< Kutoka 2 >

1 Sasa mwanamme wa kabila la Lawi alimuoa mwanamke Mlawi.
Basi mtu mmoja wa nyumba ya Lawi akaoa mwanamke Mlawi,
2 Yule mwanamke akapata mimba na kuzaa mtoto wa kiume. Alipoona ya kuwa alikuwa mtoto mwenye afaya, alimficha kwa miezi mitatu.
naye mwanamke huyo akapata mimba, akazaa mtoto wa kiume. Alipoona mtoto huyo ni mzuri, akamficha kwa miezi mitatu.
3 Lakini alipokuwa hawezi kuendelea kumficha tena, alichukua kikapu cha manyasi akakipaka sifa na lami. Akamtia mtoto ndani yake na kukiweka juu ya maji katika majani kando ya mto.
Lakini alipoona hawezi kumficha zaidi, akamtengenezea kisafina cha mafunjo, akakipaka lami. Kisha akamweka huyo mtoto ndani yake, akakificha katikati ya matete kando ya ukingo wa Mto Naili.
4 Dada yake akasimama kwa mbali ili ajue yatakayompata.
Dada ya huyo mtoto akasimama mbali ili kuona kitakachompata mtoto.
5 Binti Farao akashuka kuoga mtoni wakati vijakazi wake wakitembea kando ya mto. Naye akaona kile kikapu katika majani na akamtuma kijakazi wake kwenda kukileta.
Ndipo binti Farao akateremka mtoni Naili kuoga, nao wahudumu wake wakawa wanatembea ukingoni mwa mto. Binti mfalme akaona kisafina katikati ya manyasi, akamtuma mmoja wa watumwa wake wa kike kukichukua.
6 Alipokifungua, aliomwona mtoto. Tazama, mtoto alikuwa analia. Alimhurumia na kusema, “Bila shaka huyu ni mmoja wapo wa watoto wa Waebrania.”
Alifungua kisafina akaona mtoto ndani yake. Mtoto alikuwa akilia, akamhurumia. Akasema, “Huyu ni mmoja wa watoto wa Kiebrania.”
7 Basi dada wa yule mtoto akamwambia binti Farao, “Je naweza kwenda kukutafutia mwanamke wa Kiebrania aje akulele mtoto kwa ajili yako?”
Ndipo dada wa huyo mtoto akamuuliza binti Farao, “Je, niende nikakutafutie mmoja wa wanawake wa Kiebrania akulelee huyu mtoto?”
8 Binti Farao akamwambia, “Nenda.” Hivyo yule binti akaenda na kumwita mama yake yule mtoto.
Binti Farao akamjibu, “Ndiyo, nenda.” Yule msichana akaenda akamleta mama wa mtoto.
9 Binti Farao akamwambia mama yake yule mtoto, “Mchukue mtoto huyu ukaninyonyeshee, nami nitakupa posho.” Hivyo yule mwanamke akamchukua mtoto na kumnyonyesha.
Binti Farao akamwambia, “Mchukue huyu mtoto unisaidie kumlea, nami nitakulipa.” Basi yule mwanamke akamchukua mtoto na kumlea.
10 Mtoto alipokuwa mkubwa, akamleta kwa binti Farao, na akawa mtoto wake. Akamwita jina lake Musa akisema, “Kwa sababu nilimtoa katika maji.”
Mtoto alipokua, akampeleka kwa binti Farao, naye akawa mwanawe. Akamwita jina lake Mose akisema, “Nilimtoa kwenye maji.”
11 Musa alipokuwa mtu mzima, alienda kwa watu wake na kuona kazi ngumu walizokuwa wanafanya. Alimuona Mmisri akimpiga Mwebrania, mmoja wa watu wa jamii yake.
Siku moja, baada ya Mose kukua, akaondoka kwenda walikokuwa watu wake, na akachunguza jinsi walivyokuwa wakifanya kazi ngumu. Akamwona Mmisri akimpiga Mwebrania, mmojawapo wa watu wake.
12 Aliangalia huku na kule, na alipoona ya kuwa hakuna mtu, alimuua yule mmisri na kuuficha mwili wake katika mchanga.
Mose akatazama huku na huko asione mtu yeyote, akamuua yule Mmisri, akamficha mchangani.
13 Alienda tena siku iliyofuata, na tazama, Waebrania wawili walikuwa wanapigana. Alimwambia yule aliyekuwa na makosa, “Kwa nini unampigia mwenzako?”
Kesho yake akatoka, akaona Waebrania wawili wakipigana. Akamuuliza yule aliyekosa, “Mbona unampiga Mwebrania mwenzako?”
14 Lakini yule mtu alisema, “Ni nani aliyekuweka wewe kuwa kiongozi na mwamuzi juu yetu? Unataka kuniua na mimi kama ulivyomuua yule mmisri?” Ndipo Musa akaogopa na kusema, “Hakika niliyoyafanya yamejulikana.”
Yule mtu akamjibu, “Ni nani aliyekufanya mtawala na mwamuzi juu yetu? Je, unataka kuniua kama ulivyomuua yule Mmisri?” Ndipo Mose akaogopa na kuwaza, “Jambo lile nililofanya lazima limefahamika.”
15 Farao aliposikia habari hizi, alijaribu kumuua Musa. Lakini Musa alikimbia na kwenda kuishi katika nchi ya Wamidiani. Kule alikaa chini kando ya mto.
Farao aliposikia jambo hili, alijaribu kumuua Mose, lakini Mose akamkimbia Farao na kwenda kuishi katika nchi ya Midiani, akaketi kando ya kisima.
16 Wakati huo kuhani wa Midiani alikuwa na mabinti saba. Walikuja mtoni kuchota maji na kujaza vyombo vyao ili wawanyweshe mifuko ya baba yao.
Kuhani wa Midiani alikuwa na binti saba, nao wakaja kisimani ili kuchota maji na kujaza hori kwa ajili ya kunyweshea mifugo ya baba yao.
17 Wachungaji walikuja na kutaka kuwafukuza, lakini Musa alienda kuwasaidia. Kisha akawanywesha mifugo wao.
Baadhi ya wachungaji wakaja wakawafukuza hao wasichana. Ndipo Mose akainuka, akawasaidia na kunywesha mifugo yao.
18 Wale mabinti walipoenda kwa Reueli baba yao, aliwauliza, “Kwa nini mmerudi nyumbani mapema hivi leo?”
Hao wasichana waliporudi nyumbani kwa Reueli baba yao, akawauliza, “Imekuwaje leo mmerudi mapema hivyo?”
19 Wakamwambia, “Mmisri mmoja alituokoa dhidi ya wachungaji. Pia alichota maji na kuwanywesha mifugo wetu.”
Wakamjibu, “Mmisri mmoja alituokoa kutoka mikononi mwa wachungaji. Pia mtu huyo alituchotea maji na kunywesha mifugo.”
20 Kisha akawauliza binti zake, “Yu wapi sasa? Kwa nini mlimwacha? Mwiteni ili apate kula chakula pamoja nasi.”
Akawauliza binti zake, “Yuko wapi? Mbona mmemwacha? Mkaribisheni ale chakula.”
21 Musa akakubali kukaa na yule mtu ambaye pia alimpa binti yake Zipora ili amuoe.
Mose akakubali kukaa kwa huyo mtu, ambaye alimpa Mose binti yake aliyeitwa Sipora amwoe.
22 Alizaa mtoto wa kiume, na Musa akamwita jina lake Geshomu; akisema; “Nimekuwa mkazi katika nchi ya ugeni.”
Sipora alizaa mtoto wa kiume, naye Mose akamwita Gershomu, akisema, “Nimekuwa mgeni katika nchi ya kigeni.”
23 Muda mrefu baadaye, mfalme wa Misri akafa. Waisraeli walilalamika kwa sababu ya kazi za utumwa. Walilia kutafuta msaada, na maombi yao yakamfikia Mungu kwa sababu ya mateso yao.
Baada ya muda mrefu, mfalme wa Misri akafa. Waisraeli wakalia kwa huzuni katika utumwa wao, walilia na kilio chao cha kutaka msaada kwa ajili ya utumwa kikamfikia Mungu.
24 Mungu aliposikia malalamiko yao, Mungu alikumbuka agano lake na Abrahamu, na Isaka, na Yakobo.
Mungu akasikia kilio chao cha huzuni, akakumbuka Agano alilofanya na Abrahamu pamoja na Isaki na Yakobo.
25 Mungu aliwaona Waisraeli na akaielewa hali yao.
Kwa hiyo Mungu akawaangalia Waisraeli na kuwahurumia.

< Kutoka 2 >