< Torati 31 >
1 Musa alikwenda na kuzungumza maneno haya kwa Israeli yote.
Kisha Mose akaenda akasema maneno haya kwa Waisraeli wote:
2 Alisema kwao, “Kwa sasa nina umri wa miaka mia moja na ishirini; Siwezi kutoka na kuingia tena; Yahwe ameniambia, “Hautavuka Yordani hii”
“Sasa nina miaka mia moja na ishirini nami siwezi tena kuwaongoza. Bwana ameniambia, ‘Hutavuka Yordani.’
3 Yahwe Mungu wako, atakutangulia mbele yako; ataangamiza mataifa haya mbele yako, nawe utawanyanganya. Yoshua atakwenda kabla yako, kama Yahwe alivyonena.
Bwana Mungu wenu, yeye mwenyewe atavuka mbele yenu. Ataangamiza mataifa haya mbele yenu, nanyi mtaimiliki nchi yao. Pia Yoshua atavuka mbele yenu, kama Bwana alivyosema.
4 Yahwe atawafanya kwao kama alivyofanya kwa Sihoni na kwa Ogu, wafalme wa Waamori, na kwa nchi yao, aliyoiangamiza.
Naye Bwana atawafanyia watu hao kile alichowafanyia Sihoni na Ogu, wafalme wa Waamori, ambao aliwaangamiza pamoja na nchi yao.
5 Yahwe atakupatia ushindi juu yao utakapokutana nao vitani, nawe utafanya kwao yote ntakayokuamuru.
Bwana atawakabidhi kwenu, nanyi lazima mwatendee yale yote niliyowaamuru.
6 Uwe hodari na mwenye ujasiri mwema, usiogope, na usiwaogope; kwa maana Yahwe Mungu wako, ni yeye aendaye kabla yako; hatakuangusha wala kukuacha.”
Kuweni imara na moyo wa ushujaa. Msiogope wala msifadhaike kwa sababu yao, kwa kuwa Bwana Mungu wenu anakwenda pamoja nanyi; kamwe hatawaacha wala hatawatupa ninyi.”
7 Musa akamwita Yoshua na akamwambia machoni pa Israeli yote, “Uwe hodari na mwenye ujasiri mwema, kwa kuwa utaondoka na hawa watu katika nchi ambayo Yahwe ameapa kwa mababu zao kuwapatia; utafanya wairithi.
Kisha Mose akamwita Yoshua na akamwambia mbele ya Israeli wote, “Uwe imara na moyo wa ushujaa, kwa kuwa ni lazima uende na watu hawa katika nchi ile Bwana aliyowaapia baba zao kuwapa, nawe ni lazima uwagawie kama urithi wao.
8 Yahwe, yeye ndiye atakwenda kabla yako; atakuwa pamoja nawe; hatakuangusha wala hatakutelekeza; usiogope, usivunjike moyo.”
Bwana mwenyewe atakutangulia naye atakuwa pamoja nawe; kamwe hatakuacha wala hatakutupa. Usiogope, wala usifadhaike.”
9 Musa aliandika sheria hii na kuwapatia makuhani, wana wa Walawi, ambao walibeba sanduku la agano la Yahwe; pia aligawa nakala zake kwa wazee wote wa Israeli.
Kwa hiyo Mose akaandika sheria hii na kuwapa makuhani, wana wa Lawi, waliochukua Sanduku la Agano la Bwana na wazee wote wa Israeli.
10 Musa aliwaamuru na kusema, “Katika kila mwisho wa miaka saba, kwa muda uliowekwa wa kudumu kwa ajili ya kufuta madeni, katika Sikukuu ya Vibanda,
Kisha Mose akawaamuru, akasema: “Mwishoni mwa kila miaka saba, katika mwaka wa kufuta madeni, wakati wa Sikukuu ya Vibanda,
11 ambapo Israeli yote imekuja kujitokeza mbele ya Yahwe Mungu wako katika mahali atakayochagua kuwa patakatifu pake, utasoma sheria hii mbele ya Israeli yote wakisikia.
Waisraeli wote wanapokuja mbele za Bwana Mungu wenu mahali atakapopachagua, utasoma sheria hii mbele yao masikioni mwao.
12 Kusanya watu, wanaume, wanawake, na wadogo, na mgeni wako aliye miongoni mwa malango yako, ili waweze kusikia na kujifunza, na ili kwamba wamheshimu Yahwe Mungu wako na kushika maneno yote ya sheria hii.
Kusanya watu wote, wanaume, wanawake, watoto na wageni wanaoishi katika miji yenu, ili waweze kusikia na kujifunza kumcha Bwana Mungu wenu na kufuata kwa bidii maneno yote ya sheria hii.
13 Fanya hivi ili kwamba watoto wao, ambao hawajajua, waweze kusikia na kujifunza kumheshimu Yahwe Mungu wako, maadamu unaishi katika nchi ambayo utaenda juu ya Yordani kuimiliki.”
Watoto wao, ambao hawaijui sheria hii, lazima waisikie na kujifunza kumcha Bwana Mungu wenu kwa muda mtakaoishi katika nchi mnayovuka Yordani kuimiliki.”
14 Yahwe alimwambia Musa, “Tazama, siku inakuja ambayo lazima utakakufa; muite Yoshua na mjidhihirishe katika hema la makutano, ili kwamba niweze kuwapatia amri.” Musa an Yoshua waliondoka na kujidhihirisha katika hema la makutano.
Bwana akamwambia Mose, “Sasa siku ya kifo chako imekaribia. Mwite Yoshua, mkajihudhurishe katika Hema la Kukutania, mahali nitakapompa maagizo ya kazi.” Kwa hiyo Mose na Yoshua wakaja na kujihudhurisha kwenye Hema la Kukutania.
15 Yahwe alijifunua kwenye hema kwa nguzo ya wingu; nguzo ya wingu ilisimama juu ya mlango wa hema.
Kisha Bwana akatokea katika Hema katika nguzo ya wingu, nalo wingu likasimama juu ya ingilio la Hema.
16 Yahwe alimwambia Musa, “Tazama, utalala na baba zako; watu hawa watainuka na kujifanya kama kahaba na kwenda kwa miungu ya ajabu ambayo imo miongoni mwao katika nchi wanapokwenda. Wataniacha na kuvunja agano langu ambalo nimefanya nao.
Kisha Bwana akamwambia Mose: “Unakwenda kupumzika na baba zako, nao watu hawa hivi karibuni watazini na miungu migeni ya nchi wanayoingia. Wataniacha na kuvunja Agano nililofanya nao.
17 Basi, katika siku hiyo, hasira yangu itawaka dhidi yao nami nitawaacha. Nitaficha uso wangu kwao nao watamezwa. Maafa na taabu nyingi yatawakumba ili waseme katika siku hiyo, “Maafa haya hayajaja kwetu kwa sababu Mungu hayupo kati yetu?”
Siku hiyo nitawakasirikia na kuwaacha; nitawaficha uso wangu, nao wataangamizwa. Maafa mengi na shida nyingi zitakuja juu yao, nao siku hiyo watauliza, ‘Je, maafa haya hayakuja juu yetu kwa sababu Mungu wetu hayuko pamoja nasi?’
18 Hakika nitaficha uso wangu kwao katika siku hiyo kwa sababu ya uovu wote ambao watakuwa wametenda, kwa sababu wamegeukia miungu mingine.
Nami hakika nitauficha uso wangu siku hiyo kwa sababu ya maovu yao yote kwa kugeukia miungu mingine.
19 Basi sasa andika wimbo huu kwa ajili yenu na wafundishe watu wa Israeli. Uweke vinywani mwao, ili kwamba wimbo huu uweze kuwa shahidi kwangu dhidi ya watu wa Israeli.
“Sasa ujiandikie wimbo huu, uwafundishe Waisraeli na uwaamuru wauimbe, ili upate kuwa ushahidi wangu dhidi yao.
20 Kwa maana nitakapowaleta katika nchi ambayo niliapa kwa mababu zao, nchi inayotiririka kwa maziwa na asali, na watakapokula na kuridhika na kunenepa, ndipo watageukia miungu mingine nao watawatumikia na kunidharau na watavunja agano langu.
Nitakapokwisha kuwaingiza katika nchi itiririkayo maziwa na asali, nchi niliyowaahidi baba zao kwa kiapo, nao watakapokula wakashiba na kufanikiwa, watageukia miungu mingine na kuiabudu, wakinikataa mimi na kuvunja Agano langu.
21 Maovu na taabu nyingi zitakapokuja juu ya watu hawa, huu wimbo utashuhudia mbele yao (kwa maana hautasahaulika vinywani mwa uzao wao). Kwa maana najua mipango wanayotengeneza leo, hata kabla sijawaleta katika nchi niliyowaahidi.
Maafa na shida zitakapokuja juu yao, wimbo huu utashuhudia dhidi yao, kwa sababu hautasahauliwa na wazao wao. Ninajua lile wanaloandaa kufanya, hata kabla sijawaingiza katika nchi niliyowaahidi kwa kiapo.”
22 Kwa hiyo Musa aliandika huu wimbo siku hiyo hiyo na kuwafundisha watu wa Israeli.
Hivyo Mose akaandika wimbo huu siku ile na akawafundisha Waisraeli.
23 Yahwe alimpa Yoshua mwana wa Nuni amri na kusema, “Uwe hodari na mwenye ujasiri mwema; kwa maana utawaleta watu wa Israeli katika nchi niliyoapa kwao, nami nitakuwa pamoja nawe.”
Bwana akampa Yoshua mwana wa Nuni agizo hili: “Uwe hodari na shujaa, kwa kuwa utawaleta Waisraeli katika nchi niliyowaahidi kwa kiapo, nami mwenyewe nitakuwa pamoja nawe.”
24 Ikatokea kwamba Musa alipomaliza kuandika maneno ya sheria hii katika kitabu,
Baada ya Mose kumaliza kuandika kwenye kitabu maneno ya sheria hii kutoka mwanzo hadi mwisho,
25 aliwaamuru Walawi waliobeba sanduku la agano la Yahwe, na kusema,
akawapa Walawi wale waliolibeba Sanduku la Agano la Bwana agizo hili, akawaambia:
26 “Chukua kitabu hiki cha sheria na kiweke pembeni mwa sanduku la agano la Yahwe Mungu wenu, ili kiweze kuwa pale kama ushahidi dhidi yenu.
“Chukueni Kitabu hiki cha Sheria mkakiweke kando ya Sanduku la Agano la Bwana Mungu wenu. Hapo ndipo kitakapokaa kama shahidi dhidi yenu.
27 Maana nafahamu uasi wenu na shingo zenu ngumu; tazama, maadamu nipo hai pamoja nanyi hata leo, mmekuwa waasi dhidi ya Yahwe; itakuaje baada ya mimi kufa?
Kwa kuwa ninajua jinsi mlivyo waasi na mlivyo na shingo ngumu. Kama mmekuwa mkiasi dhidi ya Bwana nikiwa bado niko hai na nikiwa pamoja nanyi, mtaasi mara ngapi baada ya kufa kwangu!
28 Nikusanyieni wazee wote wa makabila yenu, na maafisa wenu, ili nizungumze maneno haya masikioni mwao na kuziita mbingu na nchi kushuhudia dhidi yao.
Kusanyeni mbele yangu wazee wote wa makabila yenu na maafisa wenu wote, ili nipate kusema maneno haya masikioni mwao na kuziita mbingu na nchi ili kushuhudia dhidi yao.
29 Kwa maana najua baada ya kifo changu mtajiharibu kabisa na kugeuka kuiacha njia niliyowaamuru; maafa yatawakumba katika siku zijazo. Haya yatatokea kwa sababu mtafanya yaliyo maovu machoni pa Yahwe, ili kumchokoza katika hasira kwa mikono ya kazi yenu.”
Kwa kuwa ninajua baada ya kifo changu hakika mtakuwa waovu kabisa na kugeuka kutoka njia niliyowaamuru ninyi. Katika siku zijazo, maafa yatawapata kwa sababu mtafanya maovu mbele ya macho ya Bwana, na kuchochea hasira yake kwa yale mikono yenu itakayokuwa imefanya.”
30 Musa alinena masikioni mwa kusanyiko lote la Israeli maneno yote ya wimbo huu hadi yalipokamilika.
Mose akayasoma maneno ya wimbo huu kutoka mwanzo hadi mwisho katika masikio ya kusanyiko lote la Israeli: