jamaa yako, nami nitakustawisha,'
Ndipo Yakobo akaomba, “Ee Mungu wa baba yangu Abrahamu, Mungu wa baba yangu Isaki, Ee Bwana, ambaye uliniambia, ‘Rudi katika nchi yako na jamaa yako, nami nitakufanya ustawi,’
10 Mimi sistahili matendo yako yote ya agano la uaminifu na ustahilifu wote uliomfanyia mtumishi wako. Kwa maana nilikuwa na fimbo tu nilipovuka mto huu wa Yordani, na sasa nimekuwa matuo mawili.
mimi sistahili fadhili na uaminifu wako wote ulionitendea mimi mtumishi wako. Nilikuwa na fimbo tu mkononi mwangu nilipovuka mto huu wa Yordani, lakini sasa ninayo makundi mawili.
11 Tafadhari niokoe kutoka katika mikono ya ndugu yangu, mikono ya Esau, kwa maana namwogopa, kwamba atakuja na kunishambulia mimi na wamama na watoto.
Nakuomba, uniokoe na mkono wa ndugu yangu Esau, kwa maana ninaogopa kuwa atakuja kunishambulia, pia mama pamoja na watoto wao.
12 Lakini ulisema, 'hakika nitakufanya ufanikiwe. Nitaufanya uzao wako kuwa kama mchanga wa bahari, ambao hauwezi kuhesabika kwa hesabu yake.”
Lakini umeshasema, ‘Hakika nitakufanya ustawi na kuufanya uzao wako kuwa mwingi kama mchanga wa baharini ambao hauwezi kuhesabika!’”
13 Yakobo akakaa pale usiku huo. Akachukua baadhi ya alivyokuwa navyo kama zawadi kwa Esau, ndugu yake:
Akalala pale usiku ule, miongoni mwa vitu alivyokuwa navyo, akachagua zawadi kwa ajili ya Esau ndugu yake:
14 mbuzi majike mia mbili na mabeberu ishirini, kondoo majike mia mbili na madume ya kondoo ishirini,
Mbuzi waume ishirini na mbuzi wake 200, kondoo dume ishirini na kondoo wake 200.
15 ngamia wakamwao thelathini na wana wao, ng'ombe madume arobaini na madume kumi ya ng'ombe, punda wa kike ishirini na madume yake ishirini.
Ngamia wake thelathini pamoja na ndama zao, ngʼombe wake arobaini na mafahali kumi, punda wake ishirini na punda waume kumi.
16 Akawaweka katika mikono ya watumishi wake, kila kundi peke yake. Akawambia watumishi, “Tangulieni mbele yangu na mwache nafasi kati ya makundi ya wanyama.”
Akaviweka chini ya uangalizi wa watumishi wake, kila kundi peke yake na kuwaambia, “Nitangulieni na kuacha nafasi kati ya makundi.”
17 Akamwagiza mtumishi wa kwanza, akisema, “Ndugu yangu Esau atakapokutana nawe na kukuuliza, akasema, 'Ninyi ni wa nani? Mnakwenda wapi? Na wanyama hawa mbele yenu ni wa nani?
Akamwagiza yule aliyetangulia kuwa, “Ndugu yangu Esau atakapokutana nawe na kukuuliza, ‘Wewe ni wa nani? Unakwenda wapi? Wanyama hawa wote mbele yako ni mali ya nani?’
18 Ndipo umwambie, 'Ni wa mtumishi wako Yakobo. Ni zawadi wanaopelekwa kwa bwana wangu Esau. Na tazama, yeye pia anakuja nyuma yetu.”
Ndipo utakaposema, ‘Ni mali ya mtumishi wako Yakobo. Ni zawadi ambazo zimetumwa kwa bwana wangu Esau, naye anakuja nyuma yetu.’”
19 Yakobo akatoa maelekezo kwa kundi la pili pia, la tatu, na watu wote walioyafuata makundi ya wanyama. Akasema, mseme vilevile kwa Esau mtakapokutana naye.
Akamwagiza pia yule mtumishi wa kundi la pili, la tatu na yale mengine yote yaliyofuata akiwaambia, “Mtamwambia Esau maneno hayo hayo mtakapokutana naye.
20 Mnapaswa pia kusema, 'mtumwa wako Yakobo pia anakuja nyuma yetu.” Kwani alifikiri, “nitamtuliza Esau kwa zawadi nilizozituma mbele yangu. Kisha baadaye, nitakapomwona, bila shaka atanipokea.”
Hakikisheni mmesema, ‘Mtumishi wako Yakobo anakuja nyuma yetu.’” Kwa kuwa alifikiri, “Nitaweza kumtuliza kwa zawadi hizi ninazotanguliza, hatimaye, nitakapomwona, huenda atanikubali.”
21 Hivyo zawadi zikatangulia mbele yake. Yeye mwenyewe akakaa kambini usiku huo
Kwa hiyo zawadi za Yakobo zilitangulia mbele yake, lakini yeye mwenyewe alilala kambini usiku ule.
22 Yakobo akaamka wakati wa usiku, na akawachukua wakeze, wajakazi wake na wanaye kumi na wawili. Akawawavusha kijito cha Yaboki.
Usiku ule Yakobo akaamka akawachukua wake zake wawili, watumishi wake wawili wa kike na wanawe kumi na mmoja na akavuka kivuko cha Yaboki.
23 Kwa njia hii akawapeleka kupitia chemichemi pamoja na mali yake yote.
Baada ya kuwavusha ngʼambo ya kijito, alivusha pia mali zake zote.
24 Yakobo akaachwa peke yake, na mtu akashindana naya mpaka alfajiri.
Kwa hiyo Yakobo akaachwa peke yake na mtu mmoja akashikana naye mweleka mpaka mapambazuko.
25 Mtu yule alipoona kwamba hawezi kumshinda, akalipiga paja lake. Paja la Yakobo likatenguka alipokuwa akishindana naye.
Yule mtu alipoona kuwa hawezi kumshinda, aligusa kiungio cha nyonga ya Yakobo kwa hiyo nyonga yake ikateguka wakati alipokuwa akishikana mweleka na yule mtu.
26 Yule mtu akasema, “Niache niende, kwani kunakucha.” Yakobo akasema, sitakuacha uende mpaka uwe umenibariki.”
Ndipo yule mtu akasema, “Niache niende, kwa kuwa ni mapambazuko.” Lakini Yakobo akajibu, “Sitakuacha uende usiponibariki.”
27 Yule mtu akamwuliza, “Jina lako ni nani?” Yakobo akasema, “Yakobo.” Yule mtu akasema,
Yule mtu akamuuliza, “Jina lako nani?” Akajibu, “Yakobo.”
28 “Jina lako halitakuwa Yakobo tena, ila Israeli. Kwa kuwa umeshindana na Mungu na wanadamu na umeshinda.”
Ndipo yule mtu akasema, “Jina lako halitakuwa tena Yakobo, bali Israeli, kwa sababu umeshindana na Mungu na watu pia, nawe umeshinda.”
29 Yakobo akamwambia, “Tafadhari niambie jina lako.” Akasema, “Kwa nini kuniuliza jina langu?” Kisha akambariki pale.
Yakobo akasema, “Tafadhali niambie jina lako.” Lakini akajibu, “Kwa nini kuniuliza Jina langu?” Ndipo akambariki huko.
30 Yakobo akapaita mahali pale Penieli kwani alisema, “Nimemwona Mungu uso kwa uso, na maisha yangu yamesalimika.”
Kwa hiyo Yakobo akapaita mahali pale Penieli, akasema, “Ni kwa sababu nimemwona Mungu uso kwa uso na bado maisha yangu yameokoka.”
31 Jua likatoka wakati Yakobo anaipita Penieli. Alikuwa akichechemea kwa sababu ya paja lake.
Jua lilikuwa linachomoza Yakobo alipoondoka Penueli, naye alikuwa akichechemea kwa sababu ya nyonga yake.
32 Ndiyo maana wana wa Israeli hawali kano ya paja iliyopo katika nyonga ya paja, kwa sababu yule mtu aliziumiza hizo kano alipotegua paja la Yakobo.
Kwa hiyo mpaka leo Waisraeli hawali mshipa ulioungana na kiungio cha nyonga, kwa sababu kiungio cha nyonga ya Yakobo kiliteguliwa karibu na mshipa huo.

< Mwanzo 32 >