< Kutoka 37 >
1 Bezaleli akafanya Sanduku la mbao za mshita. Mikono miwili na nusu urefu wake, na mkono mmoja na nusu upana wake, na mkono mmoja na nusu kimo chake.
Bezaleli akatengeneza Sanduku la mbao za mshita: urefu wake ulikuwa dhiraa mbili na nusu, upana wake dhiraa moja na nusu, na kimo chake dhiraa moja na nusu.
2 Kisha akalifunika kwa dhahabu safi ndani na nje na kulifanyia ukingo wa dhahabu kulizunguka pande zote.
Akalifunika kwa dhahabu safi ndani na nje, na kulizungushia ukingo wa dhahabu.
3 Kisha akalitengenezea pete nne za dhahabu, za juu ya miguu yake minne, pete mbili upande wake mmoja na pete mbili upande wake mwingine
Akasubu pete nne za dhahabu na kuzifungia kwenye miguu yake minne, pete mbili kwa upande mmoja na pete mbili kwa upande mwingine.
4 Kisha akafanya miti ya mshita na kuifunika kwa dhahabu.
Kisha akatengeneza mipiko ya mti wa mshita na kuzifunika kwa dhahabu.
5 Halafu akaitia miti hiyo kwenye zile pete zilizo pande za Sanduku ili kulibeba Sanduku.
Akaiingiza hiyo mipiko kwenye zile pete katika pande mbili za Sanduku ili kulibeba.
6 Naye akafanya kifuniko cha dhahabu safi. Mikono miwili na nusu urefu wake, na mkono mmoja na nusu upana wake.
Akatengeneza kifuniko cha upatanisho kwa dhahabu safi: urefu wake ulikuwa dhiraa mbili na nusu, na upana wake dhiraa moja na nusu.
7 Bezaleli akafanya makerubi wawili wa dhahabu. Kwa kazi ya kufua akawafanya kwenye miisho yote miwili ya kifuniko.
Kisha akatengeneza makerubi wawili wa dhahabu iliyofuliwa katika miisho ya hicho kifuniko.
8 Kerubi mmoja kwenye mwisho ule, na yule kerubi mwingine kwenye mwisho huu. Aliwafanya makerubi juu ya kifuniko kwenye miisho yote miwili.
Akatengeneza kerubi mmoja kwenye mwisho mmoja, na kerubi mwingine kwenye mwisho mwingine; akawatengeneza kuwa kitu kimoja na hicho kifuniko katika miisho hiyo miwili.
9 Nao wakawa makerubi wanaonyoosha mabawa yao mawili kuelekea juu, wakisitiri kifuniko kwa mabawa yao, nazo nyuso zao zilikuwa zikielekeana. Nyuso za makerubi hao zilielekea kifuniko hicho.
Makerubi hao walikuwa wametandaza mabawa kuelekea juu, wakitia kivuli hicho kifuniko. Makerubi hao walielekeana, wakitazama hicho kifuniko.
10 Bezaleli akafanya meza ya mbao za mshita. Mikono miwili urefu wake, na mkono mmoja upana wake, na mkono mmoja na nusu kimo chake.
Akatengeneza meza ya mbao za mshita yenye urefu wa dhiraa mbili, upana wa dhiraa moja, na kimo cha dhiraa moja na nusu.
11 Halafu akaifunika kwa dhahabu safi na kufanya ukingo wa dhahabu kuizunguka pande zote.
Kisha akaifunika kwa dhahabu safi, na kuitengenezea ukingo wa dhahabu kuizunguka pande zote.
12 Kisha akafanya mzingo wa upana wa kiganja kuizunguka na kufanya ukingo wa dhahabu kwa ajili ya mzingo wake kuizunguka pande zote.
Pia akatengeneza upapi wenye upana wa nyanda nne, na kuufanyia ule upapi ukingo wa dhahabu kuuzunguka pande zote.
13 Tena, akatengeneza pete nne za dhahabu kwa ajili yake na kuziweka pete hizo kwenye zile pembe nne zilizokuwa kwa ajili ya ile miguu minne.
Akasubu pete nne za dhahabu kwa ajili ya meza hiyo, na kuzifungia kwenye pembe nne, pale penye miguu yake minne.
14 Pete hizo zilikuwa karibu na ule mzingo, ili kutegemeza ile miti ya kuibeba meza hiyo.
Pete hizo ziliwekwa karibu na ukingo ule ili kuishikilia ile mipiko iliyotumika kuibebea hiyo meza.
15 Halafu akafanya ile miti ya mshita na kuifunika kwa dhahabu ili kuibeba ile meza.
Mipiko hiyo ya kubebea meza ilitengenezwa kwa mti wa mshita, na ilikuwa imefunikwa kwa dhahabu.
16 Baada ya hilo akafanya kutokana na dhahabu safi vile vyombo vilivyo juu ya meza, sahani zake na vikombe vyake na mabakuli yake na mitungi yake iliyotumiwa kumimina matoleo ya kinywaji.
Vyombo vyote vya mezani vilitengenezwa kwa dhahabu safi: yaani sahani zake, masinia, na bakuli na bilauri zake kwa ajili ya kumiminia sadaka za vinywaji.
17 Kisha akafanya kinara cha taa cha dhahabu safi. Kwa kazi ya kufua akakifanya kinara cha taa. Pande zake na matawi yake, vikombe vyake, mafundo yake na maua yake vikatokea kwake.
Akatengeneza kinara cha taa cha dhahabu safi iliyofuliwa vizuri katika kitako chake na ufito wake; vikombe vyake vilivyofanana na ua, matovu na maua vilikuwa kitu kimoja.
18 Na matawi sita yalikuwa yakitoka kwenye pande zake, matawi matatu ya kinara cha taa kutoka kwenye upande wake mmoja na matawi mengine matatu ya kinara cha taa kutoka kwenye ule upande wake mwingine.
Matawi sita yalitokeza kuanzia ule ufito wa katikati wa kinara cha taa: matawi matatu upande mmoja na matatu upande mwingine.
19 Vikombe vitatu vyenye umbo la maua ya mlozi vilikuwa kwenye kikundi kimoja cha matawi, vifundo na maua yakifuatana; na vikombe vitatu vyenye umbo la maua ya mlozi vilikuwa kwenye kile kikundi kingine cha matawi, vifundo na maua yakifuatana. Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa yale matawi sita yaliyokuwa yakitoka katika kile kinara cha taa.
Vikombe vitatu vya mfano wa maua ya mlozi yenye matovu na maua vilikuwa katika tawi moja, vikombe vitatu katika tawi jingine, na vivyo hivyo kwa matawi yote sita yaliyotokeza kwenye kile kinara cha taa.
20 Na kwenye kile kinara cha taa kulikuwa na vikombe vinne vyenye umbo la maua ya mlozi, vifundo vyake na maua yake yakifuatana.
Juu ya kinara chenyewe kulikuwepo na vikombe vinne vya mfano wa maua ya mlozi yakiwa na matovu yake na maua yake.
21 Na kile kifundo chini ya matawi mawili kilitoka kwake, na kifundo kilicho chini ya yale matawi mengine mawili kilitoka kwake, na kifundo kingine kilicho chini ya matawi mengine mawili zaidi kilitoka kwake, kwa ajili ya matawi sita yanayotoka katika kinara.
Tovu moja lilikuwa chini ya jozi ya kwanza ya matawi yaliyotokeza kwenye kinara cha taa, tovu la pili chini ya jozi ya pili, nalo tovu la tatu chini ya jozi ya tatu, yaani, matawi sita kwa jumla.
22 Vifundo vyake na matawi yake vilitoka kwake, vyote vilikuwa kitu kimoja cha kazi ya kufua, cha dhahabu safi.
Matovu na matawi yote yalikuwa kitu kimoja na kile kinara cha taa, yakiwa yamefuliwa kwa dhahabu safi.
23 Kisha akafanya taa zake saba na mikasi ya tambi zake na vyetezo vyake kutokana na dhahabu safi.
Akatengeneza taa zake saba, na pia mikasi ya kusawazishia tambi, pamoja na masinia, zote kwa dhahabu safi.
24 Alikifanya kwa talanta ya dhahabu safi, hicho pamoja na vyombo vyake vyote.
Akatengeneza kinara hicho cha taa pamoja na vifaa vyake vyote kutumia talanta moja ya dhahabu safi.
25 Sasa akafanya madhabahu ya uvumba kutokana na mbao za mshita. Mkono mmoja urefu wake na mkono mmoja upana wake, ikiwa mraba, na mikono miwili kimo chake. Pembe zake zilitoka kwake.
Akatengeneza madhabahu ya kufukizia uvumba kwa mbao za mshita. Ilikuwa ya mraba, urefu na upana wake dhiraa moja, na kimo cha dhiraa mbili, nazo pembe zake zilikuwa kitu kimoja nayo.
26 Kisha akaifunika kwa dhahabu safi, upande wake wa juu na pande zake za kando kuizunguka na pembe zake, naye akafanya ukingo wa dhahabu kuizunguka pande zote.
Akafunika hayo madhabahu juu na pande zote na pia zile pembe zake kwa dhahabu safi, na akayafanyizia ukingo wa dhahabu kuizunguka.
27 Naye akaifanyia pete mbili za dhahabu chini ya ukingo wake kwenye pande zake mbili, kwenye pande zake mbili zinazoelekeana, za kutegemeza ile miti ya kuibeba.
Akatengeneza pete mbili za dhahabu kwa ajili ya madhabahu chini ya huo ukingo, zikiwa mbili kila upande, za kushikilia hiyo mipiko iliyotumika kuyabebea madhabahu.
28 Kisha akafanya ile miti ya mshita na kuifunika kwa dhahabu.
Akatengeneza mipiko kwa miti ya mshita na kuifunika kwa dhahabu.
29 Tena akafanya yale mafuta yanayotumiwa kutia mafuta na ule uvumba safi uliotiwa manukato, kazi ya mtengenezaji wa marhamu.
Pia akatengeneza mafuta matakatifu ya upako, na uvumba safi wenye harufu nzuri, kazi ya mtengeneza manukato.