< Mwanzo 25 >

1 Abraham akaoa mke mwingine; jina lake aliitwa Ketura.
Abrahamu alioa mke mwingine, ambaye jina lake aliitwa Ketura.
2 Akamzalia Zimrani, Jokshani, Medani, Midiani, Ishbaki, na Shua.
Huyu alimzalia Zimrani, Yokshani, Medani, Midiani, Ishbaki na Shua.
3 Jokshani akamzaa Sheba na Dedani. Wana wa Dedani walikuwa ni Waashuru, Waletushi, na Waleumi.
Yokshani alikuwa baba wa Sheba na Dedani, wazao wa Dedani walikuwa Waashuri, Waletushi na Waleumi.
4 Wana wa Midiani walikuwa ni Efa, Eferi, Hanoki, Abida, na Eldaa. Hawa wote walikuwa ni wana wa Ketura.
Wana wa Midiani walikuwa Efa, Eferi, Hanoki, Abida na Eldaa. Hawa wote walikuwa uzao wa Ketura.
5 Abraham akampatia Isaka vitu vyote alivyokuwa navyo.
Abrahamu akamwachia Isaki kila kitu alichokuwa nacho.
6 Ingawaje, wakati alipokua angali akiishi, aliwapatia zawadi wana wa masuria wake na kuwapeleka katika nchi ya mashariki, mbali na Isaka, mwanae.
Lakini Abrahamu alipokuwa bado hai, akawapa watoto wa masuria wake zawadi, kisha akawaondoa waende kuishi pande za mashariki mbali na mwanawe Isaki.
7 Hizi ndizo zilikuwa siku za miaka ya uhai wake Abraham alizoishi, miaka 175.
Kwa jumla, Abrahamu aliishi miaka 175.
8 Abraham akapumua pumzi ya mwisho na akafa katika uzee mwema, mzee aliye shiba siku, na akakusanywa kwa watu wake.
Ndipo Abrahamu akapumua pumzi ya mwisho na akafa akiwa mwenye umri mzuri, mzee aliyeshiba siku, naye akakusanywa pamoja na watu wake.
9 Isaka na Ishmaili, wanae wakamzika katika pango la Makipela, katika shamba la Efron mwana wa Soari Mhiti, pango lililokuwa karibu na Mamre.
Watoto wake Isaki na Ishmaeli wakamzika katika pango la Makpela karibu na Mamre, katika shamba lililokuwa la Efroni mwana wa Sohari Mhiti,
10 Shamba hili Abraham alilinunua kwa watoto wa Hethi. Abraham akazikwa pale pamoja na Sara mkewe.
Shamba ambalo Abrahamu alilinunua kwa Wahiti. Hapo ndipo Abrahamu alipozikwa pamoja na mkewe Sara.
11 Baada ya kifo cha Abraham, Mungu akambariki Isaka mwanae, na Isaka akaishi karibu na Beerlalahairoi.
Baada ya kifo cha Abrahamu, Mungu akambariki mwanawe Isaki, ambaye baadaye aliishi karibu na Beer-Lahai-Roi.
12 Na sasa hawa ndio walikuwa wana wa Ishimaeli, mwana wa Abraham, ambaye Hajiri Mmisri mtumishi wake Sara, alizaa kwa Abraham.
Hivi ndivyo vizazi vya Ishmaeli mtoto wa Abrahamu, ambaye mjakazi wake Sara, Hagari Mmisri, alimzalia Abrahamu.
13 Haya ndiyo yalikuwa majina ya wana wa Ishimaeli, kuanzia mzaliwa wa kwanza: Nebayothi - mzaliwa wa kwanza wa Ishimaeli, Kedari, Adbeeli, Mibsamu,
Haya ndiyo majina ya wana wa Ishmaeli, yaliyoorodheshwa kulingana na jinsi walivyozaliwa: Mzaliwa wa kwanza wa Ishmaeli ni Nebayothi, akafuatia Kedari, Adbeeli, Mibsamu,
14 Mishma, Duma, Masa,
Mishma, Duma, Masa,
15 Hadadi, Tema, Yeturi, Nafishi, na Kedema.
Hadadi, Tema, Yeturi, Nafishi na Kedema.
16 Hawa ndio walikuwa wana wa Ishimaeli, na haya ndiyo majina yao, kwa vijiji vyao, na katika vituo vyao; Maseyidi kumi na wawili kufuatana na kabila zao.
Hawa walikuwa wana wa Ishmaeli na haya ni majina ya viongozi wa makabila kumi na mawili kulingana na makao yao na kambi zao.
17 Hii ndiyo ilikuwa miaka ya Ishimaeli, miaka 137: akapumua pumzi yake ya mwisho na akafa, na akakusanywa pamoja na watu wake.
Kwa jumla Ishmaeli aliishi miaka 137. Akapumua pumzi ya mwisho, akafa, naye akakusanywa pamoja na watu wake.
18 Walioshi toka Havila mpaka Shuri, ambayo iko karibu na Misri, kuelekea Ashuru. Waliishi kwa uadui kati yao.
Wazao wa Ishmaeli waliishi kuanzia nchi ya Havila hadi Shuri, karibu na mpaka wa Misri, unapoelekea Ashuru. Hao waliishi kwa uhasama na ndugu zao wote.
19 Haya ndiyo yalikuwa matukio kumuhusu Isaka, mwana wa Abraham: Abraham alimzaa Isaka.
Hivi ndivyo vizazi vya Isaki mwana wa Abrahamu. Abrahamu akamzaa Isaki,
20 Isaka alikuwa na umri wa miaka arobaini alipomuoa Rebeka, binti wa ethueli Mshami wa Padani Aramu, ndugu wa Labani Mshami.
Isaki alikuwa na umri wa miaka arobaini alipomwoa Rebeka binti Bethueli Mwaramu kutoka Padan-Aramu, nduguye Labani Mwaramu.
21 Isaka akamwomba Yahwe kwa ajili ya mke wake kwa sababu alikuwa tasa, na Yahwe akajibu maombi yake, Rebeka mkewe akabeba mimba.
Isaki akamwomba Bwana kwa ajili ya mke wake, kwa sababu alikuwa tasa. Bwana akajibu maombi yake na Rebeka mkewe akapata mimba.
22 Watoto hawa walipokuwa tumboni mwake wakasumbuka, naye akasema, “Kwa nini jambo hili linatokea kwangu mimi?” Akaenda kumuuliza Yahwe kuhusu jambo hili.
Watoto wakashindana tumboni mwake, akasema, “Kwa nini haya yanatokea kwangu?” Kwa hiyo akaenda kumuuliza Bwana.
23 Yahwe akamwambia, “Mataifa mawili yako katika tumbo lako, na mataifa haya mawili yatatengana ndani yako. Taifa moja litakuwa lenye nguvu kuliko lingine, na yule mkubwa atamtumikia mdogo.
Bwana akamjibu, “Mataifa mawili yamo tumboni mwako, na mataifa hayo mawili kutoka ndani yako watatenganishwa. Mmoja atakuwa na nguvu zaidi kuliko mwingine, na yule mkubwa atamtumikia yule mdogo.”
24 Ulipo wadia wakati wa kujifungua, tazama, kulikuwa na mapacha ndani ya tumbo lake.
Wakati wake wa kujifungua ulipotimia, walikuwepo mapacha wa kiume tumboni mwake.
25 Wakwanza akatoka akiwa mwekundu mwili wote kama vazi la nywele. Wakamwita jina lake Esau.
Wa kwanza kuzaliwa alikuwa mwekundu, mwili wake wote ulikuwa kama mtu aliyevaa vazi lenye nywele; wakamwita jina lake Esau.
26 Baada ya hapo ndugu yake akatoka. Mkono wake ukiwa umeshika kisigino cha Esau. Akaitwa jina lake Yakobo. Isaka alikuwa na umri wa miaka sitini wakati mke wake alipo wazaa hawa watoto.
Baadaye, ndugu yake akatoka, mkono wake ukiwa umemshika Esau kisigino; akaitwa jina lake Yakobo. Isaki alikuwa mwenye miaka sitini Rebeka alipowazaa.
27 Vijana hawa wakakua, Hesau akawa mwindaji hodari, mtu wa nyikani; lakini Yakobo alikuwa mtu mkimya, aliye tumia muda wake akiwa katika mahema.
Watoto wakakua, naye Esau akakuwa mwindaji hodari, mtu wa mbugani, wakati Yakobo alikuwa mtu mtulivu, mwenye kukaa nyumbani.
28 Kisha Isaka akampenda Esau kwa sababu alikula wanyama ambao alikuwa anawinda, lakini Rebeka akampenda Yakobo.
Isaki, ambaye alikuwa anapendelea zaidi nyama za porini, alimpenda Esau, bali Rebeka alimpenda Yakobo.
29 Yakobo akapika mchuzi. Esau akaja kutoka nyikani, akiwa dhaifu kutokana na njaa.
Siku moja Yakobo alipika mchuzi wa dengu, Esau akarudi kutoka porini akiwa na njaa kali.
30 Esau akamwambia Yakobo, “Nilishe mchuzi mwekundu. Tafadhari, nimechoka!” Na hii ndiyo sababu jina lake aliitwa Edomu.
Esau akamwambia Yakobo, “Haraka, nipe huo mchuzi mwekundu! Nina njaa kali sana!” (Hii ndiyo sababu pia aliitwa Edomu.)
31 Yakobo akasema, “Kwanza uniuzie haki yako ya mzaliwa wa kwanza.”
Yakobo akamjibu, “Niuzie kwanza haki yako ya mzaliwa wa kwanza.”
32 Esau akasema, “Tazama, nakaribia kufa. Ni nini kwangu haki ya mzaliwa wa kwanza?”
Esau akasema, “Tazama, mimi niko karibu ya kufa, itanifaa nini haki ya mzaliwa wa kwanza?”
33 Yakobo akasema, “Kwanza uape kwangu mimi,” kwa hiyo Esau akaapa kiapo na kwa njia hii akawa ameuza haki yake ya mzaliwa wa kwanza kwa Yakobo.
Yakobo akamwambia, “Niapie kwanza.” Hivyo Esau akamwapia, akamuuzia Yakobo haki yake ya kuzaliwa.
34 Yakobo akampatia Esau mkate pamoja na mchuzi wa dengu. Akala na kunywa, kisha akainuka na akaenda zake. Kwa njia hii Esau akawa ameidharau haki yake ya mzaliwa wa kwanza.
Ndipo Yakobo akampa Esau mkate na ule mchuzi wa dengu. Akala na kunywa, kisha akainuka akaenda zake. Kwa hiyo Esau alidharau haki yake ya mzaliwa wa kwanza.

< Mwanzo 25 >