< Kutoka 28 >
1 Umuite Aruni kaka yako na wana wake - Nadabu, na Abihu, na Eleazari, na Ithamari - miongoni mwa wana wa Israeli, ili anitumikie katika kazi ya ukuhani.
“Mtwae Aroni ndugu yako aliyeletwa kwako kutoka miongoni mwa Waisraeli, pamoja na wanawe Nadabu, Abihu, Eleazari na Ithamari, ili wanitumikie katika kazi ya ukuhani.
2 Nawe utamfanyia Aruni ndugu yako mavazi matakatifu, kwa utukufu na kwa uzuri.
Mshonee Aroni ndugu yako mavazi matakatifu ili yampe ukuu na heshima.
3 Nawe utawaambia watu wote wenye moyo wa hekima, niliowajaza na roho ya hekima wamfanyie Aruni mavazi ili kumtakasa anitumikie katika kazi ya ukuhani.
Waambie mafundi stadi wote niliowapa hekima katika shughuli hiyo wamtengenezee Aroni mavazi hayo, ili awekwe wakfu, anitumikie katika kazi ya ukuhani.
4 Na mavazi watakayoyafanya ni kifuko cha kifuani, na naivera, na joho, na kanzu ya kazi ya urembo, na kilemba, na mshipi; nao watawafanyia Aruni nduguye, na wanawe, mavazi matakatifu ili anitumikie katika kazi ya ukuhani.
Haya ndiyo mavazi watakayoshona: kifuko cha kifuani, kisibau, kanzu, joho lililorembwa, kilemba na mshipi. Mavazi haya yatashonwa kwa ajili ya ndugu yako Aroni na wanawe ili wanitumikie katika kazi ya ukuhani.
5 Nao wataitwaa dhahabu, na nguo ya rangi ya samawi, na ya rangi ya zambarau, na ya rangi nyekundu.
Waambie watumie dhahabu na nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu pamoja na kitani safi.
6 Nao waifanye naivera kwa nyuzi za dhahabu, na za samawi, na za zambarau, na nyekundu, na kitani nzuri yenye kusokotwa kwa kazi ya mstadi.
“Tengeneza kisibau cha dhahabu, na nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, za rangi nyekundu na kitani safi iliyosokotwa, kazi ya fundi stadi.
7 Lazima itakuwa na vipande viwili vya mabegani, vilivyoungana kwenye ncha zake mbili; ili ipate kuunganywa.
Kitakuwa na vipande viwili vya mabegani vilivyoshikizwa kwenye pembe zake mbili ili kufungia kisibau.
8 Na mshipi wa kazi ya ustadi ulio juu yake, ili kuifunga mahali pake; utakuwa wa kazi kama ile ya naivera, ya vitu vile vile ya nyuzi za dhahabu, na za rangi ya samawi, na ya zambarau, na nyekundu, na kitani nzuri yenye kusokotwa.
Mshipi wa kiunoni uliofumwa kwa ustadi utafanana nacho: utakuwa kitu kimoja na hicho kisibau, nao utengenezwe kwa dhahabu na nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na nyekundu na kwa kitani iliyosokotwa vizuri.
9 Nawe utatwaa vito viwili vya shohamu, ya rangi ya chani-kiwiti, nawe utachora juu yake majina ya wana wa Israeli;
“Chukua vito viwili vya shohamu, na uchore juu yake majina ya wana wa Israeli
10 Majina yao sita katika kito kimoja, na majina sita yaliyosalia katika kile kito cha pili, kwa utaratibu wa kuzaliwa kwao.
kufuatana na walivyozaliwa: majina sita katika kito kimoja, na mengine sita katika kito kingine.
11 Kwa kazi mtu mwenye kuchora mawe kama vile muhuri ichorwavyo, utavichora hivi vito viwili, sawasawa na majina ya wana wa Israeli, nawe utavitia katika vijalizo vya dhahabu.
Yachore majina ya wana wa Israeli juu ya vito hivyo viwili kama vile sonara anavyochonga muhuri. Kisha uvitie vito hivyo katika vijalizo vya dhahabu,
12 Nawe utavitia vile vito viwili juu ya vipande vya mabegani vya hiyo naivera, viwe vito vya ukumbusho kwa ajili ya wana wa Israeli. Naye Aruni atayachukua majina yao mbele za Yahweh juu ya mabega yake mawili ili kuwa ukumbusho.
na uvifungie juu ya vipande vya mabega ya kisibau yawe kama vito vya ukumbusho kwa wana wa Israeli. Aroni atavaa majina hayo mabegani mwake kama kumbukumbu mbele za Bwana.
13 Nawe fanya vijalizo viwili vya dhahabu
Tengeneza vijalizo vya dhahabu
14 na mikufu miwili ya dhahabu safi; utaifanya iwe mfano wa kamba, ya kazi ya kusokotwa; nawe uitie ile mikufu ya kazi ya kusokotwa katika vile vijalizo.
na mikufu miwili ya dhahabu safi iliyosokotwa kama kamba, na uifunge mikufu hiyo kwenye vijalizo.
15 Nawe lazima utafanya kifuko cha kifuani cha hukumu, kazi ya fundi stadi; utakifanya kwa kuiandama ile kazi ya hiyo naivera. Fanya nyuzi za dhahabu, na za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na nyekundu, na kitani safi yenye kusokotwa, ndivyo utakavyokifanya.
“Fanyiza kifuko cha kifuani kwa ajili ya kufanya maamuzi, kazi ya fundi stadi. Kitengeneze kama kile kisibau: cha dhahabu, na nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu, cha kitani safi iliyosokotwa.
16 Kitakuwa mraba, tena cha kukunjwa; urefu wake utakuwa shibiri moja, na upana wake shibiri moja.
Kitakuwa cha mraba, chenye urefu wa shibiri moja na upana wa shibiri moja, na kikunjwe mara mbili.
17 Nawe ukijaze viweko vya vito, safu nne za vito; safu moja itakuwa ni akiki, na yakuti ya rangi ya manjano, na baharamani, hivi vitakuwa safu ya kwanza.
Kisha weka safu nne za vito vya thamani juu yake. Safu ya kwanza itakuwa na akiki, yakuti manjano na zabarajadi;
18 Na safu ya pili itakuwa zumaridi, na yakuti samawi, na almasi.
katika safu ya pili itakuwa na almasi, yakuti samawi na zumaridi;
19 Na safu ya tatu itakuwa hiakintho, na akiki nyekundu, na amethisto.
safu ya tatu itakuwa na hiakintho, akiki nyekundu na amethisto;
20 Na safu ya nne itakuwa ni zabarajadi, na shohamu, na yaspi. Vito hivyo vitakazwa ndani ya dhahabu kwa kujaa mahali pake.
na safu ya nne itakuwa na krisolitho, shohamu na yaspi. Yote yatiwe kwenye vijalizo vya dhahabu.
21 Na vile vito vitakuwa sawasawa na majina ya wana wa Israeli, kumi na viwili, sawasawa na majina yao. Mfano wa kuchora kwa muhuri kila kimoja sawasawa na jina lake, vitakuwa vya hizo kabila kumi na mbili.
Patakuwa na vito kumi na viwili, kila kimoja kwa jina mojawapo la wana wa Israeli, kila kimoja kichorwe kama muhuri kikiwa na jina mojawapo la yale makabila kumi na mawili.
22 Nawe lazima utie katika kile kifuko cha kifuani mikufu mfano wa kamba, ya kazi ya kusokotwa, ya dhahabu safi.
“Kwa ajili ya kile kifuko cha kifuani, tengeneza mikufu ya dhahabu safi, iliyosokotwa kama kamba.
23 Nawe utie maduara mawili ya dhahabu katika kile kifuko cha kifuani, na kuzitia hizo pete mbili katika ncha mbili za kifuko cha kifuani.
Tengeneza pete mbili za dhahabu kwa ajili yake, uzifungie kwenye pembe mbili za hicho kifuko cha kifuani.
24 Nawe utie hiyo mikufu miwili ya dhahabu iliyosokotwa katika zile pete mbili zilizo katika ncha za kifuko cha kifuani.
Funga ile mikufu miwili ya dhahabu kwenye hizo pete zilizo katika pembe za hicho kifuko cha kifuani,
25 Na ncha zile nyingine za hiyo mikufu miwili ya kusokotwa utazitia katika vile vijalizo viwili, na kuvitia katika vile vipande vya mabegani vya naivera upande wa mbele.
nazo zile ncha nyingine za mkufu zifunge kwenye vile vijalizo viwili, na uzishikamanishe na vile vipande vya mabega vya kile kisibau upande wa mbele.
26 Nawe utafanya viduara vili vya dhahabu, uzitie katika hizo ncha mbili za kifuko cha kifuani, katika ukingo wake.
Tengeneza pete mbili za dhahabu, uzishikamanishe kwenye pembe mbili za chini, upande wa ndani wa kifuko cha kifuani karibu na kisibau.
27 Nawe lazima ufanye viduara vili vya dhahabu, na kuzitia katika vile vipande viwili vya mabegani vya ile naivera chini yake, upande wa mbele, karibu na kifungo chake, juu ya huo mshipi wa naivera uliosukwa kwa ustadi.
Tengeneza pete nyingine mbili za dhahabu, na uzishikamanishe sehemu ya chini ya vipande vya mabega upande wa mbele wa kile kisibau, karibu na pindo juu kidogo ya mshipi wa kiunoni wa kisibau.
28 Nao watakikaza kile kileso kwa vile viduara vyake kwenye viduara za naivera kwa ukanda wa rangi ya samawi, ili kwamba kikae pale juu ya ule mshipi wa naivera uliosukwa kwa ustadi, ili kwamba kifuko cha kifuani kisiachane na naivera.
Pete za kifuko cha kifuani zitafungwa kwenye pete zile za kisibau kwa kamba ya buluu, ziunganishwe na ule mshipi wa kiunoni, ili kifuko cha kifuani kisisogee kutoka kwenye kile kisibau.
29 Na Aruni atayachukua majina ya wana wa Israeli katika kile kifuko cha kifuani cha hukumu juu ya moyo wake kwa kufanya maamuzi, hapo atakapoingia ndani ya mahali patakatifu, kuwa ukumbusho mbele yaYahweh daima.
“Wakati wowote Aroni aingiapo Mahali Patakatifu, atakuwa na yale majina ya wana wa Israeli moyoni mwake juu ya kile kifuko cha kifuani cha uamuzi kama kumbukumbu ya kudumu mbele za Bwana.
30 Nawe utie hizo Urimu na Thumimu katika kile kifuko cha kifuani cha hukumu; nazo zitakuwa juu ya moyo wa Aruni, hapo atakapoingia ndani mbele ya Yahweh na Aruni atachukua hukumu ya hao wana wa Israeli juu ya moyo wake mbele ya Yahweh daima.
Pia weka Urimu na Thumimu ndani ya kifuko cha kifuani, yawe juu ya moyo wa Aroni kila mara aingiapo mbele za Bwana. Kwa hiyo siku zote Aroni atakuwa na uwezo kufanya maamuzi kwa ajili ya wana wa Israeli mbele za Bwana.
31 Nawe fanya hiyo joho ya naivera ya rangi ya samawi yote.
“Shona joho la kisibau lote kwa kitambaa cha rangi ya buluu tupu,
32 Nayo itakuwa na tundu katikati yake kwa kupitisha kichwa; itakuwa na utepe wa kazi ya kusokotwa kuzunguka hilo tundu lake, mfano wa tundu lililo katika kanzu ya chuma, ili lisipasuke.
na katikati uweke nafasi ya kuingizia kichwa. Kutakuwa na utepe uliofumwa, unaofanana na ukosi kuizunguka nafasi hiyo, ili isichanike.
33 Nawe katika pindo zake utatia makomamanga ya rangi ya samawi, na ya rangi ya zambarau, na ya rangi nyekundu, kuzunguka pindo zake kotekote; na njuga za dhahabu kati ya hayo makomamanga pande zote.
Tengeneza makomamanga ya nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu kuzunguka pindo la hilo joho, na uweke pia vikengele vya dhahabu kati ya hayo makomamanga.
34 Kengele ya dhahabu na komamanga, kengele ya dhahabu na komamanga, katika pindo za joho kuizunguka pande zote.
Hivyo vikengele vya dhahabu na makomamanga vitapishana kuzunguka upindo wa joho lile.
35 Nayo itakuwa juu ya Aruni akitumika; na sauti ya hizo kengele itasikilikana hapo aingiapo ndani ya mahali patakatifu mbele ya Yahweh na hapo atokapo nje, ili kwamba asife.
Ni lazima Aroni alivae anapofanya huduma. Sauti ya hivyo vikengele itasikika anapoingia na kutoka Mahali Patakatifu mbele za Bwana, ili asije akafa.
36 Nawe fanya bamba la dhahabu safi na kuchora juu yake, mfano wa machoro ya muhuri, “Mtakatifu kwa Yahweh.”
“Tengeneza bamba la dhahabu safi na uchore juu yake maneno haya kama vile muhuri huchorwa: Mtakatifu kwa Bwana.
37 Nawe ulitie hilo bamba katika ukanda wa rangi ya samawi, nalo litakuwa katika kile kilemba; litakuwa upande wa mbele wa kile kilemba.
Lifunge hilo bamba kwa kamba ya buluu kwenye kilemba, nalo ni lazima liwe mbele ya kilemba.
38 Nalo litakuwa katika kipaji cha uso cha Aruni, na Aruni atauchukua uovu wa vile vitu vitakatifu, watakavyovitakasa hao wana wa Israeli katika vipawa vyao vyote vitakatifu, nalo litakuwa katika kipaji chake cha uso sikuzote, ili kwamba vipate kukubaliwa mbele za Yahweh.
Aroni alivae bamba hilo kwenye paji la uso wake, naye atachukua hatia kuhusu sadaka takatifu za Waisraeli wanazoweka wakfu, sadaka za aina yoyote. Litakuwa kwenye paji la uso wa Aroni daima ili zikubalike kwa Bwana.
39 Na hiyo kanzu utaifuma ya kitani nzuri ya kazi ya urembo, ufanye na kilemba cha nguo ya kitani nzuri, nawe utafanya mshipi wa kazi ya mwenye kutia taraza.
“Fuma koti la kitani safi na ufanye kilemba cha kitani safi. Mshipi uwe ni kazi ya mtarizi.
40 Kisha utafany kanzu kwa ajili ya wana wa Aruni, nawe wafanyie mishipi, wafanyie na kofia kwa utukufu na uzuri.
Watengenezee wana wa Aroni makoti, mishipi na kofia, ili kuwapa ukuu na heshima.
41 Nawe mvike huyo nduguye Aruni na wanawe nao mavazi hayo; nawe watie mafuta, na kuwaweka kwa kazi takatifu, na kuwatakasa, ili wapate kunitumikia mimi katika kazi ya ukuhani.
Baada ya kumvika Aroni ndugu yako pamoja na wanawe nguo hizi, watie mafuta na kuwabariki. Waweke wakfu ili wanitumikie katika kazi ya ukuhani.
42 Nawe wafanyie suruali za nguo ya kitani, ili kufunika tupu ya miili yao; suruali hizo zitafika tangu kiunoni hata mapajani.
“Watengenezee nguo za ndani za kitani zitakazofunika mwili, kutoka kiunoni hadi mapajani.
43 Aruni na wanawe watazivaa, hapo watakapoingia katika hema ya kukutania, au hapo watakapoikaribia madhabahu ili watumike katika mahali patakatifu; wasije wakachukua uovu, wakafa; hii itakuwa ni amri ya milele kwake yeye, na kwa wazao wake.
Aroni na wanawe ni lazima wavae haya kila wanapoingia katika Hema la Kukutania au wanaposogelea madhabahu wakati wa kutoa huduma katika Mahali Patakatifu, ili wasije wakafanya kosa wakafa. “Haya yawe maagizo ya kudumu kwa Aroni na vizazi vyake.