< Waefeso 2 >
1 Kama vile mlivyo kuwa mmekufa katika makosa na dhambi zenu.
2 Ilikuwa katika haya kwamba kwanza mlienenda kulingana na nyakati za ulimwengu huu. Mlikuwa mkienenda kwa kufuata mtawala wa mamlaka ya anga. Hii ndiyo roho yake yule afanyaye kazi katika wana wa kuasi. (aiōn )
3 Sisi wote hapo mwanzo tulikuwa miongoni mwa hawa wasioamini. Tulikuwa tukitenda kwa namna ya tamaa mbaya za miili yetu. Tulikuwa tukifanya mapenzi ya mwili na ufahamu wetu. Tulikuwa kwa asili wana wa ghadhabu kama wengine.
4 Lakini Mungu ni mwingi wa rehema kwa sababu ya pendo lake kubwa alilotupenda sisi.
5 Wakati tulipokuwa wafu katika makosa yetu, alituleta pamoja katika maisha mapya ndani ya Kristo. Ni kwa neema kwamba mmeokolewa.
6 Mungu alitufufua pamoja na kutufanya kukaa pamoja katika mahali pa mbingu ndani ya Kristo Yesu.
7 Alifanya hivi ili katika nyakati zijazo aweze kutuonesha utajiri mkuu wa neema yake. Hutuonesha sisi hili kwa njia ya wema wake ndani ya Kristo Yesu. (aiōn )
8 Kwa neema mmeokolewa kwa njia ya imani. Na hii haikutoka kwetu. Ni zawadi ya Mungu.
9 Haitokani na matendo. Matokeo yake, asiwepo mmoja wapo wa kujisifu.
10 Kwa sababu sisi tu kazi ya Mungu, tumeumbwa katika Kristo Yesu kutenda matendo mema. Ni matendo haya ambayo Mungu aliyapanga tangu zamani za kale kwa ajili yetu, ili tutembee katika hayo.
11 Kwa hiyo kumbukeni kwamba hapo zamani mlikuwa watu wa Mataifa kwa jinsi ya mwili. Mnaitwa “msio na tohara” kwa kile kinachoitwa tohara ya mwili inayofanywa kwa mikono ya binadamu.
12 Kwa wakati huo mlikuwa mmetengwa na Kristo. Mlikuwa wageni kwa watu wa Israel. Mlikuwa wageni kwa agano la ahadi. Hamkuwa na uhakika wa wakati ujao. Mlikuwa bila Mungu katika ulimwengiu.
13 Lakini sasa katika Kristo Yesu ninyi ambao hapo mwanzo mlikuwa mbali na Mungu mmeletwa karibu na Mungu kwa damu ya Kristo.
14 Kwa maana yeye ndiye amani yetu. Alifanya wawili kuwa mmoja. Kwa mwili wake aliuharibu ukuta wa utengano ambao ulikuwa umetutenganisha, huo uadui.
15 Kwamba alikomesha sheria ya amri na kanuni ili kwamba aumbe mtu mmoja mpya ndani yake. Akafanya amani.
16 Alifanya hivi ili kuwapatanisha makundi mawili ya watu kuwa mwili mmoja kwa Mungu kupitia msalaba. Kwa njia ya msalaba aliufisha uadui.
17 Yesu alikuja na kutangaza amani kwenu ninyi mliokuwa mbali na amani kwao wale waliokuwa karibu.
18 Kwa maana kwa njia ya Yesu sisi wote wawili tuna nafasi kwa yule Roho mmoja kuingia kwa Baba.
19 Hivyo basi, ninyi watu wa mataifa si wasafiri na wageni tena. Bali ni wenyeji pamoja na wale waliotengwa kwa ajili ya Mungu na wajumbe katika nyumba ya Mungu.
20 Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii. Kristo Yesu mwenyewe alikuwa jiwe kuu la pembeni.
21 Katika yeye jengo lote limeungamanishwa pamoja na kukua kama hekalu ndani ya Bwana.
22 Ni ndani yake ninyi nanyi mnajengwa pamoja kama mahali pa kuishi pa Mungu katika Roho.