< Kutoka 37 >
1 Bezaleli akafanya Sanduku la mbao za mshita. Mikono miwili na nusu urefu wake, na mkono mmoja na nusu upana wake, na mkono mmoja na nusu kimo chake.
2 Kisha akalifunika kwa dhahabu safi ndani na nje na kulifanyia ukingo wa dhahabu kulizunguka pande zote.
3 Kisha akalitengenezea pete nne za dhahabu, za juu ya miguu yake minne, pete mbili upande wake mmoja na pete mbili upande wake mwingine
4 Kisha akafanya miti ya mshita na kuifunika kwa dhahabu.
5 Halafu akaitia miti hiyo kwenye zile pete zilizo pande za Sanduku ili kulibeba Sanduku.
6 Naye akafanya kifuniko cha dhahabu safi. Mikono miwili na nusu urefu wake, na mkono mmoja na nusu upana wake.
7 Bezaleli akafanya makerubi wawili wa dhahabu. Kwa kazi ya kufua akawafanya kwenye miisho yote miwili ya kifuniko.
8 Kerubi mmoja kwenye mwisho ule, na yule kerubi mwingine kwenye mwisho huu. Aliwafanya makerubi juu ya kifuniko kwenye miisho yote miwili.
9 Nao wakawa makerubi wanaonyoosha mabawa yao mawili kuelekea juu, wakisitiri kifuniko kwa mabawa yao, nazo nyuso zao zilikuwa zikielekeana. Nyuso za makerubi hao zilielekea kifuniko hicho.
10 Bezaleli akafanya meza ya mbao za mshita. Mikono miwili urefu wake, na mkono mmoja upana wake, na mkono mmoja na nusu kimo chake.
11 Halafu akaifunika kwa dhahabu safi na kufanya ukingo wa dhahabu kuizunguka pande zote.
12 Kisha akafanya mzingo wa upana wa kiganja kuizunguka na kufanya ukingo wa dhahabu kwa ajili ya mzingo wake kuizunguka pande zote.
13 Tena, akatengeneza pete nne za dhahabu kwa ajili yake na kuziweka pete hizo kwenye zile pembe nne zilizokuwa kwa ajili ya ile miguu minne.
14 Pete hizo zilikuwa karibu na ule mzingo, ili kutegemeza ile miti ya kuibeba meza hiyo.
15 Halafu akafanya ile miti ya mshita na kuifunika kwa dhahabu ili kuibeba ile meza.
16 Baada ya hilo akafanya kutokana na dhahabu safi vile vyombo vilivyo juu ya meza, sahani zake na vikombe vyake na mabakuli yake na mitungi yake iliyotumiwa kumimina matoleo ya kinywaji.
17 Kisha akafanya kinara cha taa cha dhahabu safi. Kwa kazi ya kufua akakifanya kinara cha taa. Pande zake na matawi yake, vikombe vyake, mafundo yake na maua yake vikatokea kwake.
18 Na matawi sita yalikuwa yakitoka kwenye pande zake, matawi matatu ya kinara cha taa kutoka kwenye upande wake mmoja na matawi mengine matatu ya kinara cha taa kutoka kwenye ule upande wake mwingine.
19 Vikombe vitatu vyenye umbo la maua ya mlozi vilikuwa kwenye kikundi kimoja cha matawi, vifundo na maua yakifuatana; na vikombe vitatu vyenye umbo la maua ya mlozi vilikuwa kwenye kile kikundi kingine cha matawi, vifundo na maua yakifuatana. Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa yale matawi sita yaliyokuwa yakitoka katika kile kinara cha taa.
20 Na kwenye kile kinara cha taa kulikuwa na vikombe vinne vyenye umbo la maua ya mlozi, vifundo vyake na maua yake yakifuatana.
21 Na kile kifundo chini ya matawi mawili kilitoka kwake, na kifundo kilicho chini ya yale matawi mengine mawili kilitoka kwake, na kifundo kingine kilicho chini ya matawi mengine mawili zaidi kilitoka kwake, kwa ajili ya matawi sita yanayotoka katika kinara.
22 Vifundo vyake na matawi yake vilitoka kwake, vyote vilikuwa kitu kimoja cha kazi ya kufua, cha dhahabu safi.
23 Kisha akafanya taa zake saba na mikasi ya tambi zake na vyetezo vyake kutokana na dhahabu safi.
24 Alikifanya kwa talanta ya dhahabu safi, hicho pamoja na vyombo vyake vyote.
25 Sasa akafanya madhabahu ya uvumba kutokana na mbao za mshita. Mkono mmoja urefu wake na mkono mmoja upana wake, ikiwa mraba, na mikono miwili kimo chake. Pembe zake zilitoka kwake.
26 Kisha akaifunika kwa dhahabu safi, upande wake wa juu na pande zake za kando kuizunguka na pembe zake, naye akafanya ukingo wa dhahabu kuizunguka pande zote.
27 Naye akaifanyia pete mbili za dhahabu chini ya ukingo wake kwenye pande zake mbili, kwenye pande zake mbili zinazoelekeana, za kutegemeza ile miti ya kuibeba.
28 Kisha akafanya ile miti ya mshita na kuifunika kwa dhahabu.
29 Tena akafanya yale mafuta yanayotumiwa kutia mafuta na ule uvumba safi uliotiwa manukato, kazi ya mtengenezaji wa marhamu.