< Waefeso 1 >
1 Paulo, mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, kwa waliotengwa kwa ajili ya Mungu walioko Efeso na ambao ni waaminifu katika Kristo Yesu.
Paulo, mtume wa Kristo Yesu, kwa mapenzi ya Mungu: Kwa watakatifu walioko Efeso, walio waaminifu katika Kristo Yesu:
2 Neema iwe kwenu na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo.
Neema na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana wetu Yesu Kristo iwe nanyi.
3 Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo apewe sifa. Ni yeye aliyetubariki kwa kila baraka za kiroho, katika mahali pa mbingu ndani ya Kristo.
Ahimidiwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki sisi kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho ndani ya Kristo.
4 Kabla ya kuumbwa ulimwengu, Mungu alituchagua sisi ambao tunaamini katika Kristo. Alituchagua sisi ili tuweze kuwa watakatifu na tusiolaumika mbele yake.
Kwa maana alituchagua katika yeye kabla ya kuumbwa ulimwengu ili tuwe watakatifu na bila lawama mbele zake. Kwa upendo
5 Katika pendo Mungu alituchagua mwanzo kwa kututwaa kama watoto wake kwa njia ya Yesu Kristo. Alifanya hivi kwa sababu alipendezwa kufanya kile alichotamani.
alitangulia kutuchagua tuwe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo kwa furaha yake na mapenzi yake mwenyewe.
6 Matokeo yake ni kwamba Mungu anatukuzwa kwa neema ya utukufu wake. Hiki ndicho alichotupatia bure kwa njia ya mpendwa wake.
Kwa hiyo tunamsifu Mungu kwa huruma zake kuu alizotumiminia sisi katika Mwanawe Mpendwa.
7 Kwa kuwa katika mpendwa wake, tunaukombozi kupitia damu yake, msamaha wa dhambi. Tunalo hili kwa sababu ya utajiri wa neema yake.
Ndani yake tunao ukombozi kwa njia ya damu yake, yaani, msamaha wa dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake
8 Alifanya neema hii kuwa nyingi kwa ajili yetu katika hekima na ufahamu.
aliyotumiminia kwa wingi, kwa hekima yote na maarifa yote.
9 Mungu alifanya ijulikane kwetu ile kweli iliyofichika ya mpango, kutokana na hamu iliyodhihirishwa ndani ya Kristo.
Naye alitujulisha siri ya mapenzi yake sawasawa na uradhi wa mapenzi yake, ambayo alikusudia katika Kristo,
10 Wakati nyakati zimetimia kwa utimilifu wa mpango wake, Mungu ataviweka pamoja kila kitu cha mbinguni na cha juu ya nchi ndani ya Kristo.
ili yapate kutimizwa wakati mkamilifu utakapowadia, yaani, kuvitia vitu vyote vya mbinguni na vya duniani pamoja, chini ya kiongozi mmoja, ndiye Kristo.
11 Katika Kristo tulikuwa tumechaguliwa na kukusudiwa kabla ya wakati. Hii ilikuwa ni kutokana na mpango wa anayefanya vitu vyote kwa kusudi la mapenzi yake.
Katika Kristo sisi nasi tumepata urithi, tukisha kuchaguliwa sawasawa na kusudi la Mungu, yeye ambaye hufanya mambo yote kulingana na kusudi la mapenzi yake,
12 Mungu alifanya hivyo ili kwamba tuweze kuwapo kwa sifa ya utukufu wake. Tulikuwa wa kwanza kuwa na ujasiri ndani ya Kristo.
ili kwamba, sisi tuliokuwa wa kwanza kuweka tumaini katika Kristo, tupate kuishi kwa sifa ya utukufu wake.
13 Ilikuwa kwa njia ya Kristo kwamba mlisikia neno la kweli, injili ya wokovu wenu kwa njia ya Kristo. Ilikuwa katika yeye pia kwamba mmeamini na kutiwa mhuri na Roho Mtakatifu aliye ahidiwa.
Ninyi pia mliingia ndani ya Kristo mliposikia Neno la kweli, Injili ya wokovu wenu. Mkiisha kuamini, ndani yake mlitiwa muhuri, yaani, Roho Mtakatifu mliyeahidiwa,
14 Roho ndiyo dhamana ya urithi wetu mpaka umiliki utakapopatikana. Hii ilikuwa ni kwa sifa ya utukufu wake.
yeye ambaye ni amana yetu akituhakikishia urithi wetu hadi ukombozi wa wale walio milki ya Mungu kwa sifa ya utukufu wake.
15 Kwa sababu hii, tangu wakati niliposikia kuhusu imani yenu ndani ya Bwana Yesu na kuhusu pendo lenu kwa wale wote ambao wametengwa kwa ajili yake.
Kwa sababu hii, tangu niliposikia juu ya imani yenu katika Bwana Yesu na upendo wenu kwa watakatifu wote,
16 Sijaacha kumshukuru Mungu kwa ajili yenu na kuwataja katika maombi yangu.
sijaacha kumshukuru Mungu kwa ajili yenu, nikiwakumbuka katika maombi yangu.
17 Ninaomba kwamba Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, baba wa utukufu, atawapeni roho ya hekima, mafunuo ya ufahamu wake.
Nazidi kumwomba Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awajalieni ninyi roho ya hekima na ya ufunuo, ili mpate kumjua zaidi.
18 Ninaomba kwamba macho yenu ya moyoni yatiwe nuru kwa ninyi kujua ni upi ujasiri wa kuitwa kwenu. Naomba kwamba mjue utajiri wa utukufu wa urithi wake miongoni mwa wale waliotengwa kwa ajili yake.
Ninaomba pia kwamba macho ya mioyo yenu yatiwe nuru ili mpate kujua tumaini mliloitiwa, utajiri wa urithi wa utukufu wake kwa watakatifu
19 Naomba kwamba ujue ukuu uzidio wa nguvu yake ndani yetu ambao tunaamini. Huu ukuu ni kutokana na kufanya kazi katika nguvu zake.
na uweza wake mkuu usiolinganishwa kwa ajili yetu sisi tuaminio. Uweza huo unaofanya kazi ndani yetu, ni sawa na ile nguvu kuu mno
20 Hii ni nguvu iliyofanya kazi ndani ya Kristo wakati Mungu alipomfufua kutoka kwa wafu na kumketisha katika mkono wake wa kuume katika mahali pa mbingu.
aliyoitumia katika Kristo alipomfufua kutoka kwa wafu, na akamketisha mkono wake wa kuume huko mbinguni,
21 Alimketisha Kristo juu mbali na utawala, mamlaka, nguvu, enzi, na kila jina litajwalo. Alimketisha Yesu si tu kwa wakati huu lakini kwa wakati ujao pia. (aiōn )
juu sana kuliko falme zote na mamlaka, enzi na milki, na juu ya kila jina litajwalo, si katika ulimwengu huu tu, bali katika ule ujao pia. (aiōn )
22 Mungu amevitiisha vitu vyote chini ya miguu ya Kristo. Amemfanya yeye kichwa juu ya vitu vyote katika kanisa.
Naye Mungu ameweka vitu vyote viwe chini ya miguu yake na amemfanya yeye awe kichwa cha vitu vyote kwa ajili ya Kanisa,
23 Ni kanisa kwamba ndilo mwili wake, ukamilifu wake ambaye hujaza vitu vyote katika njia zote.
ambalo ndilo mwili wake, ukamilifu wake yeye aliye yote katika yote.