< Mwanzo 28 >

1 Isaka akamwita Yakobo, akambariki, na kumwagiza, “Usichukuwe mwanamke katika wanawake wa Kikanaani.
Basi Isaki akamwita Yakobo, akambariki na akamwamuru, akisema, “Usioe mwanamke wa Kikanaani.
2 Inuka, nenda Padani Aramu, katika nyumba ya Bethueli baba wa mama yako, na uchukue mwanamke pale, mmojawapo wa binti za Labani, kaka wa mama yako.
Nenda mara moja mpaka Padan-Aramu, kwenye nyumba ya Bethueli baba wa mama yako. Uchukue mke kati ya binti za Labani ambaye ni ndugu wa mama yako.
3 Mungu Mwenyezi na akubariki, akupe uzao na akuzidishe, hata uwe wingi wa watu.
Mungu Mwenyezi na akubariki uwe na uzao uongezeke idadi yako upate kuwa jamii kubwa ya watu.
4 Na akupe baraka ya Ibrahimu, wewe, na uzao wako baada yako, kwamba uweze kumilki nchi ambapo umekuwa ukiishi, ambayo Mungu alimpa Ibrahimu.”
Na akupe wewe na uzao wako baraka aliyopewa Abrahamu, upate kumiliki nchi unayoishi sasa kama mgeni, nchi ambayo Mungu alimpa Abrahamu.”
5 Hivyo Isaka akamwondoa Yakobo. Yakobo akaenda Padani Aramu, kwa Labani mwana wa Bethueli Mwaramu, kaka wa Rebeka, mama yao Yakobo na Esau.
Kisha Isaki akamuaga Yakobo, naye akaenda Padan-Aramu, kwa Labani mwana wa Bethueli Mwaramu, ndugu wa Rebeka, aliyekuwa mama wa Yakobo na Esau.
6 Basi Esau alipoona kwamba Isaka amembariki Yakobo na kumpeleka Padani Aramu, kuchukua mke kutoka pale. Lakini pia akaona kwamba Isaka alikuwa amembariki na kumwagiza, akisema, “Usichukue mke katika wanawake wa Kanaani.”
Sasa Esau akajua kuwa Isaki amembariki Yakobo na kumtuma kwenda Padan-Aramu ili achukue mke huko na kwamba alipombariki alimwamuru akisema, “Usioe mke katika binti za Wakanaani,”
7 Esau pia akaona kwamba Yakobo alikuwa amemtii baba yake na mama yake, na alikuwa amekwenda Padani Aramu.
tena kwamba Yakobo amewatii baba yake na mama yake naye amekwenda Padan-Aramu.
8 Esau akaona kwamba wanawake wa Kanaani hawakumpendeza Isaka baba yake.
Esau akatambua jinsi ambavyo baba yake Isaki anavyowachukia binti za Wakanaani.
9 Hivyo akaenda kwa Ishmaeli, na kuchukua, mbali na wake aliokuwa nao, Mahalathi binti Ishmaeli, mwana wa Ibrahimu, dada wa Nebayothi, kuwa mke wake.
Ndipo Esau akaenda kwa Ishmaeli, akamwoa Mahalati, ndugu wa Nebayothi na binti wa Ishmaeli mwana wa Abrahamu, kuongezea wale wake wengine aliokuwa nao.
10 Yakobo akatoka Beersheba na akaelekea Harani.
Yakobo akatoka Beer-Sheba kwenda Harani.
11 Akaja mahali fulani na akakaa pale usiku kucha, kwa kuwa jua lilikuwa limekuchwa. Akachukua mojawapo ya mawe katika eneo hilo, akaliweka chini ya kichwa chake, na akalala usingizi katika eneo hilo.
Alipofika mahali fulani, akalala hapo kwa sababu jua lilikuwa limetua. Akachukua jiwe moja la mahali pale, akaliweka chini ya kichwa chake akajinyoosha akalala usingizi.
12 Akaota na kuona ngazi imewekwa juu ya nchi. Ncha yake ilifika hata mbinguni na malaika wa Mungu walikuwa wakishuka na kupanda juu yake.
Akaota ndoto ambayo aliona ngazi imesimamishwa juu ya ardhi, ncha yake ikiwa imefika mbinguni na malaika wa Mungu wakawa wakipanda na kushuka juu yake.
13 Tazama, Yahwe amesimama juu yake na kusema, “Mimi ni Yahwe, Mungu wa Ibrahimu baba yako, na Mungu wa Isaka. Nchi uliyolala juu yake, nitakupa wewe na uzao wako.
Juu yake alisimama Bwana, akasema, “Mimi ni Bwana, Mungu wa baba yako Abrahamu na Mungu wa Isaki. Nchi ambayo umelala juu yake, nitakupa wewe na uzao wako.
14 Uzao wako utakuwa kama mavumbi ya ardhi, na utaenea mbali kuelekea magharibi, mashariki, kaskazini, na kusini. Kupitia kwako na kupitia uzao wako familia zote za dunia zitabarikiwa.
Uzao wako utakuwa kama mavumbi ya nchi, nawe utaenea upande wa magharibi na mashariki, kaskazini na kusini. Kupitia wewe na uzao wako mataifa yote ya duniani yatabarikiwa.
15 Tazama, mimi nipo nawe, na nitakulinda kila uendako, Nitakurudisha katika nchi hii tena; kwani sitakuacha. Nitafanya kila nililokuahidi.”
Niko pamoja nawe nami nitakulinda kila uendako na nitakurudisha katika nchi hii. Sitakuacha mpaka nitakapofanya hayo niliyokuahidi.”
16 Yakobo akaamka katika usingizi, na akasema, “Hakika Yahwe yupo mahali hapa, sikujua hili.”
Yakobo alipoamka kutoka usingizini, akawaza, “Hakika Bwana yuko mahali hapa, wala mimi sikujua.”
17 Akaogopa na kusema, “Eneo hili linatisha kama nini! Hili sio kingine zaidi ya nyumba ya Mungu. Hili ni lango la mbinguni.”
Kwa hiyo akaogopa, akasema, “Mahali hapa panatisha kama nini! Bila shaka hapa ndipo nyumba ya Mungu ilipo, hili ni lango la mbinguni.”
18 Yakobo akaamka mapema asubuhi na akachukua jiwe alilokuwa ameliweka chini ya kichwa chake. Akaliweka kama nguzo na kumimina mafuta juu yake.
Asubuhi yake na mapema, Yakobo akalichukua lile jiwe aliloliweka chini ya kichwa chake, akalisimamisha kama nguzo na kumimina mafuta juu yake.
19 Akapaita pale Betheli, lakini jina la kawaida la mji lilikuwa Luzu.
Mahali pale akapaita Betheli, ingawa mji ule hapo kwanza uliitwa Luzu.
20 Yakobo akatoa nadhiri, kusema, “Ikiwa Mungu atakuwa nami na atanilinda katika njia nipitayo, na atanipa mkate wa kula, na mavazi ya kuvaa,
Kisha Yakobo akaweka nadhiri, akisema, “Kama Mungu akiwa pamoja nami na kunilinda katika safari niendayo, akinipa chakula nile na nguo nivae
21 hata nikarudi salama katika nyumba ya baba yangu, ndipo Yahwe atakapokuwa Mungu wangu.
na nirudi salama nyumbani kwa baba yangu, hapo ndipo Bwana atakuwa Mungu wangu,
22 Kisha jiwe hili nililoliweka kama nguzo litakuwa jiwe takatifu. Kutoka katika kila utakachonipa, kwa hakika nitakupa tena sehemu ya kumi.”
nalo jiwe hili nililolisimamisha kama nguzo litakuwa nyumba ya Mungu na katika yote utakayonipa nitakutolea wewe sehemu ya kumi.”

< Mwanzo 28 >