< Kutoka 2 >
1 Sasa mwanamme wa kabila la Lawi alimuoa mwanamke Mlawi.
2 Yule mwanamke akapata mimba na kuzaa mtoto wa kiume. Alipoona ya kuwa alikuwa mtoto mwenye afaya, alimficha kwa miezi mitatu.
3 Lakini alipokuwa hawezi kuendelea kumficha tena, alichukua kikapu cha manyasi akakipaka sifa na lami. Akamtia mtoto ndani yake na kukiweka juu ya maji katika majani kando ya mto.
4 Dada yake akasimama kwa mbali ili ajue yatakayompata.
5 Binti Farao akashuka kuoga mtoni wakati vijakazi wake wakitembea kando ya mto. Naye akaona kile kikapu katika majani na akamtuma kijakazi wake kwenda kukileta.
6 Alipokifungua, aliomwona mtoto. Tazama, mtoto alikuwa analia. Alimhurumia na kusema, “Bila shaka huyu ni mmoja wapo wa watoto wa Waebrania.”
7 Basi dada wa yule mtoto akamwambia binti Farao, “Je naweza kwenda kukutafutia mwanamke wa Kiebrania aje akulele mtoto kwa ajili yako?”
8 Binti Farao akamwambia, “Nenda.” Hivyo yule binti akaenda na kumwita mama yake yule mtoto.
9 Binti Farao akamwambia mama yake yule mtoto, “Mchukue mtoto huyu ukaninyonyeshee, nami nitakupa posho.” Hivyo yule mwanamke akamchukua mtoto na kumnyonyesha.
10 Mtoto alipokuwa mkubwa, akamleta kwa binti Farao, na akawa mtoto wake. Akamwita jina lake Musa akisema, “Kwa sababu nilimtoa katika maji.”
11 Musa alipokuwa mtu mzima, alienda kwa watu wake na kuona kazi ngumu walizokuwa wanafanya. Alimuona Mmisri akimpiga Mwebrania, mmoja wa watu wa jamii yake.
12 Aliangalia huku na kule, na alipoona ya kuwa hakuna mtu, alimuua yule mmisri na kuuficha mwili wake katika mchanga.
13 Alienda tena siku iliyofuata, na tazama, Waebrania wawili walikuwa wanapigana. Alimwambia yule aliyekuwa na makosa, “Kwa nini unampigia mwenzako?”
14 Lakini yule mtu alisema, “Ni nani aliyekuweka wewe kuwa kiongozi na mwamuzi juu yetu? Unataka kuniua na mimi kama ulivyomuua yule mmisri?” Ndipo Musa akaogopa na kusema, “Hakika niliyoyafanya yamejulikana.”
15 Farao aliposikia habari hizi, alijaribu kumuua Musa. Lakini Musa alikimbia na kwenda kuishi katika nchi ya Wamidiani. Kule alikaa chini kando ya mto.
16 Wakati huo kuhani wa Midiani alikuwa na mabinti saba. Walikuja mtoni kuchota maji na kujaza vyombo vyao ili wawanyweshe mifuko ya baba yao.
17 Wachungaji walikuja na kutaka kuwafukuza, lakini Musa alienda kuwasaidia. Kisha akawanywesha mifugo wao.
18 Wale mabinti walipoenda kwa Reueli baba yao, aliwauliza, “Kwa nini mmerudi nyumbani mapema hivi leo?”
19 Wakamwambia, “Mmisri mmoja alituokoa dhidi ya wachungaji. Pia alichota maji na kuwanywesha mifugo wetu.”
20 Kisha akawauliza binti zake, “Yu wapi sasa? Kwa nini mlimwacha? Mwiteni ili apate kula chakula pamoja nasi.”
21 Musa akakubali kukaa na yule mtu ambaye pia alimpa binti yake Zipora ili amuoe.
22 Alizaa mtoto wa kiume, na Musa akamwita jina lake Geshomu; akisema; “Nimekuwa mkazi katika nchi ya ugeni.”
23 Muda mrefu baadaye, mfalme wa Misri akafa. Waisraeli walilalamika kwa sababu ya kazi za utumwa. Walilia kutafuta msaada, na maombi yao yakamfikia Mungu kwa sababu ya mateso yao.
24 Mungu aliposikia malalamiko yao, Mungu alikumbuka agano lake na Abrahamu, na Isaka, na Yakobo.
25 Mungu aliwaona Waisraeli na akaielewa hali yao.