< Wagalatia 3 >
1 Wagalatia wajinga, ni jicho gani ovu lililowaharibu? Je Yesu Kristo hakuoneshwa kama msulubiwa mbele ya macho yenu?
2 Mimi nataka tu kufahamu hili kutoka kwenu. Je mlimpokea Roho kwa matendo ya sheria au kwa kuamini kile mlichosikia?
3 Je, ninyi ni wajinga kiasi hiki? Je mlianza katika Roho ili mmalize katika mwili?
4 Je mliteseka kwa mambo mengi bure, kama kweli yalikuwa ya bure?
5 Je yeye atoaye Roho kwenu na kutenda matendo ya nguvu kati yenu hufanya kwa matendo ya sheria au kwa kusikia pamoja na imani?
6 Abraham “Alimwamini Mungu akahesabiwa kuwa mwenye haki”.
7 Kwa namna ile ile eleweni kwamba, wale ambao wanaamini ni watoto wa Abrahamu.
8 Andiko lilitabiri kwamba Mungu angewahesabia haki watu wa mataifa kwa njia ya imani. Injili ilihubiriwa kwanza kwa Abrahamu: “katika wewe mataifa yote yatabarikiwa”.
9 Ili baadaye wale ambao wana imani wabarikiwe pamoja na Abrahamu, ambaye alikuwa na imani.
10 Wale ambao wanategemea matendo ya sheria wako chini ya laana. Kwa kuwa imeandikwa, “Amelaaniwa kila mtu ambaye hashikamani na mambo yote yaliyoandikwa katika kitabu cha sheria, kuyatenda yote.”
11 Sasa ni wazi kwamba Mungu hamhesabii haki hata mmoja kwa sheria, kwa kuwa “Mwenye haki ataishi kwa imani”.
12 Sheria haitokani na imani, lakini badala yake “Ambaye hufanya mambo haya katika sheria, ataishi kwa sheria.”
13 Kristo alitukomboa sisi kutoka katika laana ya sheria wakati alipofanyika laana kwa ajili yetu. Kwa kuwa imeandikwa, “Amelaaniwa kila mtu aangikwaye juu ya mti.”
14 Lengo lilikuwa kwamba, baraka ambazo zilikuwa kwa Ibrahimu zingekuja kwa watu wa mataifa katika Kristo Yesu, ili kwamba tuweze kupokea ahadi ya Roho kupitia imani.
15 Ndugu, ninazungumza kwa namna ya kibinadamu. Hata wakati ambapo agano la kibinadamu limekwisha kuwekwa imara, hakuna awezaye kupuuza au kuongezea.
16 Sasa ahadi zilisemwa kwa Ibrahim na kwa kizazi chake. Haisemi, “kwa vizazi,” kumaanisha wengi, bali badala yake kwa mmoja pekee, “kwa kizazi chako,” ambaye ni Kristo.
17 Sasa nasema hivi, sheria ambayo ilikuja miaka 430 baadaye, haiondoi agano la nyuma lililowekwa na Mungu.
18 Kwa kuwa kama urithi ungelikuja kwa njia ya sheria, usingekuwa tena umekuja kwa njia ya ahadi. Lakini Mungu aliutoa bure kwa Ibrahimu kwa njia ya ahadi.
19 Kwa nini sasa sheria ilitolewa? Iliongezwa kwa sababu ya makosa, mpaka mzao wa Ibrahimu aje kwa wale ambao kwao alikuwa ameahidiwa. Sheria iliwekwa katika shinikizo kupitia malaika kwa mkono wa mpatanishi.
20 Sasa mpatanishi humaanisha zaidi ya mtu mmoja, bali Mungu ni mmoja peke yake.
21 Kwa hiyo je sheria iko kinyume na ahadi za Mungu? La hasha! Kwa kuwa kama sheria iliyokuwa imetolewa ilikuwa na uwezo wa kuleta uzima, haki ingepatikana kwa sheria.
22 Lakini badala yake, andiko limefunga mambo yote chini ya dhambi. Mungu alifanya hivi ili kwamba ahadi yake ya kutuokoa sisi kwa imani katika Yesu Kristo iweze kupatikana kwa wale wanao amini.
23 Lakini kabla ya imani katika Kristo haijaja, tulikuwa tumefungwa na kuwa chini ya sheria hadi uje ufunuo wa imani.
24 Kwa hiyo sheria ilifanyika kiongozi wetu hadi Kristo alipokuja, ili kwamba tuhesabiwe haki kwa imani.
25 Sasa kwa kuwa imani imekuja, hatuko tena chini ya mwangalizi.
26 Kwa kuwa ninyi nyote ni watoto wa Mungu kupitia imani katika Kristo Yesu.
27 Wote ambao mlibatizwa katika Kristo mmejivika Kristo.
28 Hakuna Myahudi wala Myunani, mtumwa wala huru, mwanaume wala mwanamke, kwa kuwa ninyi nyote ni mmoja katika Kristo Yesu.
29 Kama ninyi ni wa Kristo, basi ni uzao wa Ibrahimu, warithi kwa mujibu wa ahadi.