< Torati 31 >
1 Musa alikwenda na kuzungumza maneno haya kwa Israeli yote.
2 Alisema kwao, “Kwa sasa nina umri wa miaka mia moja na ishirini; Siwezi kutoka na kuingia tena; Yahwe ameniambia, “Hautavuka Yordani hii”
3 Yahwe Mungu wako, atakutangulia mbele yako; ataangamiza mataifa haya mbele yako, nawe utawanyanganya. Yoshua atakwenda kabla yako, kama Yahwe alivyonena.
4 Yahwe atawafanya kwao kama alivyofanya kwa Sihoni na kwa Ogu, wafalme wa Waamori, na kwa nchi yao, aliyoiangamiza.
5 Yahwe atakupatia ushindi juu yao utakapokutana nao vitani, nawe utafanya kwao yote ntakayokuamuru.
6 Uwe hodari na mwenye ujasiri mwema, usiogope, na usiwaogope; kwa maana Yahwe Mungu wako, ni yeye aendaye kabla yako; hatakuangusha wala kukuacha.”
7 Musa akamwita Yoshua na akamwambia machoni pa Israeli yote, “Uwe hodari na mwenye ujasiri mwema, kwa kuwa utaondoka na hawa watu katika nchi ambayo Yahwe ameapa kwa mababu zao kuwapatia; utafanya wairithi.
8 Yahwe, yeye ndiye atakwenda kabla yako; atakuwa pamoja nawe; hatakuangusha wala hatakutelekeza; usiogope, usivunjike moyo.”
9 Musa aliandika sheria hii na kuwapatia makuhani, wana wa Walawi, ambao walibeba sanduku la agano la Yahwe; pia aligawa nakala zake kwa wazee wote wa Israeli.
10 Musa aliwaamuru na kusema, “Katika kila mwisho wa miaka saba, kwa muda uliowekwa wa kudumu kwa ajili ya kufuta madeni, katika Sikukuu ya Vibanda,
11 ambapo Israeli yote imekuja kujitokeza mbele ya Yahwe Mungu wako katika mahali atakayochagua kuwa patakatifu pake, utasoma sheria hii mbele ya Israeli yote wakisikia.
12 Kusanya watu, wanaume, wanawake, na wadogo, na mgeni wako aliye miongoni mwa malango yako, ili waweze kusikia na kujifunza, na ili kwamba wamheshimu Yahwe Mungu wako na kushika maneno yote ya sheria hii.
13 Fanya hivi ili kwamba watoto wao, ambao hawajajua, waweze kusikia na kujifunza kumheshimu Yahwe Mungu wako, maadamu unaishi katika nchi ambayo utaenda juu ya Yordani kuimiliki.”
14 Yahwe alimwambia Musa, “Tazama, siku inakuja ambayo lazima utakakufa; muite Yoshua na mjidhihirishe katika hema la makutano, ili kwamba niweze kuwapatia amri.” Musa an Yoshua waliondoka na kujidhihirisha katika hema la makutano.
15 Yahwe alijifunua kwenye hema kwa nguzo ya wingu; nguzo ya wingu ilisimama juu ya mlango wa hema.
16 Yahwe alimwambia Musa, “Tazama, utalala na baba zako; watu hawa watainuka na kujifanya kama kahaba na kwenda kwa miungu ya ajabu ambayo imo miongoni mwao katika nchi wanapokwenda. Wataniacha na kuvunja agano langu ambalo nimefanya nao.
17 Basi, katika siku hiyo, hasira yangu itawaka dhidi yao nami nitawaacha. Nitaficha uso wangu kwao nao watamezwa. Maafa na taabu nyingi yatawakumba ili waseme katika siku hiyo, “Maafa haya hayajaja kwetu kwa sababu Mungu hayupo kati yetu?”
18 Hakika nitaficha uso wangu kwao katika siku hiyo kwa sababu ya uovu wote ambao watakuwa wametenda, kwa sababu wamegeukia miungu mingine.
19 Basi sasa andika wimbo huu kwa ajili yenu na wafundishe watu wa Israeli. Uweke vinywani mwao, ili kwamba wimbo huu uweze kuwa shahidi kwangu dhidi ya watu wa Israeli.
20 Kwa maana nitakapowaleta katika nchi ambayo niliapa kwa mababu zao, nchi inayotiririka kwa maziwa na asali, na watakapokula na kuridhika na kunenepa, ndipo watageukia miungu mingine nao watawatumikia na kunidharau na watavunja agano langu.
21 Maovu na taabu nyingi zitakapokuja juu ya watu hawa, huu wimbo utashuhudia mbele yao (kwa maana hautasahaulika vinywani mwa uzao wao). Kwa maana najua mipango wanayotengeneza leo, hata kabla sijawaleta katika nchi niliyowaahidi.
22 Kwa hiyo Musa aliandika huu wimbo siku hiyo hiyo na kuwafundisha watu wa Israeli.
23 Yahwe alimpa Yoshua mwana wa Nuni amri na kusema, “Uwe hodari na mwenye ujasiri mwema; kwa maana utawaleta watu wa Israeli katika nchi niliyoapa kwao, nami nitakuwa pamoja nawe.”
24 Ikatokea kwamba Musa alipomaliza kuandika maneno ya sheria hii katika kitabu,
25 aliwaamuru Walawi waliobeba sanduku la agano la Yahwe, na kusema,
26 “Chukua kitabu hiki cha sheria na kiweke pembeni mwa sanduku la agano la Yahwe Mungu wenu, ili kiweze kuwa pale kama ushahidi dhidi yenu.
27 Maana nafahamu uasi wenu na shingo zenu ngumu; tazama, maadamu nipo hai pamoja nanyi hata leo, mmekuwa waasi dhidi ya Yahwe; itakuaje baada ya mimi kufa?
28 Nikusanyieni wazee wote wa makabila yenu, na maafisa wenu, ili nizungumze maneno haya masikioni mwao na kuziita mbingu na nchi kushuhudia dhidi yao.
29 Kwa maana najua baada ya kifo changu mtajiharibu kabisa na kugeuka kuiacha njia niliyowaamuru; maafa yatawakumba katika siku zijazo. Haya yatatokea kwa sababu mtafanya yaliyo maovu machoni pa Yahwe, ili kumchokoza katika hasira kwa mikono ya kazi yenu.”
30 Musa alinena masikioni mwa kusanyiko lote la Israeli maneno yote ya wimbo huu hadi yalipokamilika.