< Mwanzo 15 >
1 Baada ya mabo haya neno la Yahwe likamjia Abram katika maono, likisema, “Usiogope, Abram! mimi ni ngao yako na thawabu yako kubwa sana.”
2 Abram akasema, “Bwana Yahwe, utanipatia nini, kwa kuwa naenda bila mtoto, na mrithi wa nyumba yangu ni Eliezeri wa Dameski?”
3 Abram akasema, “Kwakuwa hujanipatia uzao, tazama, mwangalizi wa nyumba yangu ndiye mrithi wangu.”
4 Kisha, tazama, neno la Yahwe likaja kwake, kusema, “Mtu huyu hatakuwa mrithi wako; isipokuwa atakaye toka katika mwili wako ndiye atakuwa mrithi wako.”
5 Kisha akamtoa nje, na akasema, Tazama mbinguni, na uzihesabu nyota, ikiwa unaweza kuzihesabu.” Kisha akamwambia, hivyo ndivyo uzao wako utakavyokuwa.
6 Akamwamini Yahwe, na akamuhesabia jambo hili kuwa mwenye haki.
7 Akamwambia, Mimi ni Yahwe, niliye kutoa katika Uru ya Wakaldayo, na kukupatia nchi hii kuirithi.”
8 Akasema, “Bwana Yahwe, nitajua je kuwa nitairithi?”
9 Kisha akamwambia, “Nipatie ndama wa umri wa miaka mitatu, mbuzi mke wa umri wa miaka mitatu, na kondoo mume wa umri wa miaka mitatu, na njiwa na mwana njiwa.”
10 Akamletea hivi vyote, akavipasua katika sehemu mbili, akaweka kila kipande kuelekea mwenzake, ila ndege hakuawapasua.
11 Wakati ndege walipokuja juu ya mizoga, Abram akawafukuza.
12 Kisha wakati jua lilipokuwa likizama, Abram akalala usingizi mzito na tazama, hofu ya giza kuu ikamfunika.
13 Kisha Yahwe akamwambia Abram, “Ujuwe kwa hakika kwamba uzao wako watakuwa wageni katika nchi ambayo si ya kwao, na watatumikishwa na kuteswa kwa miaka mia nne.
14 Nitahukumu taifa ambalo watalitumikia, na baadye watatoka wakiwa na mali nyingi.
15 Lakini utakwenda kwa baba zako kwa amani, na utazikwa katika uzee mwema.
16 Katika kizazi cha nne watakuja tena hapa, kwa sababu uovu wa Waamori haujafikia mwisho wake.”
17 Jua lilipokuwa limezama na kuwa giza, tazama, chungu cha moshi wenye moto na miali ya mwanga ilipita kati ya vile vipande.
18 Siku hiyo Yahwe akafanya agano na Abram, akisema, “Ninatoa nchi hii kwa uzao wako, kutoka mto wa Misri hadi kwenye mto mkuu, Frati -
19 Mkeni, Mkenizi, na Mkadmoni,
20 Mhiti, Mperizi, Mrefai,
21 Mwamori, Mkanaani, Mgirgashi, na Myebusi.