< Mwanzo 11 >
1 Sasa nchi yote ilikuwa inatumia lugha moja na ilikua na usemi mmoja.
Wakati huo dunia yote ilikuwa na lugha moja na msemo mmoja.
2 Ikawa waliposafiri upande wa mashariki, wakaona eneo tambarare katika nchi ya Shinari na wakakaa pale.
Watu walipoelekea upande wa mashariki, wakafika kwenye tambarare katika nchi ya Shinari nao wakaishi huko.
3 Wakasemezana, “Haya njoni, tufanye matofari na tuyachome kikamilifu.” Walikuwa na matofari badala ya mawe na lami kama chokaa.
Wakasemezana wao kwa wao, “Njooni, tufyatue matofali na tuyachome vizuri kwa moto.” Walitumia matofali badala ya mawe, na lami kwa ajili ya kushikamanishia hayo matofali.
4 Wakasema, “njoni, na tujenge mji sisi wenyewe na mnara ambao kilele chake kitafika angani, na tujifanyie jina. Kama hatutafanya, basi tutatawanyika katika uso wa nchi yote.”
Ndipo wakasema, “Njooni, tujijengee mji wenye mnara ambao utafika hadi mbinguni, ili tujipatie jina tusije tukatawanyika usoni pa dunia yote.”
5 Kwa hiyo Yahwe akashuka kuona mji na mnara ambao wazao wa Ibrahimu walikuwa wamejenga.
Lakini Bwana akashuka ili auone mji na mnara ambao wanadamu waliokuwa wanaujenga.
6 Yahwe akasema, “Tazama, watu hawa ni taifa moja na lugha moja, na wameanza kufanya hivi! Hivikaribuni halitashindikana jambo watakalo kusudia kulifanya.
Bwana akasema, “Ikiwa kama taifa moja wanaozungumza lugha moja wameanza kufanya hili, basi hakuna lolote watakalopanga kufanya ambalo halitawezekana kwao.
7 Njoni, tushuke na tuvuruge lugha yao pale, ili kwamba wasielewane.”
Njooni, tushuke tuvuruge lugha yao ili wasielewane wao kwa wao.”
8 Kwa hiyo Yahwe akawatawanya kutoka pale kwenda pande zote za uso wa nchi na wakaacha kujenga mji.
Hivyo Bwana akawatawanya kutoka mahali pale kwenda katika dunia yote, nao wakaacha kuujenga huo mji.
9 Kwa hiyo, jina lake ukaitwa Babeli, kwa sababu hapo Yahwe alivuruga lugha ya nchi yote na tangu pale Yahwe akawatawanya ng'ambo juu ya uso wa nchi yote.
Ndiyo maana pakaitwa Babeli, kwa sababu hapo ndipo Bwana alipoivuruga lugha ya dunia nzima. Kutoka hapo Bwana akawatawanya katika uso wa dunia yote.
10 Hivi ndivyo vilikuwa vizazi vya Shemu. Shemu alikuwa na umri wa miaka mia moja, na akamzaa Alfaksadi miaka miwili baada ya gharika.
Hivi ndivyo vizazi vya Shemu. Miaka miwili baada ya gharika, Shemu alipokuwa na miaka 100, akamzaa Arfaksadi.
11 Shemu akaishi miaka miatano baada ya kumzaa Alfaksadi. Pia akazaa wana wengine wa kiume na wa kike.
Baada ya kumzaa Arfaksadi, Shemu aliishi miaka 500, akazaa watoto wengine wa kiume na wa kike.
12 Wakati Alfaksadi alipokuwa ameishi miaka thelathini na mitano akamzaa Shela.
Wakati Arfaksadi alipokuwa na miaka thelathini na mitano, akamzaa Shela.
13 Alfaksadi aliishi miaka 403 baada ya kumzaa Shela. Akawazaa pia wana wengine wa kiume na wa kike.
Baada ya Arfaksadi kumzaa Shela, aliishi miaka 403, akazaa watoto wengine wa kiume na wa kike.
14 Wakati Shela alipokuwa ameishi miaka thelathini, akamzaa Eberi.
Shela alipokuwa na miaka thelathini, akamzaa Eberi.
15 Shela aliishi miaka 403 baada ya kumzaa Eberi. Akawazaa pia wana wengine wa kiume na wa kike.
Shela baada ya kumzaa Eberi, aliishi miaka 403, akazaa watoto wengine wa kiume na wa kike.
16 Wakati Eberi alipokuwa ameishi miaka thelathini na minne, akamzaa Pelegi.
Eberi alipokuwa na miaka thelathini na minne, akamzaa Pelegi.
17 Eberi aliishi miaka 430 baada ya kumzaa Pelegi. Akawazaa pia wana wengine wa kiume na wa kike.
Baada ya Eberi kumzaa Pelegi, aliishi miaka 430, akazaa watoto wengine wa kiume na wa kike.
18 Wakati Pelegi alipokuwa ameishi miaka thelathini, akamzaa Reu.
Pelegi alipokuwa na miaka thelathini, akamzaa Reu.
19 Pelegi aliishi miaka 209 baada ya kumza a Reu. Akawazaa pia wana wengine wa kiume na wa kike.
Baada ya Pelegi kumzaa Reu, aliishi miaka 209, akazaa watoto wengine wa kiume na wa kike.
20 Wakati Reu alipokuwa ameishi miaka thelathini na miwili, alimzaa Serugi.
Reu alipokuwa na miaka thelathini na miwili, akamzaa Serugi.
21 Reu aliishi miaka207 baada ya kumzaa Seregu. Akawazaa pia wana wengine wa kiume na wa kike.
Baada ya Reu kumzaa Serugi, aliishi miaka 207, akazaa watoto wengine wa kiume na wa kike.
22 Wakati Seregu alipokuwa ameishi miaka thelathini, akamzaa Nahori.
Serugi alipokuwa na miaka thelathini, akamzaa Nahori.
23 Seregu aliishi miaka mia mbili baada ya kumzaa Nahori. Akawazaa pia wana wengine wa kiume na wa kike.
Baada ya Serugi kumzaa Nahori, aliishi miaka 200, akazaa watoto wengine wa kiume na wa kike.
24 Wakati Nahori alipokuwa ameishi miaka ishirini na tisa, akamzaa Tera.
Nahori alipokuwa na miaka ishirini na tisa, akamzaa Tera.
25 Nahori aliishi mika 119 baada ya kumzaa Tera. Akawazaa pia wana wengine wa kiume na wa kike.
Baada ya Nahori kumzaa Tera, aliishi miaka 119, akazaa watoto wengine wa kiume na wa kike.
26 Baada ya Tera kuishi miaka sabini, akamzaa Abram, Nahori, na Haran.
Tera alipokuwa na miaka sabini, akamzaa Abramu, Nahori na Harani.
27 Hivi ndivyo vilikuwa vizazi vya Tera. Tera alimzaa Abram, Nahori, na Harani, na Harani akamzaa Lutu.
Hawa ndio wazao wa Tera. Tera aliwazaa Abramu, Nahori na Harani. Harani akamzaa Loti.
28 Harani akafa machoni pa baba yake Tera katika nchi aliyozaliwa, katika Ur wa Wakaldayo.
Tera alipokuwa bado hai, Harani akafa huko Uru ya Wakaldayo, nchi alimozaliwa.
29 Abram na Nahori wakajitwalia wake. Mke wa Abram aliitwa Sarai na mke wa Nahori aliitwa Milka, binti wa Harani, aliyekuwa baba wa Milka na Iska.
Abramu na Nahori walioa. Mke wa Abramu aliitwa Sarai, na mke wa Nahori aliitwa Milka; Milka na Iska walikuwa watoto wa Harani.
30 Sasa Sarai alikuwa Tasa; hakuwa na mtoto.
Sarai alikuwa tasa, hakuwa na watoto.
31 Tera akamtwaa Abram mwanawe, Lutu mwana wa mwanawe Harani, na Sarai mkwewe, mke wa mwanawe Abram, na kwa pamoja wakatoka Ur wa Wakaldayo, kwenda katika nchi ya Kanaani. Lakini walipofika Harani wakakaa pale.
Tera akamchukua Abramu mwanawe, Loti mwana wa Harani mwanawe, na Sarai mkwewe, mke wa Abramu mwanawe, wakatoka kwa pamoja katika Uru ya Wakaldayo kwenda nchi ya Kanaani. Lakini walipofika Harani, wakaishi huko.
32 Tera akaishi miaka 205 kisha akafa hapao Harani.
Tera alikufa huko Harani akiwa na miaka 205.