< Ezekieli 21 >

1 Kisha neno la Yahwe likanijia, kusema,
Neno la Bwana likanijia kusema:
2 “Mwanadamu, weka uso wako kuelekea Yerusalemu, na neno juu ya patakatifu; tabiri juu ya nchi ya Israeli.
“Mwanadamu, uelekeze uso wako juu ya Yerusalemu na uhubiri dhidi ya mahali patakatifu. Tabiri dhidi ya nchi ya Israeli
3 Sema juu ya nchi ya Israeli, 'Yahwe asema hivi: Tazama! Ni juu yako! Nitautoa upanga wangu kutoka kwenye ala yake na kuwakatilia mbali wote yaani mtu mwenye haki na mtu mwovu kutoka kwako!
uiambie: ‘Hili ndilo Bwana asemalo: Mimi niko kinyume nawe. Nitautoa upanga wangu kwenye ala yake na kumkatilia mbali mwenye haki na mwovu.
4 Ili niwakatilie mbali wote, mwenye haki na mwovu kutoka kwako, upanga wangu utatoka kwenye ala yake juu ya wote wenye mwili kutoka kusini hata kaskazini.
Kwa sababu nitamkatilia mbali mwenye haki na mwovu, upanga wangu utakuwa wazi dhidi ya kila mmoja kuanzia kusini mpaka kaskazini.
5 Kisha wote wenye mwili watajua yakwamba mimi, Yahwe, nimeutoa upanga wangu kutoka kwenye ala yake. Hautarudi tena!'
Ndipo watu wote watajua ya kuwa Mimi Bwana nimeutoa upanga wangu kwenye ala yake, nao hautarudi humo tena.’
6 Kwa hiyo, mwanadamu, gumia kama kuvunjika kwa viuno vyako! Katika uchungu gumia mbele ya macho yao!
“Kwa hiyo lia kwa uchungu, mwanadamu! Lia kwa uchungu mbele yao kwa moyo uliopondeka na kwa huzuni nyingi.
7 Kisha itatokea kwamba watakuuliza, 'Kwa sababu gani unalia?' Kisha utasema, 'Kwa sababu ya habari inayokuja, kwa kuwa kila moyo utakuwa dhaifu, na kila mkono utasita! Kila roho itazimia, na kila goti litatiririrka kama maji. Tazama! Inakuja na itakuwa kama hivi! -hivi ndivyo Bwana Yahwe asemavyo.”'
Nao watakapokuuliza, ‘Kwa nini unalia kwa uchungu?’ Utasema hivi, ‘Kwa sababu ya habari zinazokuja. Kila moyo utayeyuka na kila mkono utalegea, kila roho itazimia na kila goti litalegea kama maji.’ Habari hizo zinakuja! Hakika zitatokea, asema Bwana Mwenyezi.”
8 Kisha neno la Yahwe likanijia, kusema,
Neno la Bwana likanijia, kusema:
9 “Mwanadamu, tabiri na sema, 'Bwana asema hivi: sema: Upanga! Upanga! Utachongwa na kusuguliwa!
“Mwanadamu, tabiri na useme, ‘Hili ndilo Bwana asemalo: “‘Upanga, upanga, ulionolewa na kusuguliwa:
10 Utanolewa ili kushiriki katika machinjio makubwa! Utasuguliwa ili uwe kama mng'ao wa radi! Je! Tufanye furaha katika fimbo ya mwana wa mfalme? Upanga ujao huchukia kila hiyo fimbo!
umenolewa kwa ajili ya mauaji, umesuguliwa ili ungʼae kama umeme wa radi! “‘Je, tuifurahie fimbo ya utawala ya mwanangu Yuda? Upanga unaidharau kila fimbo ya namna hiyo.
11 Hivyo upanga utatolewa kwa ajili ya kusuguliwa, na kisha kushikika kwa mkono! Upanga umechongwa na umesuguliwa na utatolewa kwenye mkono wa yule auaye!'
“‘Upanga umewekwa tayari ili kusuguliwa, ili upate kushikwa mkononi, umenolewa na kusuguliwa, umewekwa tayari kwa mkono wa muuaji.
12 Ita msaada na omboleza, mwanadamu! Kwa kuwa upanga umekuja juu ya watu wangu! Uko juu ya wakuu wote wa Israeli. Wametolewa dhidi ya upanga pamoja na watu wangu. Kwa hiyo, piga paja lako!
Piga kelele na uomboleze, ee mwanadamu, kwa kuwa upanga u dhidi ya watu wangu; u dhidi ya wakuu wote wa Israeli. Wametolewa wauawe kwa upanga pamoja na watu wangu. Kwa hiyo pigapiga kifua chako.
13 Kwa kuwa kuna kujaribiwa, lakini itakuwaje kama fimbo ya kifalme haitakuwepo tena? -hivi ndivyo Bwana Yahwe asemavyo.
“‘Kwa maana upanga huu umejaribiwa na kuhakikishwa, itakuwaje basi fimbo ya ufalme ya Yuda inayoudharau kama haitakuwepo tena, bali itakuwa imeondolewa kabisa? asema Bwana Mwenyezi.’
14 Basi wewe, mwanadamu, tabiri, na piga makofi, kwa kuwa upanga utakushambulia hata mara tatu! Upanga kwa wale watakaochinjwa! Utakuwa upanga kwa ajili ya kuchinjia, ukiwatoboa pande zote!
“Hivyo basi, mwanadamu, tabiri na ukapige makofi. Upanga wako na upige mara mbili, naam, hata mara tatu. Ni upanga wa kuchinja, upanga wa mauaji makuu, ukiwashambulia kutoka kila upande.
15 Ili kuyeyusha mioyo yao na kuongeza kuanguka kwao, nimeweka machinjio ya upanga juu ya malango! Ole! Umeundwa kama mng'ao wa radi, umetengwa kwa ajili ya kuua!
Ili mioyo ipate kuyeyuka na wanaouawa wawe wengi, nimeweka upanga wa kuchinja kwenye malango yao yote. Lo! Umetengenezwa umetemete kama umeme wa radi, umeshikwa kwa ajili ya kuua.
16 Wewe, upanga! Nyooka upande wa kuume! Nyooka upande wa kushoto! Nenda popote ulipoelekeza uso wako.
Ee upanga, kata upande wa kuume, kisha upande wa kushoto, mahali popote makali yako yatakapoelekezwa.
17 Kwa kuwa pia nitapiga mikono yangu miwili kwa pamoja (makofi), na kisha nitaleta ghadhabu yangu kwa waliobakia! Mimi, Yahwe, nimesema hivi!”
Mimi nami nitapiga makofi, nayo ghadhabu yangu itapungua. Mimi Bwana nimesema.”
18 Neno la Yahwe likanijia tena, kusema,
Neno la Bwana likanijia kusema:
19 “Sasa wewe, mwanadamu, teua njia mbili kwa ajili ya upanga wa mfalme wa Babeli upate kuja. Njia hizo mbili zitaanza katika nchi moja, na kibao cha barabarani kitamwonyesha mmoja wao kama kuuelekea mji.
“Mwanadamu, weka alama njia mbili ambazo upanga wa mfalme wa Babeli utapitia, njia hizo zikianzia katika nchi hiyo hiyo. Weka kibao pale ambapo njia zinagawanyika kuelekea mjini.
20 Onyesha njia moja kwa ajili ya jeshi la Wababeli kuja Raba, mji wa Waamoni. Onyesha nyingine kuelekea jeshi la Yuda na mji wa Yerusalemu, ambayo imeimarishwa.
Weka alama njia moja kwa ajili ya upanga upate kuja dhidi ya Raba ya Waamoni na nyingine upate kuja dhidi ya Yuda na Yerusalemu iliyozungushiwa ngome.
21 Kwa kuwa mfalme wa Babeli atasimama kwenye makutano ya barabara, kwenye njia panda, ili kufanya uganga. Alitingisha mishale na kuuliza mwelekeo kutoka kwa sanamu na atalichunguza ini.
Kwa kuwa mfalme wa Babeli sasa amesimama katika njia panda, katika makutano ya njia mbili, akipiga ramli: anapiga kura kwa kutumia mishale, anataka shauri kwa sanamu zake, anachunguza maini ya wanyama.
22 Katika mkono wake wa kuume kutakuwa na dalili kuhusu Yerusalemu, kuweka mitambo ya kubomolea juu ya hiyo, kufungua kinywa chake kupanga kuchinja, kutoa sauti ya vita, kuweka mitambo ya kubomolea juu ya malango, kujenga ngazi, na kusimamisha wima minara ya boma.
Upande wake wa kuume inakuja kura ya Yerusalemu, ambapo ataweka vyombo vya kuvunjia boma, ili kuamrisha mauaji, kupiga ukelele wa vita, kuweka vyombo vya kuvunjia boma kwenye malango, kuweka jeshi kuzunguka na kufanya uzingiraji.
23 Itaonekana kuwa ishara isiyofaa katika macho ya wale walio katika Yerusalemu, wale walioapa kiapo kwa Wababeli! Lakini mfalme atawashtaki kwa kuvunja sheria ya mkataba ili kuwabariki!
Itakuwa kama kupiga ramli kwa uongo kwa wale watu ambao wameapa kumtii yeye. Lakini mfalme wa Babeli atawakumbusha juu ya uovu wao na kuwachukua mateka.
24 Kwa hiyo Bwana Yahwe asema hivi: Kwa sababu umeuleta uovu wako kwenye kumbukumbu zangu, makosa yenu yatafunuliwa! Dhambi zenu zitaonekana katika matendo yenu yote! Kwa sababu hii utamkumbusha kila mtu mtakamatwa kwa mkono wa adui yenu!
“Kwa hiyo hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: ‘Kwa sababu enyi watu mmekumbusha uovu wenu kwa kuasi waziwazi, mkidhihirisha dhambi zenu katika yale yote mfanyayo, kwa kuwa mmefanya jambo hili, mtachukuliwa mateka.
25 Kama wewe, mchafu na mtawala mwovu wa Israeli, ambaye siku ya hukumu imekuja, na ambaye mda wa kufanya uovu umekoma,
“‘Ee mtawala kafiri na mwovu wa Israeli, ambaye siku yako imewadia, ambaye wakati wako wa adhabu umefikia kilele chake,
26 Bwana Yahwe asema hivi kwako: Toa kilemba na vua taji! Mambo hayatakuwa tena kama yalivyokuwa! Kiinue kilicho chini na kiinue kilichoinuka!
hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Vua kilemba, ondoa taji. Kwa kuwa mambo hayatakuwa kama yalivyokuwa. Aliye mnyonge atakwezwa na aliyekwezwa atashushwa.
27 Uharibifu! Uharibifu! Nitaiharibu! Haitakuwa tena hadi atakapokuja yeye ambaye ameteuliwa kutekeleza hukumu.
Mahame! Mahame! Nitaufanya mji kuwa mahame! Hautajengwa upya mpaka aje yule ambaye ndiye mwenye haki nao; yeye ndiye nitakayempa.’
28 Basi wewe, mwanadamu, tabiri na sema, 'Bwana Yahwe asema hivi hawa ni watu wa Amoni kuhusiana na ujio wa aibu yao: Upanga, upanga umechirwa! Umenolewa kwa ajili ya kuchinja, hivyo utakuwa kama kimuli muli cha radi!
“Nawe, mwanadamu, tabiri na useme, ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo kuhusu Waamoni na matukano yao. “‘Upanga, upanga, umefutwa kwa ajili ya kuua, umesuguliwa ili kuangamiza na unametameta kama umeme wa radi!
29 Wakati manabii wameona maono ya uongo juu yako, wakati watakapofanya matambiko kuuijia kwa uongo juu yako, huu upanga utaanguka chini juu ya shingo za mwovu ambao wako karibu kuuawa, ambao siku ya ghadhabu imekuja na ambao mda wa uovu unakaribia kuisha.
Wakati wakitoa maono ya uongo kwa ajili yako, wanapobashiri uongo kwa ajili yako, wanakuweka wewe kwenye shingo za watu wapotovu, wale walio waovu, wale ambao siku yao imewadia, wakati wa adhabu yao ya mwisho.
30 Rudisha upanga kwenye gala yake. Katika mahali ulipoumbwa, katika nchi ya chimbuko lako, nitakuhukumu!
Urudishe upanga kwenye ala yake! Katika mahali ulipoumbiwa, katika nchi ya baba zako, huko nitakuhukumu.
31 Nitamwaga hasira yangu juu yako! Nitapuliza upepo wa moto wa ghadhabu juu yako na kukuweka kwenye mkono wa watu wakatili, watu wajuao kuangamiza!
Nitamwaga ghadhabu yangu juu yako na kupuliza moto wa hasira yangu dhidi yako; nitakutia mikononi mwa watu wakatili, watu stadi katika kuangamiza.
32 Utakuwa kuni kwa ajili ya moto! Damu yako itakuwa kati ya nchi. Hutakumbukwa tena, kwa kuwa mimi, Yahwe nimesema hivi!”'
Mtakuwa kuni za kuwashia moto, damu yenu itamwagwa katika nchi yenu, wala hamtakumbukwa tena; kwa maana Mimi Bwana nimesema.’”

< Ezekieli 21 >