< Mwanzo 2 >
1 Kisha mbingu na nchi zilimalizika, na viumbe hai vyote vilivyo jaza mbingu na nchi.
Kwa hiyo mbingu na dunia zikakamilika, pamoja na vyote vilivyomo.
2 Siku ya saba Mungu alifikia mwisho wa kazi yake ambayo aliifanya, na kwa hiyo alipumzika siku ya saba kutoka kwenye kazi yake yote.
Katika siku ya saba Mungu alikuwa amekamilisha kazi aliyokuwa akiifanya, hivyo siku ya saba akapumzika kutoka kazi zake zote.
3 Mungu akaibarikia siku ya saba na akaitakasa, kwa sababu katika siku hiyo alipumzika kutoka kwenye kazi yake yote ambayo aliifanya katika uumbaji.
Mungu akaibariki siku ya saba akaifanya takatifu, kwa sababu katika siku hiyo alipumzika kutoka kazi zote za kuumba alizokuwa amefanya.
4 Haya yalikuwa ni matukio yahusuyo mbingu na nchi, wakati vilipoumbwa, katika siku ambayo Yahwe Mungu aliumba nchi na mbingu.
Haya ndiyo maelezo ya mbingu na dunia wakati zilipoumbwa. Bwana Mungu alipoziumba mbingu na dunia,
5 Hapakuwa na msitu wa shambani uliokuwa katika nchi, na hapakuwa na mmea wa shambani uliokuwa umechipuka, kwa kuwa Yahwe Mungu alikuwa hajasababisha mvua kunyesha juu ya nchi, na hapakuwa na mtu wa kulima ardhi.
hapakuwepo na mche wa shambani uliokuwa umejitokeza ardhini, wala hapakuwepo na mmea wa shamba uliokuwa umeota, kwa kuwa Bwana Mungu alikuwa hajanyeshea mvua juu ya nchi, na hapakuwepo mtu wa kuilima ardhi,
6 Lakini ukungu uliinuka juu kutoka kwenye nchi na kuutia maji uso wote wa ardhi.
lakini umande ulitokeza kutoka ardhini na kunyesha uso wote wa nchi:
7 Yahwe Mungu aliumba mtu kutoka mavumbi ya ardhi, na akampulizia puani pumzi ya uhai, na mtu akawa kiumbe hai.
Bwana Mungu alimuumba mtu kutoka mavumbi ya ardhi, akampulizia pumzi ya uhai puani mwake, naye mtu akawa kiumbe hai.
8 Yahwe Mungu aliotesha bustani upande wa mashariki, katika Edeni, na pale akamuweka mtu ambaye alimuumba.
Basi Bwana Mungu alikuwa ameotesha bustani upande wa mashariki, katika Edeni, huko akamweka huyo mtu aliyemuumba.
9 Kutoka ardhini Yahwe Mungu alifanya kila mti uote ambao unapendeza na ni mzuri kwa chakula. Hii ni pamoja na mti wa uzima ambao ulikuwa katikati ya bustani, na mti wa ujuzi wa mema na mabaya.
Bwana Mungu akafanya aina zote za miti ziote kutoka ardhini, miti yenye kupendeza macho na mizuri kwa chakula. Katikati ya bustani ulikuwepo mti wa uzima na mti wa kujua mema na mabaya.
10 Mto ukatoka nje ya Edeni kuitia maji bustani. Na kutoka pale ukagawanyika na kuwa mito minne.
Mto wa kunyeshea bustani ulitiririka toka Edeni, kuanzia hapa ukagawanyika kuwa mito minne.
11 Jina la ule wa kwanza ni Pishoni. Huu ni ule ambao unatiririka kupitia nchi yote ya Havila, ambapo kuna dhahabu.
Mto wa kwanza uliitwa Pishoni, nao huzunguka nchi yote ya Havila ambako kuna dhahabu.
12 Dhahabu ya inchi ile ni nzuri. pia kuna bedola na jiwe shohamu.
(Dhahabu ya nchi hiyo ni nzuri, bedola na vito shohamu pia hupatikana huko.)
13 Jina la mto wa pili ni Gihoni. Huu unatiririka kupitia nchi yote ya kushi.
Jina la mto wa pili ni Gihoni, ambao huzunguka nchi yote ya Kushi.
14 Jina la mto wa tatu ni Hidekeli, ambao unatiririka mashariki mwa Ashuru. Mto wa nne ni Frati.
Jina la mto wa tatu ni Tigrisi, unaopita mashariki ya Ashuru. Mto wa nne ni Frati.
15 Yahwe Mungu alimtwaa mtu na kumweka ndani ya bustani ya Edeni kuilima na kuitunza.
Bwana Mungu akamchukua huyo mtu, akamweka kwenye Bustani ya Edeni ailime na kuitunza.
16 Yahwe Mungu alimuagiza mtu akisema, “kutoka kwenye kila mti bustanini waweza kula kwa uhuru.
Bwana Mungu akamwagiza huyo mtu, akamwambia, “Uko huru kula matunda ya mti wowote katika bustani,
17 Lakini kutoka kwenye mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa kuwa siku utakayo kula kutoka katika mti huo, utakufa hakika.”
lakini kamwe usile matunda ya mti wa kujua mema na mabaya, kwa maana siku utakapokula matunda yake, hakika utakufa.”
18 Kisha Yahwe Mungu akasema, “siyo jambo jema kwamba mtu huyu lazima awe pekeyake. Nitamfanyia msaidizi anaye mfaa.”
Bwana Mungu akasema, “Si vyema huyu mtu awe peke yake. Nitamfanyia msaidizi wa kumfaa.”
19 Kutoka ardhini Yahwe Mungu akafanya kila mnyama wa kondeni na kila ndege wa angani. Kisha akawaleta kwa mtu huyu aone angewapatia majina gani. Jina ambalo mtu huyu alimwita kila kiumbe hai, hili ndilo lilikuwa jina lake.
Basi Bwana Mungu alikuwa amefanyiza kutoka ardhi wanyama wote wa porini na ndege wote wa angani. Akawaleta kwa huyu mtu aone atawaitaje, nalo jina lolote alilokiita kila kiumbe hai, likawa ndilo jina lake.
20 Mtu huyu akawapatia majina wanyama wote, ndege wote wa angani, na kila mnyama wa mwitu. Lakini kwa mtu mwenyewe hapakuwa na msaidizi wa kumfaa yeye.
Hivyo Adamu akawapa majina wanyama wote wa kufugwa, ndege wa angani, na wanyama wote wa porini. Lakini kwa Adamu hakupatikana msaidizi wa kumfaa.
21 Yahwe Mungu akaleta usingizi mzito kwa mtu huyu, kwa hiyo mtu huyu akalala. Yahwe Mungu akatwaa moja ya mbavu za mtu huyu na akapafunika pale alipo chukua ubavu.
Hivyo Bwana Mungu akamfanya Adamu kulala usingizi mzito, naye alipokuwa amelala akachukua moja ya mbavu zake, akapafunika mahali pale kwa nyama.
22 Kwa ubavu ambao Yahwe Mungu alichukua toka kwa mtu huyu, akafanya mwanamke na akamleta kwa mtu huyu.
Kisha Bwana Mungu akamfanya mwanamke kutoka kwenye ule ubavu aliouchukua kutoka kwa huyo mwanaume, akamleta huyo mwanamke kwa huyo mwanaume.
23 Mwanaume akasema, “kwa sasa, huyu ni mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu. ataitwa 'mwanamke,' kwa sababu ametwaliwa katika mwanaume.
Huyo mwanaume akasema, “Huyu sasa ni mfupa wa mifupa yangu na nyama ya nyama yangu, ataitwa ‘mwanamke,’ kwa kuwa alitolewa katika mwanaume.”
24 Kwa hiyo mwanaume atawaacha baba yake na mama yake, ataungamanika na mke wake, na watakuwa mwili mmoja.
Kwa sababu hii mwanaume atamwacha baba yake na mama yake na kuambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja.
25 Wote wawili walikuwa uchi, mwanaume na mke wake, lakini hawakuona aibu.
Adamu na mkewe wote wawili walikuwa uchi, wala hawakuona aibu.