< Mwanzo 12 >

1 Kisha Yahwe akamwambia Abram, “Nenda utoke katika nchi yako, na toka kwa ndugu zako, na kwa jamaa za baba yako, uende katika nchi nitakayo kuonesha.
Bwana akawa amemwambia Abramu, “Ondoka kutoka nchi yako, uache jamii yako na nyumba ya baba yako, uende hadi nchi nitakayokuonyesha.
2 Nitakufanya uwe taifa kubwa, na nitakubariki na kulifanya jinalako kuwa kubwa, na utafanyika baraka.
“Mimi nitakufanya taifa kubwa na nitakubariki, Nitalikuza jina lako, nawe utakuwa baraka.
3 Nitawabariki wakubarikio, lakini asiye kuheshimu nita mlaani. Kupitia kwako familia zote za nchi zitabarikiwa.
Nitawabariki wale wanaokubariki, na yeyote akulaaniye nitamlaani; na kupitia kwako mataifa yote duniani yatabarikiwa.”
4 Kwa hiyo Abram akaondoka kama vile Yahwe alivyo mwambia kufanya, na Lutu akaenda pamoja naye. Abram alikuwa na miaka sabini na mitano wakati alipotoka Harani.
Hivyo Abramu akaondoka kama Bwana alivyokuwa amemwambia; naye Loti akaondoka pamoja naye. Wakati Abramu alipoitwa aondoke Harani, alikuwa na miaka sabini na mitano.
5 Abram akamchukua Sarai mkewe, Lutu, mtoto wa ndugu yake, na vyote walivyomiliki ambavyo wamevikusanya, na watu ambao wamewapata wakiwa huko Harani. Wakatoka kwenda katika nchi ya Kanaani, wakafika nchi ya Kanaani.
Abramu akamchukua Sarai mkewe pamoja na Loti mwana wa ndugu yake, mali zote walizokuwa nazo pamoja na watu aliokuwa amewapata huko Harani, wakasafiri mpaka nchi ya Kanaani, wakafika huko.
6 Abram akapitia katikati ya nchi hadi Shekemu, hadi mwaloni wa More. Wakati huo wakanaani waliishi katika nchi hiyo.
Abramu akasafiri katika nchi hiyo akafika huko Shekemu, mahali penye mti wa mwaloni ulioko More. Wakati huo Wakanaani walikuwa wanaishi katika nchi hiyo.
7 Yahwe akamtokea Abram, na kusema, “Nitawapa uzao wako nchi hii.” Kwa hiyo Abram akamjengea madhabahu, Yahwe ambaye alimtokea.
Bwana akamtokea Abramu, akamwambia, “Nitawapa uzao wako nchi hii.” Hivyo hapa akamjengea madhabahu Bwana aliyekuwa amemtokea.
8 Kutoka pale akaenda kwenye nchi ya mlima mashariki mwa Betheli, ambapo alipiga hema yake, magaribi kukiwa na Betheli na mashariki kukiwa na mji wa Ai. Akajenga madhabahu ya Yahwe pale na kuliitia jina la Yahwe.
Kutoka huko Abramu akasafiri kuelekea kwenye vilima mashariki ya Betheli, naye akapiga hema huko, Betheli ikiwa upande wa magharibi na Ai upande wa mashariki. Huko alimjengea Bwana madhabahu na akaliitia jina la Bwana.
9 Kisha Abram akaendelea kusafiri, akielekea upande wa Negebu.
Kisha Abramu akasafiri kuelekea upande wa Negebu.
10 Kulikuwa na njaa katika nchi, kwa hiyo Abram akaenda kukaa Misri, kwa kuwa njaa ilikua kali katika nchi.
Basi kulikuwako na njaa katika nchi, naye Abramu akashuka kwenda Misri kukaa huko kwa muda, kwa maana njaa ilikuwa kali.
11 Wakati alipokaribia kuingia Misri, akamwambia Sarai mkewe, “tazama, najua kuwa wewe ni mwanamke mzuri.
Alipokuwa karibu kuingia Misri, akamwambia Sarai mkewe, “Ninajua ya kwamba wewe ni mwanamke mzuri wa sura.
12 Wamisri watakapokuona watasema, huyu ni mke wake, na wataniua mimi, lakini watakuacha wewe hai.
Wakati Wamisri watakapokuona, watasema, ‘Huyu ni mke wake.’ Ndipo wataniua, lakini wewe watakuacha hai.
13 Hivyo wewe sema kuwa ni dada yangu, ili kwamba niwe salama kwa sababu yako, na kumba maisha yangu yatasalimika kwa sababu yako.”
Sema wewe ni dada yangu, ili nitendewe mema kwa ajili yako, na maisha yangu yatahifadhiwa kwa sababu yako.”
14 Ikawa kwamba Abram alipoingia Misri, Wamisri wakaona kwamba Sarai ni mzuri sana.
Abramu alipoingia Misri, Wamisri wakamwona Sarai kuwa ni mwanamke mzuri sana wa sura.
15 Wakuu wa Farao wakamuona, na kumsifia kwa Farao, na huyu mwanamke akachukuliwa kupelekwa nyumbani mwa Farao.
Maafisa wa Farao walipomwona, wakamsifia kwa Farao; ndipo Sarai akapelekwa kwa nyumba ya mfalme.
16 Farao akamtendea kwa wema Abram kwa ajili yake, na akampatia kondoo, maksai, punda waume watumishi wa kiume, watumishi wa kike, punda wake, na ngamia.
Kwa ajili ya Sarai, Farao akamtendea Abramu mema, naye Abramu akapata kondoo, ngʼombe, punda, ngamia na watumishi wa kiume na wa kike.
17 Kisha Yahwe akampiga Farao na nyumba yake kwa mapigo makuu kwa sababau ya Sarai, mke wa Abram.
Lakini Bwana akamwadhibu Farao na nyumba yake kwa maradhi ya kufisha kwa sababu ya kumchukua Sarai, mke wa Abramu.
18 Farao akamwita Abram na kusema, “Nini hiki ambacho umenifanyia? Kwa nini hukuniambia kuwa alikuwa mke wako?
Ndipo Farao akamwita Abramu, akamuuliza, “Umenifanyia nini? Kwa nini hukuniambia ni mke wako?
19 Kwa nini ulisema, 'ni dada yangu; na mimi nikamchukua kuwa mke wangu? Sasa kwa sababu hiyo huyu hapa mke wako. Mchukue na uende zako.”
Kwa nini ulisema, ‘Yeye ni dada yangu,’ hata nikamchukua kuwa mke wangu? Sasa basi, mke wako huyu hapa. Mchukue uende zako!”
20 Kisha Farao akatoa amri kwa watu wake kuhusiana naye, na wakamuondoa, yeye pamoja na mke wake na vyote alivyokuwa navyo.
Kisha Farao akawapa watu wake amri kuhusu Abramu, wakamsindikiza pamoja na mke wake na kila alichokuwa nacho.

< Mwanzo 12 >