< Waefeso 4 >

1 Kwa hiyo, kama mfungwa kwa ajili ya Bwana, nawasihi mtembee sawasawa na wito ambao Mungu aliwaita.
Basi, mimi niliye mfungwa wa Bwana, nawasihi mwenende kama inavyostahili wito wenu mlioitiwa.
2 Muishi kwa unyenyekevu mkuu na upole na uvumilivu. Mkichukuliana katika upendo.
Kwa unyenyekevu wote na upole, mkiwa wavumilivu, mkichukuliana kwa upendo.
3 Fanyeni bidii kuutunza umoja wa Roho katika kifungo cha amani.
Jitahidini kudumisha umoja wa Roho katika kifungo cha amani.
4 Kuna mwili mmoja na Roho moja, kama ambavyo pia mlikuwa mmeitwa katika uhakika wa taraja moja la wito wenu.
Kuna mwili mmoja na Roho mmoja, kama vile mlivyoitwa katika tumaini moja.
5 Na kuna Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja,
Tena kuna Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja,
6 na Mungu mmoja na Baba wa wote. Yeye yuko juu ya yote, na katika yote na ndani ya yote.
Mungu mmoja ambaye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote, katika yote na ndani ya yote.
7 Kwa kila mmoja wetu amepewa kipawa kulingana na kipimo cha kipawa cha Kristo.
Lakini kila mmoja wetu amepewa neema kwa kadiri ya kipimo cha kipawa cha Kristo.
8 Ni kama maandiko yasemavyo: “Alipopaa juu sana, aliongoza mateka katika utumwa. Akatoa vipawa kwa watu.”
Kwa hiyo husema: “Alipopaa juu zaidi, aliteka mateka, akawapa wanadamu vipawa.”
9 Ni nini maana ya, “Alipaa,” isipokuwa kwamba alishuka pia pande za chini za dunia?
(Asemapo “alipaa juu,” maana yake nini isipokuwa ni kusema pia kwamba Kristo alishuka pande za chini sana za dunia?
10 Yeye ambaye alishuka ni mtu yuleyule ambae pia alipaa mbali juu ya mbingu zote. Alifanya hivi ili uwepo wake uwe katika vitu vyote.
Yeye aliyeshuka ndiye alipaa juu zaidi kupita mbingu zote, ili apate kuujaza ulimwengu wote.)
11 Kristo alitoa vipawa kama hivi: mitume, manabii, wainjilisti, wachungaji, na waalimu.
Ndiye aliweka wengine kuwa mitume, wengine kuwa manabii, wengine kuwa wainjilisti, wengine kuwa wachungaji na walimu,
12 Alifanya hivi kuwawezesha waumini kwa ajili ya kazi ya huduma, kwa ajili ya kuujenga mwili wa Kristo.
kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu kwa ajili ya kazi za huduma, ili kwamba mwili wa Kristo upate kujengwa
13 Anafanya hivi hadi sisi sote tufikie umoja wa imani na maarifa ya mwana wa Mungu. Anafanya hivi hadi tuweze kukomaa kama wale waliofikia kimo kamili cha Kristo.
mpaka sote tutakapoufikia umoja katika imani na katika kumjua sana Mwana wa Mungu na kuwa watu wazima kwa kufikia kimo cha ukamilifu wa Kristo.
14 Hii ni ili kwamba tusiwe tena kama watoto, tusirushwerushwe huku na huko. Ili kwamba tusichukuliwe na kila aina ya upepo wa fundisho, kwa hila za watu katika ujanja wa udanganyifu uliopotoka.
Ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwatupwa huku na huku na kuchukuliwa na kila upepo wa mafundisho kwa hila za watu, kwa ujanja, kwa kufuata njia zao za udanganyifu.
15 Badala yake, tutaongea ukweli katika upendo na kukua zaidi katika njia zote ndani yake ambaye ndiye kichwa, Kristo.
Badala yake, tukiambiana kweli kwa upendo, katika mambo yote tukue, hata tumfikie yeye aliye kichwa, yaani, Kristo.
16 Kristo ameunganisha, kwa pamoja, mwili wote wa waumini. Umeungamanishwa pamoja na kila kiungo ili kwamba mwili wote ukue na kujijenga wenyewe katika upendo.
Kutoka kwake, mwili wote ukiwa umeungamanishwa na kushikamanishwa pamoja kwa msaada wa kila kiungo, hukua na kujijenga wenyewe katika upendo, wakati kila kiungo kinafanya kazi yake.
17 Kwa hiyo, nasema hili, na nawasihi katika Bwana: Msitembee tena kama watu wa mataifa wanavyotembea katika ubatili wa akili zao.
Hivyo nawaambia hivi, nami nasisitiza katika Bwana kwamba, msiishi tena kama watu wa Mataifa waishivyo, katika ubatili wa mawazo yao.
18 Wametiwa giza katika mawazo yao. Wamefukuzwa kutoka katika uzima wa Mungu kwa ujinga ulio ndani yao kwa sababu ya ugumu wa mioyo yao.
Watu hao akili zao zimetiwa giza na wametengwa mbali na uzima wa Mungu kwa sababu ya ujinga wao kutokana na ugumu wa mioyo yao.
19 Hawajisikii aibu. Wamejikabidhi wenyewe kwa ufisadi katika matendo machafu, katika kila aina ya uchoyo.
Wakiisha kufa ganzi, wamejitia katika mambo ya ufisadi na kupendelea kila aina ya uchafu, wakiendelea kutamani zaidi.
20 Lakini, hivi sivyo mlivyojifunza kuhusu Kristo.
Lakini ninyi, hivyo sivyo mlivyojifunza Kristo.
21 Nadhani kwamba mmesikia kuhusu yeye. Nadhani kwamba mmekuwa mkifundishwa katika yeye, kama tu ukweli ulivyo ndani ya Yesu.
Kama hivyo ndivyo ilivyo, ninyi mmemsikia, tena mmefundishwa naye, vile kweli ilivyo katika Yesu.
22 Lazima mvue mambo yote yanayoendana na mwenendo wenu wa zamani, utu wa zamani. Ni utu wa zamani unaooza kwa sababu ya tamaa za udanganyifu.
Mlifundishwa kuuvua mwenendo wenu wa zamani, utu wenu wa kale, ulioharibiwa na tamaa zake za udanganyifu,
23 Vueni utu wenu wa zamani ili kwamba mfanywe upya katika roho ya akili zenu.
ili mfanywe upya roho na nia zenu,
24 Fanyeni hivi ili muweze kuvaa utu mpya, unaoendana na Mungu. Umeumbwa katika haki na utakatifu wa kweli.
mkajivike utu mpya, ulioumbwa sawasawa na mfano wa Mungu katika haki yote na utakatifu.
25 Kwa hiyo, weka mbali udanganyifu. “Ongeeni ukweli, kila mmoja na jirani yake,” kwa sababu tu washirika kwa kila mmoja kwa mwenzake.
Kwa hiyo kila mmoja wenu avue uongo na kuambiana kweli mtu na jirani yake, kwa maana sisi sote tu viungo vya mwili mmoja.
26 Mwe na hasira, lakini msitende dhambi.” Jua lisizame mkiwa katika hasira zenu.
Mkikasirika, msitende dhambi, wala jua lisichwe mkiwa bado mmekasirika,
27 Msimpe Ibilisi nafasi.
wala msimpe ibilisi nafasi.
28 Yeyote aibaye lazima asiibe tena. Badala yake ni lazima afanye kazi. Afanye kazi yenye manufaa kwa mikono yake, ili kwamba aweze kumhudumia mtu aliye na hitaji.
Yeye ambaye amekuwa akiiba, asiibe tena, lakini lazima ajishughulishe, afanye kitu kifaacho kwa mikono yake mwenyewe, ili awe na kitu cha kuwagawia wahitaji.
29 Kauli mbaya isitoke kinywani mwenu. Badala yake, maneno lazima yatoke katika vinywa vyenu yafaayo kwa mahitaji, kuwapa faida wale wanaosikiliza.
Maneno mabaya yasitoke vinywani mwenu, bali yale yafaayo kwa ajili ya kuwajenga wengine kulingana na mahitaji yao, ili yawafae wale wasikiao.
30 Na msimhuzunishe Roho Mtakatifu wa Mungu. Ni kwa Yeye kwamba mmewekewa muhuri kwa ajili ya siku ya ukombozi.
Wala msimhuzunishe Roho Mtakatifu wa Mungu, ambaye kwake mlitiwa muhuri kwa ajili ya siku ya ukombozi.
31 Lazima muweke mbali uchungu wote, ghadhabu, hasira, ugomvi, na matusi, pamoja na kila aina ya uovu. Iweni wema ninyi kwa ninyi.
Ondoeni kabisa uchungu, ghadhabu, hasira, makelele na masingizio pamoja na kila aina ya uovu.
32 Mwe na huruma. Msameheane ninyi kwa ninyi, kama vile Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi.
Kuweni wafadhili na wenye kuhurumiana ninyi kwa ninyi, mkisameheana, kama vile naye Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi.

< Waefeso 4 >