< Ezekieli 44 >
1 Kisha yule mtu akanirudisha hata lango la nje la patakatifu linaloelekea mashariki; lilikuwa limefungwa kwa kukazwa.
2 Yahwe akanambia, “Hili lango litakuwa limefungwa; halitafunguliwa. Hakuna mtu atakaye pitia hapo, kwa kuwa Yahwe, Mungu wa Israeli ameingia kwa hilo, hivyo lilikuwa limefungwa kwa kukazwa.
3 Mtawala wa Israeli atakaa katika hilo kula chakula mbele ya Yahwe. Ataingia kwa njia ya varanda na kutoka kwa njia hiyo hiyo.”
4 Kisha akaniletea kwa njia ya lango la kaskazini linaloelekea kwenye nyumba. Hivyo nikaona na kutazama, utukufu wa Yahwe umejaa kwenye nyumba ya Yahwe, nikaanguka kifudifudi.
5 Kisha Yahwe akanambia, “Mwanadamu, andaa moyo wako na tazama kwa macho yako na sikiliza kwa masikio yako kwa yote yale nikuambiayo, kwa amri zote za nyumba ya Yahwe na maagizo yote. Fikiri kuhusu malango ya nyumba na na matokeo ya malango.
6 Kisha waambie wale walioasi, nyumba ya Israeli, 'Bwana Yahwe asema hivi: Acheni matendo yenu maovu kwenu, nyumba ya Israeli-
7 ambayo mmewaleta wageni pamoja na wasiotahiriwa mioyo na wasiotahiriwa mwili kuwa katika patakatifu pangu, kuikufuru nyumba yangu, wakati mlipokuwa mnanitolea chakula, mafuta na damu-mmevunja agano langu kwa matendo yenu maovu.
8 Hamkumaliza kazi zenu zinazohusiana na vitu vitakatifu, lakini mmewateua wengine kuchukua kazi zenu, na mmewatuma kupaangalia mahali patakatifu pangu.
9 Bwana Yahe asema hivi: hakuna mgeni, ambaye hajatahiriwa kwenye moyo wake na mwili, kutoka yeyote wa hao waishio miongoni mwa watu wa Israeli, awezaye kuingia patakatifu pangu.
10 Kisha Walawi wakaenda mbali nami-wakapotea mbali nami, kwenda kwenye sanamu zao-lakini watalipa kwa ajili ya dhambi yao.
11 Wao ni watumishi katika patakatifu pangu, waangalizi wa malango ya nyumba na kutumika kwenye nyumba na kuchinja sadaka za kuteketezwa na dhabihu za watu, na watasimama mbele za watu na kuwatumikia.
12 Lakini kwa sababu wamefanya dhabihu mbele ya sanamu zao, wamekuwa kikwazo kwa dhambi ya nyumba ya Israeli. Kwa hiyo nitainua mkono wangu kuapa kiapo dhidi yao-hivi ndivyo Bwana Yahwe asemavyo-watabeba adhabu yao.
13 Hawatakuja karibu nami kufanya kama makuhani au kukaribiakila vitu vyangu vitakatifu, vitu vitakatifu sana. Badala yake, watabeba lawama zao na hatia zao kwa ajili ya matendo yao ya karaha waliyoyafanya.
14 Lakini nitawaweka kama watunzaji wa kazi katika nyumba, kwa kazi zote na kila kitu kitakachofanyika ndani yake.
15 Kisha makuhani walawi, hao wana wa Zadoki ambao waliokamilisha kazi ya patakatifu pangu wakati wana wa Israeli walipotea mbali nami-watakuja karibu nami kuniambudu. Watasimama mbele yangu kunitolea mafuta na damu-hivi ndivyo Bwana Yahwe asemavyo.
16 Watakuja hata patakatifu pangu; wataikaribia meza yangu kuniabudu na kukamilisha kazi zao kwangu.
17 Hivyo itakuwa kwamba watakapokuja kwenye malango ya ua wa ndani, watatakiwa kuvaa mavazi ya kitani, kwa kuwa hawatakuja na sufu ndani ya lango la ua wa ndani na nyumba yake.
18 Kutakuwa na vilemba juu ya vichwa vyao na kitani ndani ya viuno vyao. Ndani wasivae nguo ambayo itawafanya watoke jasho.
19 Wakati watakapotoka nje ya ua wa nje, hata kwenye ua wa ndani ili kwenda kwa watu, watavua nguo zao walizokuwa wamezivaa kisha wakatumika; watazivua na kuziweka chini katika chumba kitakatifu, hivyo wasiwafanye wengine watakatifu kwa kugusana na nguo zao maalumu.
20 Hawatanyoa vichwa vyao wala kuruhusu nywele zao kuwa ndefu, watapunguza nywele za vichwa vyao.
21 Hakuna kuhani atakaye ruhusiwa kunywa mvinyo wakati atakapoingia kwenye uwa wa ndani,
22 hakuna kuchukua mjane au mwanamke aliyetalikiwa kama mke kwa ajili yake, lakini mwali kutoka safu ya nyumba ya Israeli au mjane aliyekuwa ameolewa na kuhani aliyepita.
23 Kwa kuwa watawafundisha watu wangu tofauti kati ya utakatifu na kukufuru; watawafanya kujua uchafu kutoka usafi.
24 Katika kubishana watasimama kwenye hukumu pamoja na amri yangu; watakuwa waadilifu. Watashika sheria yangu na amri zangu katika sikukuu, na watasherekea siku yangu ya Sabato.
25 Hawataenda kwa mtu aliyekufa ili wasiwe najisi, vinginevyo awe ni baba au mama yao, mwana wa kiume au binti, kaka au dada ambaye hajawahi kulala na mtu; vinginevyo, watakuwa najisi.
26 Baada ya kuhani kuwa najisi, watahesabu mda wa siku saba kwa ajili yake.
27 Katika siku atakayoingia mahali patakatifu, ndani kwenye uzio kutumika katika mahali patakatifu, ataleta sadaka ya dhambi kwa ajili yake mwenyewe-hivi ndivyo Bwana Yahwe asemavyo.
28 Hapa patakuwa urithi wao: Mimi ndiyo urithi wao, na usiwapatie mali katika Israeli; nitakuwa mali yao!
29 Watakula chakula cha sadaka, sadaka za dhambi, sadaka za hatia, na kila kitakachotolewa kwa ajili ya Yahwe katika Israeli, vitakuwa vyao.
30 Malimbuko ya kwanza ya vitu na kila sadaka, kila kitu kitokanacho na sadaka zenu vitakuwa mali ya makuhani, mtatoa sadaka ya chakula kizuri kwa makuhani ili kwamba baraka iweze kukaa katika nyumba zenu.
31 Makuhani hawatakula mzoga au mnyama aliyeraruliwa, iwe ni ndege au mnyama.