< Mwanzo 19 >

1 Malaika wawili wakaja Sodoma jioni, wakati ambao Lutu alikuwa amekaa langoni mwa Sodoma. Lutu akawaona, akainuka kuwalaki, na akainama uso wake chini ardhini.
Malaika wale wawili wakafika Sodoma wakati wa jioni, naye Loti alikuwa ameketi kwenye lango la mji. Wakati alipowaona, aliondoka kwenda kuwalaki na kuwasujudia hadi chini.
2 Akasema, Tafadhari Bwana zangu, nawasihi mgeuke mwende kwenye nyumba ya mtumishi wenu, mlale pale usiku na muoshe miguu yenu. Kisha muamke asubuhi na mapema muondoke.” Nao wakasema, “Hapana, usiku tutalala mjini.”
Akasema, “Bwana zangu, tafadhali karibuni kwenye nyumba ya mtumishi wenu. Mnaweza kunawa miguu na kulala hapa kisha asubuhi na mapema mwendelee na safari yenu.” Wakamjibu, “La hasha, tutalala hapa nje uwanjani.”
3 Lakini akawasihi sana, mwishowe wakaondoka pamoja nae, na wakaingia katika nyumba yake. Akaandaa chakula na kuoka mkate usiotiwa chachu, wakala.
Lakini akasisitiza kwa nguvu kwamba waingie pamoja naye nyumbani kwake. Akawaandalia chakula, mikate isiyotiwa chachu, nao wakala.
4 Lakini kabla hawaja lala, wanaume wa mji, wa Sodoma, vijana kwa wazee wakaizunguka nyumba, wanaume wote kutoka kila kona ya mji.
Kabla hawajaenda kulala, watu wote kutoka kila sehemu ya mji wa Sodoma, vijana kwa wazee, waliizunguka nyumba.
5 Wakamwita Lutu, na kumwambia, “Wale wanaume walioingia kwako usiku wakowapi? watoe hapa nje waje kwetu, ili tuweze kulala nao.”
Wakamwita Loti wakisema, “Wako wapi wale watu ambao walikuja kwako jioni hii? Watoe nje kwetu ili tuweze kuwalawiti.”
6 Lutu akatoka nje na akafunga mlango.
Loti akatoka nje kuonana nao, akaufunga mlango nyuma yake,
7 Akasema, “Nawasihi, ndugu zangu, msitende uovu.
akasema, “La hasha, rafiki zangu. Msifanye jambo hili ovu.
8 Tazama, nina mabinti wawili ambao hawajawahi kulala na mwanaume yeyote. Nawaomba tafadhari niwalete kwenu, na muwafanyie lolote muonalo kuwa jema machoni penu. Msitende lolote kwa wanaume hawa, kwa kuwa wamekuja chini ya kivuli cha dari yangu.”
Tazama, ninao binti wawili ambao kamwe hawajakutana kimwili na mwanaume. Acha niwatoe nje kwenu, nanyi mnaweza kuwafanyia lolote mnalotaka. Lakini msiwafanyie chochote watu hawa, kwa sababu wako kwenye ulinzi chini ya dari langu.”
9 Wakasema, “Ondoka hapa!” Wakasema pia, huyu alikuja kukaa hapa kama mgeni, na sasa amekuwa mwamuzi! Sasa tutakushugulilia vibaya wewe kuliko wao.” Wakamsonga sana huyo mtu, huyo Lutu, na wakakaribia kuvunja mlango.
Wakamjibu, “Tuondokee mbali.” Wakaendelea kusema, “Huyu mtu alikuja hapa kama mgeni na sasa anataka kuwa mwamuzi wetu! Tutakutenda vibaya kuliko wao.” Waliendelea kumlazimisha Loti na kusonga mbele ili kuvunja mlango.
10 Lakini wale wanaume wakamkamata Lutu na kumweka ndani na wakafunga mlango.
Lakini watu wale waliokuwa ndani wakanyoosha mkono wakamvuta Loti ndani ya nyumba na kufunga mlango.
11 Kisha wale wageni wa Lutu wakawapiga kwa upofu wale wanaume waliokuwa nje ya nyumba, vijana na wazee kwa pamoja, kiasi kwamba wakachoka wakati wakiutafuta mlango.
Kisha wakawapiga kwa upofu wale watu waliokuwa mlangoni mwa ile nyumba, vijana kwa wazee, hivyo hawakuweza kuupata mlango.
12 Basi wale watu wakamwambia Lutu, Je una mtu mwingine yeyote hapa? wakwe zako, wanao na mabinti zako, na yeyote mwingine katika huu mji, ukawatoe hapa.
Wale watu wawili wakamwambia Loti, “Una mtu mwingine yeyote hapa, wakwe zako, wana au binti, ama yeyote mwingine aliye wako katika mji huu? Waondoe hapa,
13 Kwa kuwa tunakaribia kuiangamiza sehemu hii, kwa sababu mashitaka dhidi yake mbele ya Yahwe yamezidi kiasi kwamba ametutuma kuuangamiza.”
kwa sababu tunapaangamiza mahali hapa. Kilio kwa Bwana dhidi ya watu wa hapa ni kikubwa kiasi kwamba ametutuma kupaangamiza.”
14 Lutu akatoka na akazungumza na wakwe zake, wanaume ambao walikuwa wamewaposa binti zake, akawambia, “Ondokeni upesi mahali hapa, kwa kuwa Yahwe anakaribia kuuangamiza mji.” Lakini kwa wakwe zake alionekana kuwa anawatania.
Kwa hiyo Loti alitoka ili kuzungumza na wakwe zake, waliokuwa wamewaposa binti zake. Akawaambia, “Fanyeni haraka kuondoka mahali hapa, kwa kuwa Bwana yu karibu kuangamiza mji huu!” Lakini wakwe zake walifikiri kwamba alikuwa akitania.
15 Alfajiri, malaika wakamsihi Lutu, wakisema, ondoka, mtwae mkeo na binti zako wawili ambao wako hapa, ili kwamba usipotelee katika adhabu ya mji huu.”
Kunako mapambazuko, malaika wakamhimiza Loti, wakamwambia, “Fanya haraka! Mchukue mke wako na binti zako wawili walioko hapa, la sivyo utaangamizwa wakati mji utakapoadhibiwa.”
16 Lakini akakawia-kawia. Kwa hiyo watu wale wakamshika mkono wake, na mkono wa mkewe, na mikono ya binti zake wawili, kwa sababu Yahwe alimhurumia. Wakawatoa nje, na kuwaweka nje ya mji.
Alipositasita, wale watu wakamshika mkono wake na mikono ya mke wake na binti zake wawili na kuwaongoza salama nje ya mji, kwa kuwa Bwana alikuwa na huruma kwao.
17 Wakisha kuwatoa nje mmoja wa wale watu akasema, “jiponye nafsi yako! usitazame nyuma, au usikae mahali popote kwenye hili bonde. Toroka uende milimani ili kwamba usije ukatoweshwa mbali.”
Mara walipokwisha kuwatoa nje, mmoja wao akawaambia, “Mkimbie kwa usalama wenu! Msitazame nyuma, wala msisimame popote katika nchi tambarare! Kimbilieni milimani, ama sivyo mtaangamizwa!”
18 Lutu akawambia, “Hapana, tafadhali bwana zangu!
Lakini Loti akawajibu, “La hasha, bwana zangu, tafadhalini!
19 Mtumishi wenu amepata kibali machoni pako, na umenionesha wema ulio mkuu kwa kuokoa maisha yangu, lakini sitaweza kutorokea milimani, kwa sababu mabaya yataniwahi na nitakufa.
Mtumishi wenu amepata kibali mbele ya macho yenu, nanyi mmeonyesha wema mkubwa kwangu kwa kuokoa maisha yangu. Lakini siwezi kukimbilia milimani, janga hili litanikumba, nami nitakufa.
20 Tazama, ule mji pale uko karibu nijisalimishe pale, na ni mdogo. Tafadhari niacheni nikimbilie pale ( Je Siyo mdogo ule?), na maisha yangu yataokolewa.”
Tazama, hapa kuna mji karibu wa kukimbilia, nao ni mdogo. Niruhusuni nikimbilie humo, ni mdogo sana, ama sivyo? Ndipo maisha yangu yatasalimika.”
21 Akamwambia, “Sawa, nimekubali ombi hili pia, kwamba sitaangamiza mji ambaoumeutaja.
Akamwambia, “Vema sana, nitalikubali hili ombi pia, sitauangamiza mji ulioutaja.
22 Harakisha! toroka uende pale, kwa kuwa sitafanya chochote mpaka ufike pale.” kwa hiyo mji ule ukaitwa Soari.
Lakini ukimbilie huko haraka, kwa sababu sitaweza kufanya lolote mpaka ufike huko.” (Ndiyo maana mji huo ukaitwa Soari.)
23 Jua lilikuwa limekwisha chomoza juu ya nchi wakati Lutu alipofika Soari.
Wakati Loti alipofika Soari, jua lilikuwa limechomoza katika nchi.
24 Kisha Yahwe akanyesha juu ya Sodoma na Gomora kiberiti na moto toka kwa Yahwe mbinguni.
Ndipo Bwana akanyesha moto wa kiberiti uliotoka mbinguni kwa Bwana juu ya Sodoma na Gomora.
25 Akaharibu miji ile, na bonde lote, na vyote vilivyomo katika miji, na mimea iliyo chipua juu ya ardhi.
Hivyo akaiteketeza miji ile na eneo lote la tambarare, pamoja na wote waliokuwa wanaishi katika miji, hata pia mimea yote katika nchi.
26 Lakini mke wa Lutu aliye kuwa nyuma yake, akatazama nyuma, na akawa nguzo ya chumvi.
Lakini mke wa Loti akatazama nyuma, hivyo akawa nguzo ya chumvi.
27 Abraham akaamuka asubuhi na mapema akaenda mahali alipokuwa amesimama mbele ya Yahwe.
Asubuhi na mapema siku iliyofuata, Abrahamu akaamka na kurudi mahali pale aliposimama mbele za Bwana.
28 Akatazama chini kuelekea Sodoma na Gomora na kuelekea katika nchi yote bondeni. Akaona na tazama, moshi ulikuwauki ukienda juu kutoka chini kama moshi wa tanuru.
Akatazama upande wa Sodoma na Gomora, kuelekea nchi yote ya tambarare, akaona moshi mzito ukipanda kutoka kwenye nchi, kama moshi utokao kwenye tanuru.
29 Wakati Mungu alipoharibu miji ya bondeni, Mungu akamkumbuka Abraham. Akamtoa Lutu kutoka katika maangamizi alipoangamiza miji ambayo katika hiyo Lutu aliishi.
Kwa hiyo Mungu alipoiangamiza miji ya tambarare alimkumbuka Abrahamu, akamtoa Loti kutoka kwenye lile janga lililoharibu miji ile ambamo Loti alikuwa ameishi.
30 Lakini Lutu akapanda juu kutoka Soari na kwenda kuishi katika milima akiwa pamoja na binti zake wawili, kwa sababu aliogopa kuishi Soari. Kwa hiyo akaishi pangoni, yeye na binti zake wawili.
Loti na binti zake wawili waliondoka Soari na kufanya makao yao kule milimani, kwa maana aliogopa kukaa Soari. Yeye na binti zake wawili waliishi katika pango.
31 Yule wa kwanza akamwambia yule mdogo, “Baba yetu ni mzee, na hakuna mwanaume mahali popote wa kulala na sisi kulingana na desturi ya dunia yote.
Siku moja binti mkubwa akamwambia yule mdogo, “Baba yetu ni mzee na hakuna mwanaume mahali hapa atakayekutana na sisi kimwili, kama ilivyo desturi ya mahali pote duniani.
32 Njoo na tumnyweshe baba yetu mvinyo na tulale naye ili kwamba tuendeleze uzao wa baba yetu.”
Tumnyweshe baba yetu mvinyo kisha tukutane naye kimwili ili tuhifadhi uzao wetu kupitia baba yetu.”
33 Kwa hiyo wakamnywesha baba yako mvinyo usiku ule. Kisha yule wa kwanza akaingia na akalala na baba yake; Baba yake hakujua ni wakati gani alikuja kulala, wala wakati alipo amka.
Usiku ule walimnywesha baba yao mvinyo, alipolewa binti yake mkubwa akaingia na kukutana naye kimwili. Baba yao hakujua wakati binti yake alipoingia kulala naye wala alipotoka.
34 Siku iliyo fuata yule wa kwanza akamwambia mdogowake, “Sikiliza, usiku wa jana nililala na baba yangu. Na tumnyweshe mvinyo usiku wa leo pia, na uingie ukalale naye. Ili kwamba tuendeleze uzao wa baba yetu.”
Siku iliyofuata binti mkubwa akamwambia yule mdogo, “Usiku uliopita mimi nilikutana kimwili na baba yangu. Tumnyweshe divai tena, usiku huu nawe ukutane naye kimwili ili tuweze kuhifadhi uzao wetu kupitia baba yetu.”
35 Kwa hiyo wakamnywesha baba yao mvinyo usiku ule pia, na yule mdogo akaenda na akalala naye. Baba yake hakujua ni wakati gani alilala, wala wakati alipoamka.
Kwa hiyo wakamnywesha baba yao mvinyo tena usiku ule, naye binti yake mdogo akaingia, akakutana naye kimwili. Kwa mara nyingine baba yao hakujua binti yake alipolala naye wala alipoondoka.
36 Basi hao binti wote wawili wa Lutu wakapata mimba kwa baba yao.
Hivyo binti wawili wa Loti wakapata mimba kwa baba yao.
37 Wa kwanza akazaa mwana wa kiume, na akamwita jina lake Moabu. Akawa ndiye baba wa wamoabu hata leo.
Binti mkubwa akamzaa mwana, akamwita jina lake Moabu; ndio baba wa Wamoabu hata leo.
38 Nayule mdogo naye akazaa mwana wa kiume, na akamwita Benami. Huyu ndiye baba wa watu wa Waamoni hata leo.
Binti mdogo naye pia akamzaa mwana, naye akamwita Benami; ndiye baba wa Waamoni hata leo.

< Mwanzo 19 >