< Kutoka 5 >

1 Baada ya mambo haya kutokea, Musa na Aruni walienda kwa Farao na kumwambia, ““Hivi ndivyo Yahwe, Mungu wa Israeli anasema: 'Waache watu wangu waende, ili wapate kunifanyia karamu jangwani.'”
Baadaye Mose na Aroni wakaenda kwa Farao, wakamwambia, “Hili ndilo asemalo Bwana, Mungu wa Israeli: ‘Waruhusu watu wangu waende, ili waweze kunifanyia sikukuu huko jangwani.’”
2 Farao akasema, “Yahwe ni nani? Kwa nini mimi nisikiliz sauti yake na kuwaacha Israeli waende? Mimi simjui Yahwe; na la zaidi, sitawaacha Israeli waende.”
Farao akasema, “Huyo Bwana ni nani, hata nimtii na kuruhusu Israeli uende? Simjui huyo Bwana wala sitawaruhusu Israeli waende.”
3 Wakasema, “Mungu wa Waebrania amekutana nasi. Tuache twende safari jangwani kwa siku tatu ili tutoe sadaka kwa Yahwe Mungu wetu ili asituadhibu kwa mapigo au kwa upanga.”
Ndipo Mose na Aroni wakasema, “Mungu wa Waebrania amekutana nasi. Sasa turuhusu tuwe na safari ya siku tatu ya jangwani ili tukamtolee Bwana Mungu wetu dhabihu, la sivyo aweza kutupiga sisi kwa tauni au kwa upanga.”
4 Lakini mfalme wa Misri aliwaambia, “Musa na Aruni, kwa nini mnawatoa watu kazini mwao? Nendeni kazini kwenu.”
Lakini mfalme wa Misri akasema, “Mbona ninyi Mose na Aroni mnawachukua watu waache kazi zao? Rudini kwenye kazi zenu!”
5 Pia alisema, “Sasa kuna Waebrania wengi nchini mwetu, na ninyi mnawafanya waache kazi zao.”
Kisha Farao akasema, “Tazama, sasa watu hawa ni wengi, nanyi mnawazuia kufanya kazi.”
6 Siku ile ile, Farao alitoa amri kwa wasimamizi na wanyapara wa wale watu. Akasema,
Siku iyo hiyo Farao akatoa amri hii kwa viongozi wa watumwa na wasimamizi wa watu akawaambia:
7 “Tofauti na ilivyokuwa mwanzo, “Tofauti ni ilivyokuwa awali, msiwapatie tena watu majani ya kutengenezea tofali. Waacheni wao waende kujitafutia majani wenyewe.
“Tangu sasa msiwape hawa watu nyasi za kutengenezea matofali. Wao wakusanye nyasi zao wenyewe.
8 Ingawa wanapaswa kuleta hesabu sawa ya matofali watakayotengeneza kama ilivyokuwa awali. Msipokee pungufu, kwasababu wao ni wavivu. Ndiyo maana wanapiga kelele na kusema, 'turuhusu tuende tukamtolee sadaka Mungu wetu.'
Lakini watakeni kutengeneza matofali kiasi kile kile cha mwanzo, kiwango kisipunguzwe. Wao ni wavivu, ndiyo sababu wanalia, wakisema, ‘Turuhusiwe twende kumtolea Mungu wetu dhabihu.’
9 Waongezeeni kazi wanaume ili wasipate tena muda wa kusikiliza maneno ya upotoshaji.”
Fanyeni kazi kuwa ngumu zaidi kwa watu hao ili kwamba wakazane na kazi na kuacha kusikiliza uongo.”
10 Kwa hiyo viongozi wa watu na waangalizi wao waliwajulisha watu. Walisema, “Hivi ndivyo farao amesema: 'Sitawapeni tena malighafi.
Basi viongozi wa watumwa na wasimamizi wakaenda kuwaambia watu, “Hivi ndivyo Farao asemavyo: ‘Sitawapa tena nyasi.
11 Nyinyi wenyewe mtaenda kutafuta majani popote mtakapopata, lakini kazi zenu hazitapunguzwa.
Nendeni mkatafute nyasi wenyewe popote mnapoweza kuzipata, lakini kazi yenu haitapunguzwa hata kidogo.’”
12 Basi watu hao wakatawanyika katika nchi yote ya Misri ili wapate kukusanya matakataka badala ya majani.
Basi watu wakatawanyika kote nchini Misri kukusanya mabua ya kutumia badala ya nyasi.
13 Wasimamizi wao wakawahimiza na kusema, “Malizeni kazi zenu, sawa na wakati ule majani yalipokuwapo.”
Viongozi wa watumwa wakasisitiza, wakisema, “Timizeni kazi mnayotakiwa kwa kila siku, kama wakati ule mlipokuwa mkipewa nyasi.”
14 Wanyapara wa Farao wakawapiga wasimamizi wa Waisraeli, watu walewale ambao waliwaweka kuwa wasimamizi wa watumishi. Wale Wanyapara wakakazana kuwauliza, “Kwanini hamjatimiza idadi ya matofali inayotakiwa kwenu, siku ya jana na hata leo kama ambavyo mlifanya siku za nyuma?”
Wasimamizi wa Kiisraeli waliochaguliwa na viongozi wa watumwa wa Farao walipigwa na kuulizwa, “Kwa nini hamkutimiza kiwango chenu cha kutengeneza matofali jana na leo, kama mwanzoni?”
15 Basi Wanyapara wa wana wa Israeli wakamwendea Farao na kumlilia. Walisema, “Kwanini unawatendea watumishi wako hivi?
Ndipo wasimamizi wa Kiisraeli wakaenda kumlilia Farao, wakisema: “Mbona umewatendea watumishi wako hivi?
16 Sisi watumishi wako hatupewi majani tena, lakini bado wanatuambia sisi, “Tengenezeni tofali!' Sisi watumwa wako tunapigwa sasa, lakini kosa hilo ni la watu wako.”
Watumishi wako hawapewi nyasi, hata hivyo tumeambiwa, ‘Tengenezeni matofali!’ Watumishi wako wanapigwa, lakini kosa ni la watu wako wenyewe.”
17 Lakini Farao akasema, “Ninyi ni wavivu! Wavivu ninyi! Ninyi mwasema, 'Turuhusu twende kumtolea Yahwe sadaka.'
Farao akasema, “Ninyi ni wavivu ndiyo sababu mnasema, ‘Turuhusu twende tukamtolee Bwana dhabihu.’
18 Sasa rudini kazini. Hamtapewa majani tena, lakini mnapaswa kutengeneza idadi ile ile ya matofali.”
Sasa nendeni kazini. Hamtapewa nyasi zozote, nanyi ni lazima mtengeneze matofali.”
19 Wanyapara wa wana wa Israeli wakagundua ya kuwa walikuwa kwenye shida kubwa mara walipoambiwa, “Hamtapunguza kamwe idadi ya matofali mnayotengeneza kila siku.”
Wasimamizi wa Kiisraeli walitambua kuwa wako taabani walipoambiwa, “Hamtakiwi kupunguza idadi ya matofali mliotakiwa kutengeneza kila siku.”
20 Wakakutana na Musa na Haruni, waliokuwa wamesimama nje ya Ikulu wakati wanatoka kwa Farao.
Walipoondoka kwa Farao, wakawakuta Mose na Aroni wakingojea kukutana nao,
21 Wakawaambia Musa na Haruni, “Yahwe awatazame ninyi na kuwaadhibu, kwa sababu mmetufanya sisi kuonekana wabaya mbele ya Farao na watumishi wake. Mmetia upanga mikononi mwao ili watuue.”
wakawaambia Mose na Aroni, “Bwana na awaangalie awahukumu ninyi! Mmetufanya tunuke kwa Farao na maafisa wake, nanyi mmeweka upanga mikononi mwao ili kutuua sisi.”
22 Musa akarudi kwa BWANA na kumwambia, “Bwana, kwanini umewatenda mabaya watu hawa? Kwanini kunituma mimi kwanza?
Mose akarudi kwa Bwana na kumwambia, “Ee Bwana, mbona umewaletea watu hawa taabu? Kwa nini basi ukanituma mimi?
23 Tangu nilipokuja kwa Farao kusema naye kwa jina lako, amewatenda mabaya watu hawa, wala hujawaokoa watu wako hata kidogo.”
Tangu nilipomwendea Farao kuzungumza naye kwa jina lako, amewaletea taabu watu hawa, nawe kamwe hujawakomboa watu wako.”

< Kutoka 5 >