< Kutoka 10 >

1 Yahweh akamwambia Musa, “Nenda kwa Farao, kwa kuwa nimeufanya moyo wake mgumu na moyo wa watumishi wake. Nimefanya hivi kuonyesha hizi ishara za nguvu zangu miongoni mwao.
Ndipo Bwana akamwambia Mose, “Nenda kwa Farao, kwa kuwa nimeufanya moyo wake kuwa mgumu na mioyo ya maafisa wake ili kwamba nipate kutenda ishara hizi zangu za ajabu miongoni mwao
2 Pia nimefanya hivi ili muwaambie watoto wenu na wajukuu wenu vitu nilivyo fanya, jinsi nilivyo itendea Misri kwa ukali, na jinsi nilivyo onyesha aina tofauti za ishara za nguvu zangu miongoni mwao. Kwa hili mtajua kuwa mimi ni Yahweh.”
ili upate kuwaeleza watoto wako na wajukuu wako jinsi nilivyowatendea Wamisri kwa ukali na jinsi nilivyofanya ishara zangu miongoni mwao, nanyi mpate kujua kuwa Mimi ndimi Bwana.”
3 Hivyo Musa na Aruni wakaenda kwa Farao na kumwambia, “Yahweh, Mungu wa Waebrania, anasema hivi: 'Kwa muda gani utaendelea kukataa kujinyenyekesha mbele zangu? Acha watu wangu waenda ili wakaniabudu.
Kwa hiyo Mose na Aroni wakaenda kwa Farao na kumwambia, “Hili ndilo Bwana, Mungu wa Waebrania, asemalo: ‘Utaendelea hata lini kukataa kunyenyekea mbele yangu? Waachie watu wangu waende, ili wapate kuniabudu.
4 Lakini ukikataa kuwaruhusu watu wangu kwenda, sikiliza, kesho nitaleta nzige kwenye nchi yako.
Kama ukikataa kuwaachia waende, kesho nitaleta nzige katika nchi yako.
5 Watafunika ardhi ya juu ili kwamba mtu asiweze kuona udongo. Watakula mabaki yote yalio salia kwenye mvua ya barafu ya mawe. Pia watakula kila mti unaokua shambani.
Nao watafunika uso wa ardhi hata usionekane. Watatafuna mabaki machache yaliyobakizwa baada ya ile mvua ya mawe, yaani pamoja na kila mti unaoota katika mashamba yenu.
6 Watajaza nyumba zenu, zote za watumishi wenu, na zote za Wamisri wote - jambo ambalo baba zenu wala mababu zenu hawakuwai kuona, jambo ambalo halikuwai shuhudiwa toka walipo kuwa duniani hadi leo.”' Kisha Musa akaondoka na kutoka kwa Farao.
Nzige hao watajaza nyumba zako, za maafisa wako wote na za Wamisri wote. Jambo ambalo baba zenu wala babu zenu hawajapata kuona tangu siku ile walipoanza kuishi katika nchi hii mpaka leo hii.’” Ndipo Mose akageuka na kumwacha Farao.
7 Watumishi wa Farao wakamwambia, “Mpaka lini huyu mwanaume ata kuwa msumbufu kwetu? Acha Waisraeli waende wakamuabudu Yahweh Mungu wao. Bado haujatambua kuwa Misri imeharibiwa?”
Maafisa wa Farao wakamwambia, “Mpaka lini huyu mtu atakuwa tanzi kwetu? Waachie hao watu waende zao, ili wapate kumwabudu Bwana Mungu wao. Je, bado hutambui kuwa Misri imeangamia?”
8 Musa na Aruni wakaletwa tena kwa Farao, ambaye aliwaambia, “Nendeni amkamuabudu Yahweh Mungu wenu. Lakini watu gani wataenda?”
Ndipo Mose na Aroni wakaletwa kwa Farao. Farao akawaambia, “Nendeni, mkamwabudu Bwana Mungu wenu. Lakini ni nani hasa watakaokwenda?”
9 Musa akasema, “Tutaondoka na wadogo wetu na wakubwa wetu, pamoja na wana wetu na mabinti zetu. Tutaondoka na ng'ombe na kondoo zetu, maana lazima tufanye siku kuu ya Yahweh.”
Mose akajibu, “Tutakwenda na vijana wetu na wazee, pamoja na wana wetu na binti zetu, pia pamoja na kondoo zetu, ngʼombe, mbuzi, farasi na punda kwa sababu tutaadhimisha sikukuu kwa Bwana.”
10 Farao akawaambia, “Yahweh kwa kweli awe nanyi, kama nitawaacha muende na wadogo zenu waende. Angalia, una uovu kwenye nia.
Farao akasema, “Bwana awe pamoja nanyi, kama nikiwaruhusu mwondoke pamoja na wanawake wenu na watoto wenu! Ni wazi kwamba mna makusudi mabaya.
11 Hapana! Nenda, wanaume tu miongoni mwenu, na mmuabudu Yahweh, kwa kuwa hilo ndilo mnalo litaka.” Kisha Musa na Aruni wakaondolewa uweponi mwa Farao.
La hasha! Wanaume peke yao na waende, wakamwabudu Bwana, kwa kuwa hilo ndilo mmekuwa mkiomba.” Kwa hiyo Mose na Aroni wakaondolewa mbele ya Farao.
12 Kisha Yahweh akamwambia Musa, “Nyoosha mkono wako kwenye nchi ya Misri palipo na nzige, ili washambulie nchi ya Misri na kula kila mmea, kila kitu barua ya mawe iliyo acha.”
Basi Bwana akamwambia Mose, “Nyoosha mkono wako juu ya Misri ili kundi la nzige liweze kuingia juu ya nchi na kutafuna kila kitu kiotacho katika mashamba na kila kitu kilichosazwa na ile mvua ya mawe.”
13 Musa akanyoosha na gongo lake juu ya nchi ya Misri, na Yahweh akaleta upepo wa mashariki juu ya nchi mchana wote na usiku mzima. Palipo kuwa asubui, upepo wa mashariki ulileta nzige.
Kwa hiyo Mose akanyoosha fimbo yake juu ya Misri, Bwana akauleta upepo wa mashariki ukavuma katika nchi yote mchana wote na usiku kucha, kufikia asubuhi upepo ukawa umeleta nzige.
14 Nzige wakaenda nchi yote ya Misri na kuharibu sehemu zote. Hapajawai kuwa na kundi kama hilo la nzige juu ya nchi, hakuna kama tena kama hilo litawai kutokea.
Wakaivamia Misri yote na kukaa kila eneo la nchi kwa wingi. Kamwe hapajapata kuwepo pigo la nzige kama hilo, wala halitakuwepo tena.
15 Walifunika ardhi yote ya juu ikawa giza. Walikula kila mmea na kila tunda la miti ambayo barafu ya mawe ilibakiza. Kila eneo la nchi ya Misri, hakuna mmea wa kijani ulibaki, wala mti au mmea wa shambani.
Wakafunika ardhi yote mpaka ardhi ikawa nyeusi. Wakatafuna kile chote kilichokuwa kimebakizwa na ile mvua ya mawe, kila kitu kiotacho mashambani pamoja na matunda kwenye miti. Hakuna kitu chochote cha kijani kilichosalia katika miti au mmea katika nchi yote ya Misri.
16 Kisha Farao akawaita Musa na Aruni na kuwaambia, “Nimefanya dhambi dhidi ya Yahweh na dhidi yako.
Farao akawaita Mose na Aroni kwa haraka na kuwaambia, “Nimetenda dhambi dhidi ya Bwana Mungu wenu na dhidi yenu pia.
17 Kisha sasa, nisamehe dhambi yangu wakati huu, na uombe kwa Yahweh Mungu wako aondoe hichi kifo kwangu.”
Sasa unisamehe dhambi yangu mara moja tena na umwombe Bwana Mungu wako aondoe pigo hili baya kwangu.”
18 Musa akaondoka kwa Farao na kumuomba Yahweh.
Kisha Mose akaondoka kwa Farao akamwomba Bwana.
19 Yahweh akaleta upepo mkali wa magharibi ulio wachukuwa wale nzige na kuwapeleka Bahari ya Shamu; hakuna nzige ata mmoja aliye baki eneo la Misri.
Naye Bwana akaugeuza upepo ukavuma kutoka magharibi, wenye nguvu nyingi, ambao uliwaondoa wale nzige na kuwapeleka kwenye Bahari ya Shamu. Hakuna nzige hata mmoja aliyebaki popote katika nchi ya Misri.
20 Lakini Yahweh aliufanya moyo wa Farao mgumu, na Farao hakuacha Waisraeli waende.
Lakini Bwana akaufanya moyo wa Farao kuwa mgumu, wala hakuwaachia Waisraeli waondoke.
21 Kisha Yahweh akamwambia Musa, “Nyoosha mkono wako kuelekea mbingu, ili kuwe na giza nchi yote ya Misri, giza linalo weza kuhisiwa.”
Kisha Bwana akamwambia Mose, “Nyoosha mkono wako kuelekea angani ili giza litande katika nchi ya Misri, giza ambalo watu wanaweza kulipapasa na kulihisi.”
22 Musa akanyoosha mkono wake kuelekea mbingu, na kulikuwa na giza nene nchi yote ya Misri kwa siku tatu.
Kwa hiyo Mose akaunyoosha mkono wake kuelekea angani, na giza nene likafunika pote katika nchi ya Misri kwa muda wa siku tatu.
23 Hakuna aliye muona mwingine; hakuna aliye toka nyumbani mwake kwa siku tatu. Walakini, Waisraeli wote walikuwa na taa katika sehemu walizo ishi.
Hakuna mtu yeyote aliyeweza kumwona mwenzake, wala kuondoka mahali alipokuwa kwa muda wa siku tatu. Lakini Waisraeli wote walikuwa na mwanga katika maeneo yao waliyokuwa wanaishi.
24 Farao alimuita Musa na kusema, “Nenda umuabudu Yahweh. Ata familia zenu za weza kwenda nanyie, lakini ng'ombe zenu na kondoo zenu zitabaki.”
Ndipo Farao akamwita Mose na kusema, “Nendeni, mkamwabudu Bwana. Hata wanawake na watoto wenu mwaweza kwenda nao pia, lakini kondoo, mbuzi na ngʼombe wenu waacheni.”
25 Lakini Musa akasema, “Lazima utupe wanyama kwa ajili ya dhabihu na sadaka za kuteketeza ili tuwatoe dhabihu kwa Yahweh Mungu wetu.
Lakini Mose akasema, “Huna budi kuturuhusu tuwe na dhabihu na sadaka za kuteketezwa za kutoa mbele za Bwana Mungu wetu.
26 Mifugo yetu lazima iende na sisi; ata mmoja hawezi kubaki, lazima tuwapeleke wakamuabudu Yahweh Mungu wetu. Kwa kuwa hatujui tutakacho muabudu nacho Yahweh mpaka tufike pale.
Sisi ni lazima tuondoke na mifugo yetu pia, wala hakuna ukwato utakaoachwa nyuma. Inatupasa kutumia baadhi ya hiyo mifugo katika kumwabudu Bwana Mungu wetu, kwa kuwa mpaka tutakapofika huko hatutakuwa tumefahamu ni nini tutakachotumia katika kumwabudu Bwana.”
27 Lakini Yahweh aliufanya moyo wa Farao mgumu, na hakuwaacha waende.
Lakini Bwana akaufanya moyo wa Farao kuwa mgumu, hakuwa radhi kuwaachia waondoke.
28 Farao alimwambia Musa, “Toka kwangu! Kuwa muangalifu na jambo moja, kwamba usinione tena, kwa kuwa siku utakapo uona uso wangu, utakufa.”
Farao akamwambia Mose, “Ondoka mbele yangu! Hakikisha kuwa hutakuja mbele yangu tena! Siku ile utakapouona uso wangu utakufa.”
29 Musa akasema, “Wewe mwenyewe umesema. Sitauona uso wako tena.”
Mose akamjibu, “Iwe kama ulivyosema! Kamwe sitauona uso wako tena.”

< Kutoka 10 >