< Mwanzo 14 >

1 Ikiwa katika siku za Amrafeli, mfalme wa shinari, Arioko, mfalme wa Elasari, Kedorlaoma, mfalme wa Elam na Tidali, mfalme wa Goimu,
Wakati huu Amrafeli mfalme wa Shinari, Arioko mfalme wa Elasari, Kedorlaoma mfalme wa Elamu, na Tidali mfalme wa Goimu
2 walifanya vita dhidi ya Bera mfalme wa Sodoma, Birsha, mfalme wa Gomora, Shinabu, mfalme wa Adma, Shemeberi, mfalme wa Seboim, na mfalme wa Bela(pia ikiitwa Soari).
kwa pamoja walikwenda kupigana vita dhidi ya Bera mfalme wa Sodoma, Birsha mfalme wa Gomora, Shinabu mfalme wa Adma, Shemeberi mfalme wa Seboimu, na mfalme wa Bela (yaani Soari).
3 Hawa wafalme watano wa mwisho waliungana pamoja katika bonde la Sidim (pia likiitwa bahari ya chumvi).
Hawa wote waliotajwa mwishoni waliunganisha majeshi yao kutoka Bonde la Sidimu (yaani Bahari ya Chumvi).
4 Kwa miaka kumi na mbili walimtumikia Kedorlaoma, lakini katika mwaka wa kumi na tatu waliasi.
Walikuwa wametawaliwa na Mfalme Kedorlaoma kwa miaka kumi na miwili, lakini mwaka wa kumi na tatu waliasi.
5 Kisha katika mwaka wa kumi na nne, Kedorlaoma na wafalme waliokuwa pamoja nae walikuja na kuwashambulia Warefai katika Ashteroth Karnaimu, na Wazuzi katika Hamu, Waemi katika Shawe Kiriathaimu,
Mnamo mwaka wa kumi na nne, Mfalme Kedorlaoma na wafalme waliojiunga naye walikwenda kupigana na kuwashinda Warefai katika Ashtaroth-Kanaimu, Wazuzi katika Hamu, Waemi katika Shawe-Kiriathaimu,
6 na Wahori katika mlima wao wa Seiri, mpaka El Parani iliyo karibu na jangwa.
na Wahori katika nchi ya kilima cha Seiri, hadi El-Parani karibu na jangwa.
7 Kisha wakarudi wakaja En Misifati (Pia ikiitwa Kadeshi), na kuishinda nchi yote ya Waamaleki, na pia Waamori ambao waliishi Hasasoni Tamari.
Kisha wakarudi wakaenda En-Misfati (yaani Kadeshi), wakashinda nchi yote ya Waamaleki, pamoja na Waamori waliokuwa wakiishi Hasason-Tamari.
8 Kisha mfalme wa Sodoma, mfalme wa Gomora, mfalme wa Adma, mfalme wa Seboim, na mfalme wa Bela (pia ikiitwa Soari) walikwenda na kuandaa vita
Ndipo mfalme wa Sodoma, mfalme wa Gomora, mfalme wa Adma, mfalme wa Seboimu, na mfalme wa Bela (yaani Soari) wakatoka kupanga majeshi yao kwenye Bonde la Sidimu
9 dhidi ya Kadorlaoma, mfalme wa Elam, Tidali mfalme wa Goim, Amrafeli, mfalme wa Shinari, Arioki, mfalme wa Elasari; wafme wanne dhidi ya wale watano.
dhidi ya Kedorlaoma, mfalme wa Elamu, Tidali mfalme wa Goimu, Amrafeli mfalme wa Shinari, na Arioko mfalme wa Elasari, yaani wafalme wanne dhidi ya wafalme watano.
10 Na sasa bonde la Sidimu lilikuwa limejaa mashimo ya lami, na wafalme wa Sodoma na Gomora walipokimbia, wakaanguka pale. Wale waliosalia wakakimbilia milimani.
Basi Bonde la Sidimu lilikuwa limejaa mashimo ya lami, nao wafalme wa Sodoma na wa Gomora walipokimbia, baadhi ya watu walitumbukia huko na wengine wakakimbilia vilimani.
11 Kwa hiyo adui akachukua mali zote za Sodoma na Gomora na vyakula vyao vyote, na wakaenda zao,
Wale wafalme wanne wakateka mali yote ya Sodoma na Gomora pamoja na vyakula vyao vyote, kisha wakaenda zao.
12 walipoondoka, wakamchukua pia Lutu, mtoto wa ndugu yake na Abram ambaye aliishi Sodoma, pamoja na mali zake zote.
Pia walimteka Loti mwana wa ndugu yake Abramu pamoja na mali zake, kwa kuwa alikuwa akiishi Sodoma.
13 Mmoja ambaye alitoroka alikuja na kumwambia Abram mwebrania. Alikuwa anaishi katika mialoni ya Mamre, mwamori ambaye alikuwa ni ndugu wa Eshkoli na Aneri ambao walikuwa washirika wa Abram.
Mtu mmoja aliyekuwa ametoroka akaja kumpa Abramu Mwebrania taarifa. Wakati huu Abramu alikuwa anaishi karibu na mialoni ya Mamre Mwamori, aliyekuwa ndugu yake Eshkoli na Aneri, ambao wote walikuwa wameungana na Abramu.
14 Abram aliposikia kuwa maadui wamemteka ndugu yake, akawaongoza wanaume waliofunzwa na kuzaliwa nyumbani mwake 318 na akawaongoza hadi Dani.
Abramu alipopata habari kwamba jamaa yake amechukuliwa mateka, akawaita watu 318 wa nyumbani mwake waliokuwa wamefunzwa kupigana vita, wakawafuatilia hadi Dani.
15 Akawagawanya watu wake dhidi yao usiku na kuwavamia, na kuwafukuza mpaka Hoba, ambayo iko kaskazini mwa Dameski.
Wakati wa usiku Abramu aliwagawa watu wake katika vikosi ili awashambulie, na akawafuatilia, akawafukuza hadi Hoba, kaskazini ya Dameski.
16 Kisha akarudisha mali zote, pia akamrudisha ndugu yake Lutu na mali zake, pamoja na wanawake na watu wengine.
Akarudisha mali zote, na akamrudisha Loti jamaa yake na mali zake, pamoja na wanawake na watu wengine.
17 Baada ya Abram kurudi kutoka kumpiga Kadorlaoma na wafalme waliokuwa pamoja nae, mfalme wa Sodoma akatoka kuonana nae katika bonde la Shawe (pia iliitwa bonde la mfalme).
Abramu aliporudi baada ya kumshinda Mfalme Kedorlaoma na wale wafalme waliojiunga naye, mfalme wa Sodoma akatoka kwenda kumlaki katika Bonde la Shawe (yaani Bonde la Mfalme).
18 Melkizedeki, mfalme wa Salem, akaleta mkate na divai. Alikuwa ni kuhani wa Mungu aliye juu sana.
Ndipo Melkizedeki mfalme wa Salemu alipoleta mkate na divai. Alikuwa kuhani wa Mungu Aliye Juu Sana.
19 Alimbariki akisema, “Abarikiwea Abram na Mungu aliye juu sana, muumba wa mbingu na nchi.
Naye akambariki Abramu, akisema, “Abarikiwe Abramu na Mungu Aliye Juu Sana, Muumba wa mbingu na nchi.
20 Abarikiwe Mungu aliye juu sana, ambaye amekupatia adui zako katika mikono yako.” Kisha Abram akampatia sehemu ya kumi ya kila kitu.
Abarikiwe Mungu Aliye Juu Sana, ambaye amewaweka adui zako mkononi mwako.” Ndipo Abramu akampa Melkizedeki sehemu ya kumi ya kila kitu.
21 Mfalme wa Sodama akamwambia Abram, “Nipatie watu, na ujichukulie wewe mwenyewe mali.”
Mfalme wa Sodoma akamwambia Abramu, “Nipe hao watu na hizo mali uchukue wewe mwenyewe.”
22 Abram akamwambia mfalme wa Sodoma, “Nimeinua juu mkono wangu kwa Yahwe, Mungu aliye juu sana, muumbaji wa mbingu na nchi,
Lakini Abramu akamwambia mfalme wa Sodoma, “Nimeinua mkono wangu kwa Bwana, Mungu Aliye Juu Sana, Muumba wa mbingu na dunia, na nimeapa
23 kwamba sitachukua uzi wala gidamu ya kiatu, au kitu chochote ambacho ni chako, 'ili kwamba usiseme, nimemfanya Abram kuwa tajiri.'
kwamba sitapokea kitu chochote kilicho chako, hata kama ni uzi au gidamu ya kiatu, ili kamwe usije ukasema, ‘Nimemtajirisha Abramu.’
24 Sitachukua chochote isipokuwa kile ambacho vijana wamekula na sehemu za watu waliokwenda nami. Aneri, Eskoli, na Mamre na wachukue sehemu zao.”
Sitapokea chochote, ila kile tu watu wangu walichokula na sehemu ambayo ni fungu la watu waliokwenda pamoja nami, ambao ni Aneri, Eshkoli na Mamre. Wao na wapewe fungu lao.”

< Mwanzo 14 >