< Torati 34 >
1 Musa aliondoka kutoka nyanda za Moabu mpaka mlima wa Nebo, hadi kilele cha Pisga, kilicho mkabala na Yericho. Huko Yahwe alimwonyesha nchi yote ya Gileadi kutoka umbali wa Dani,
Kisha Mose akaupanda mlima Nebo kutoka tambarare za Moabu mpaka kilele cha Pisga, ngʼambo ya Yeriko. Huko Bwana akamwonyesha nchi yote: kutoka Gileadi mpaka Dani,
2 na Naftali yote, na nchi ya Efraimu na Manase, na nchi yote ya Yuda, mpaka bahari ya magharibi,
Naftali yote, nchi ya Efraimu na Manase, nchi yote ya Yuda mpaka bahari ya magharibi,
3 na Negevi, na uwanda wa bonde la Yericho, mji wa mitende, mpaka umbali wa Soari.
Negebu na nchi yote kuanzia Bonde la Yeriko, Mji wa Mitende, hadi Soari.
4 Yahwe alimwambia, “Hii ni nchi niliyoapa kwa Abrahamu, kwa Isaka, na kwa Yakobo, na kusema, “Nitawapatia uzao wako.” Nimekuruhusu uitazame kwa macho yako, lakini hautakwenda kule.”
Kisha Bwana akamwambia, “Hii ndiyo nchi niliyomwahidi Abrahamu na Isaki na Yakobo kwa kiapo niliposema, ‘Nitawapa wazao wako.’ Nimekuruhusu uione kwa macho yako, lakini hutavuka kuingia.”
5 Basi Musa mtumishi wa Yahwe, alikufa pale katika nchi ya Moabu, kama neno la Yahwe lilivyoahidi.
Naye Mose mtumishi wa Bwana akafa huko Moabu, kama Bwana alivyokuwa amesema.
6 Yahwe alimzika katika bonde katika nchi ya Moabu mkabala na Beth-peori, lakini hakuna ajuaye kaburi lake lilipo hadi leo hii.
Mungu akamzika huko Moabu, katika bonde mkabala na Beth-Peori, lakini hakuna ajuaye kaburi lake lilipo mpaka leo.
7 Musa alikuwa na umri wa miaka mia moja na ishirini alipokufa; macho yake hayakufifia, wala nguvu asili zake hazikupungua.
Mose alikuwa na umri wa miaka mia moja na ishirini alipofariki; hata hivyo nguvu ya macho yake haikufifia wala mwili wake haukudhoofika.
8 Watu wa Israeli walimuomboleza Musa katika nyanda za Moabu kwa siku thelathini, hapo ndipo siku za maombolezo ya Musa zilipotimia.
Waisraeli wakaomboleza kwa ajili ya Mose kwenye tambarare za Moabu kwa siku thelathini, mpaka wakati wa kulia na kuomboleza ulipopita.
9 Yoshua mwana wa Nuni alikuwa amejawa na roho ya hekima, kwa maana Musa alimwekea mkono juu yake. Watu wa Israeli walimsikiliza na kufanya yale ambayo Yahwe alimuamuru Musa.
Basi Yoshua mwana wa Nuni alijazwa roho ya hekima kwa sababu Mose alikuwa ameweka mikono yake juu yake. Kwa hiyo Waisraeli wakamsikiliza na wakafanya yale ambayo Bwana alikuwa amemwagiza Mose.
10 Tangu hapo hakujatokea nabii katika Israeli kama Musa, ambaye Yahwe alimjua uso kwa uso.
Tangu wakati huo, katika Israeli hajainuka nabii mwingine kama Mose, ambaye Bwana alimjua uso kwa uso,
11 Hakujawahi kuwa na nabii yeyote kama yeye kwa ishara na miujiza ambayo Yahwe alimtuma kufanya katika nchi ya Misri, kwa Farao, na kwa watumishi wake, na kwa nchi yake yote.
aliyetenda ishara zote zile za miujiza na maajabu ambayo Bwana alimtuma kuyatenda huko Misri, yaani kwa Farao na maafisa wake wote na nchi yake yote.
12 Hakujawahi kuwa na nabii yeyote kama yeye kwa mambo yote makubwa, ya kutisha ambayo Musa aliyafanya machoni pa Israeli yote.
Kwa kuwa hakuna mtu yeyote aliyewahi kuonyesha nguvu nyingi ama kutenda matendo ya kutisha ambayo Mose aliwahi kuyafanya mbele ya Israeli yote.