< Danieli 4 >

1 Mfalme Nebukadneza aliituma amri hii kwa watu wote, mataifa, na lugha walioishi katika nchi: “Na amani yenu na iongezeke.
Mfalme Nebukadneza, Kwa kabila za watu, mataifa na watu wa kila lugha, wanaoishi katika ulimwengu wote: Mafanikio yawe kwenu sana!
2 Imeonekana vizuri kwangu kuwaambia juu ya ishara na maajabu ambayo Mungu Mkuu Aliye juu amenifanyia.
Ni furaha yangu kuwaambia kuhusu ishara za miujiza na maajabu ambayo Mungu Aliye Juu Sana amenifanyia.
3 Ni kwa namna gani Ishara zake ni kubwa, na ni kwa namna gani maajabu yake yana nguvu! Ufalme wake ni ufalme unaodumu milele, na utawala wake hudumu kizazi hadi kizazi.”
Ishara zake ni kuu aje, na maajabu yake yana nguvu aje! Ufalme wake ni ufalme wa milele; enzi yake hudumu kutoka kizazi hadi kizazi.
4 Mimi, Nebukadneza, nilikuwa ninaishi kwa furaha katika nyumba yangu, na nilikuwa nikifurahia mafanikio katika ikulu yangu.
Mimi, Nebukadneza, nilikuwa nyumbani katika jumba langu la kifalme, nikiwa ninaishi kwa raha na hali ya kufanikiwa.
5 Lakini ndoto niliyoiota ilifanya niogope. Nilipokuwa nimejilaza pale, taswira niliyoiona na maono katika akili yangu yalinitaabisha.
Niliota ndoto iliyoniogopesha. Nilipokuwa nimelala kitandani mwangu, njozi na maono yaliyopita mawazoni mwangu vilinitisha.
6 Basi nilitoa agizo la kuwaleta mbele yangu watu wote wa Babeli waliokuwa na hekima ili kwamba waweze kunitafsiria ndoto.
Hivyo nikaagiza kwamba watu wote wenye hekima wa Babeli waletwe mbele yangu kunifasiria ndoto yangu.
7 Kisha walikuja wachawi, wale ambao hudai kuzungumza na wafu, watu wenye hekima, na wasoma nyota. Niliwaambia juu ya ndoto, lakini hawakuweza kunitafsiria.
Walipokuja waganga, wasihiri, wanajimu na waaguzi, niliwaambia ndoto yangu, lakini hawakuweza kunifasiria.
8 Bali mwishoni Danieli aliingia ndani - yeye ambaye huitwa Belteshaza jina la mungu wangu, na ambaye ndani yake kuna roho ya miungu mitakatifu - na nilimwambia juu ya ndoto.
Mwishoni, Danieli alikuja mbele yangu nikamweleza hiyo ndoto. (Danieli anaitwa Belteshaza, kwa jina la mungu wangu, nayo roho ya miungu mitakatifu inakaa ndani yake.)
9 “Belteshaza, mkuu wa wachawi, ninajua kuwa roho ya miungu watakatifu iko ndani yako na ya kwamba hakuna siri iliyo ngumu kwako. Niambie kile nilichokiona katika ndoto yangu na nini maana yake.
Nilisema, “Belteshaza, mkuu wa waganga, ninajua kuwa roho ya miungu mitakatifu iko ndani yako, wala hakuna siri iliyo ngumu kwako. Hii ndiyo ndoto yangu, nifasirie.
10 Haya ndiyo niliyoyaona katika akili zangu nilipokuwa nimejilaza katika kitanda changu: Nilitazama, na kulikuwa na mti katikati ya dunia, na urefu wake ulikuwa ni mkubwa sana.
Haya ndiyo maono niliyoona nilipokuwa nimelala kitandani mwangu: Nilitazama, na mbele yangu ulisimama mti katikati ya nchi. Ulikuwa mrefu sana.
11 Mti ulikua na ukawa wenye nguvu. Na sehemu ya juu yake ilifika mbinguni, uliweza kuonekana kutoka miisho ya dunia yote.
Mti ule ulikua, ukawa mkubwa na wenye nguvu, nayo ncha yake ikagusa anga; ulionekana mpaka miisho ya dunia.
12 Majani yake yalikuwa mazuri, matunda yake yalikuwa ni mengi, na juu yake kulikuwa na chakula kwa ajili ya wote. Wanyama wa mwituni walipata kivuli chini yake, na ndege wa angani waliisha katika matawi yake. Viumbe vyote hai vililishwa katika mti huo.
Majani yake yalikuwa ya kupendeza, matunda yake yalikuwa mengi, na juu yake kulikuwa na chakula kwa ajili ya wote. Chini ya kivuli chake wanyama wa kondeni walipata hifadhi, na ndege wa angani waliishi katika matawi yake. Kila kiumbe kililishwa kutokana na mti huo.
13 Nilipokuwa nimelala kitandani kwangu, niliona katika akili zangu, mjumbe mtakatifu alishuka kutoka mbinguni.
“Katika maono niliyoyaona nikiwa nimelala kitandani mwangu, nilitazama, na mbele yangu alikuwepo mlinzi, aliye mtakatifu, akishuka kutoka mbinguni.
14 Alipiga kelele na kusema, 'Ukateni mti na yafyekeni matawi yake, yapukutisheni majani yake, na kuyasambaza matunda yake. Wanyama na wakimbie kutoka chini yake na ndege wapae mbali kutoka katika matawi yake.
Akaita kwa sauti kubwa: ‘Kateni mti huu, myafyeke matawi yake; yaondoeni majani yake na kuyatawanya matunda yake. Wanyama na wakimbie kutoka chini yake na ndege waondoke kutoka matawi yake.
15 Mkiache kisiki cha mizizi yake katika nchi, mkifunge na fungu la chuma na shaba, katikati ya mche mororo wa shambani. Na kilowanishwe na umande wa kutoka mbinguni. Kiacheni kiishi na wanyama kati ya mimea ya ardhini.
Lakini acheni kisiki chake na mizizi, kikiwa kimefungwa kwa chuma na shaba, kibaki ardhini, kwenye majani ya kondeni. “‘Mwacheni aloweshwe na umande wa mbinguni, naye aachwe aishi pamoja na wanyama miongoni mwa mimea ya dunia.
16 Akili yake na ibadilishwe kutoka akili ya kibinadamu, na apewe akili ya mnyama mpaka ipite miaka saba.
Akili yake na ibadilishwe kutoka ile ya mwanadamu na apewe akili ya mnyama, mpaka nyakati saba zipite juu yake.
17 Uamuzi huu ni kutokana na amri iliyotolewa na mjumbe. Ni uamuzi uliofanya na yeye aliye mtakatifu ili kwamba hao walio hai wajue kwamba Mungu aliye juu sana anatawala juu ya falme za watu na huwapa kwa kila mmoja apendaye kumweka juu yao, hata kwa watu wale wanyenyekevu sana.'
“‘Uamuzi huu umetangazwa na walinzi, hukumu imetangazwa na watakatifu, ili walio hai wajue kuwa Aliye Juu Sana ndiye anayetawala juu ya falme zote za wanadamu, naye humpa yeyote amtakaye na kumtawaza juu yake hata yeye aliye mnyonge sana miongoni mwa wanadamu.’
18 Mimi, Mfalme Nebukadneza nilipata ndoto hii. Sasa, wewe Belteshaza, niambie tafsiri yake, kwasababu hakuna mtu mwenye hekima katika ufalme wangu anayeweza kunitafsiria. Lakini wewe unaweza kufanya hivyo, kwa kuwa roho ya miungu watakatifu iko ndani yako.”
“Hii ndiyo ndoto niliyoipata mimi, Mfalme Nebukadneza. Sasa Belteshaza, niambie maana yake, kwa maana hakuna hata mmoja wa wenye hekima katika ufalme wangu anayeweza kunifasiria. Bali wewe waweza, kwa sababu roho ya miungu mitakatifu imo ndani yako.”
19 Ndipo Danieli aliyeitwa pia Belteshaza, alihuzunishwa kwa muda, na mawazo yake yalimshitua. Mfalme akasema, “Belteshaza, usifadhaishwe na ndoto au tafsiri yake.” Belteshaza akajibu, “Bwana wangu, ndoto hii na iwe kwa ajili ya watu wanaokuchukia, na tafsiri yake na iwe kwa ajili ya adui zako.
Ndipo Danieli (aliyeitwa pia Belteshaza) alipofadhaika sana kwa muda, nayo mawazo yake yakamtia hofu. Basi mfalme akasema, “Belteshaza, usiruhusu ndoto wala maana yake kukutia hofu.” Belteshaza akamjibu, “Bwana wangu, laiti ndoto hii ingehusu adui zako, na maana yake iwahusu watesi wako!
20 Mti ule uliouona - uliokua na ukawa na wenye nguvu, na ambao sehemu yake ya juu ilifika hata mbinguni, na ambao waweza kuonekana kutoka miisho ya dunia yote -
Mti uliouona, uliokua ukawa mkubwa na wenye nguvu, nayo ncha yake ikagusa anga na kuonekana duniani kote,
21 ambao majani yake ni mazuri, na matunda yake yalikuwa ni mengi, ili kwamba ndani yake kulikuwa na chakula cha wote, na chini yake wanyama wa mwituni walipata kivuli, na ndani yake ndege wa angani waliishi -
ukiwa na majani ya kupendeza na matunda mengi, ukitoa chakula kwa wote, na ukiwapa hifadhi wanyama wa kondeni na kuwa mahali pa viota katika matawi yake kwa ajili ya ndege wa angani.
22 huu mti ni wewe, mfalme, wewe uliyekua na kuwa na nguvu. Ukuu wako umeongezeka na kufika mbinguni, na mamlaka yako yamefika hata miisho ya dunia.
Ee mfalme, wewe ndiwe ule mti! Umekuwa mkubwa na mwenye nguvu, nao ukuu wako umekua mpaka kufika juu angani, nayo mamlaka yako yameenea mpaka miisho ya dunia.
23 Ewe mfalme, ulimwona mjumbe akishuka kutoka mbinguni na akisema, “Ukateni mti na uteketezeni, lakni kiacheni kisiki cha mizizi yake katika nchi, kifungeni kwa ukanda wa chuma na shaba, katikati ya mche mororo katika shamba. Na kilowanishwe na umande kutoka mbinguni. Kiache kiishi katika wanyama wa mwituni katika mashamba mpaka ipite miaka saba.'
“Ee mfalme, wewe ulimwona mlinzi, aliye mtakatifu, akishuka kutoka mbinguni na kusema, ‘Ukateni mti na kuuangamiza, lakini kiacheni kisiki kikiwa kimefungwa kwa chuma na kwa shaba, kwenye majani ya kondeni, wakati mizizi yake inabaki ardhini. Mwacheni aloweshwe na umande wa mbinguni, mwacheni aishi kama wanyama pori mpaka nyakati saba zipite juu yake.’
24 Mfalme, hii ni tafsiri yake. Ni agizo la Yeye Aliye Juu ambalo limekufikia, bwana wangu mfalme.
“Ee mfalme, hii ndiyo tafsiri, na hii ni amri ya Aliye Juu Sana aliyoitoa dhidi ya bwana wangu mfalme:
25 Utafukuzwa utoke miongoni mwa watu, na utaishi pamoja na wanyama wa mwituni huko mashambani. Utafanywa uwe unakula majani kama ng'ombe, na utalowanishwa na umande wa kutoka mbinguni, miaka saba itapita mpaka pale utakapokiri kwamba Mungu Aliye Juu anatawala juu ya falme zote za watu na ya kwamba yeye humpa falme hizo mtu yeyote amtakaye.
Wewe utafukuzwa mbali na wanadamu, nawe utaishi pamoja na wanyama pori; utakula manyasi kama ngʼombe, na kuloana kwa umande wa mbinguni. Nyakati saba zitapita juu yako, mpaka utakapokubali kuwa Yeye Aliye Juu Sana ndiye anayetawala juu ya falme za wanadamu, naye humtawaza yeyote amtakaye.
26 Kama ilivyoamriwa kwamba kukiacha kisiki cha mizizi ya mti, kwa njia hii ufalme wako utarudishiwa katika kipindi ambacho utajifunza kwamba mbingu inatawala.
Amri ya kuacha kisiki pamoja na mizizi yake inamaanisha kwamba ufalme wako utarejezwa kwako utakapokubali kwamba Mbingu ndizo zitawalazo.
27 Hivyo basi, mfalme, ushauri wangu na ukubalike kwako. Acha kutenda dhambi na utende haki. Geuka uache uovu wako wa kuonesha huruma kwa walionewa, na itakuwa kwamba mafanikio yako yataongezwa.”
Kwa hiyo, ee mfalme, uwe radhi kupokea shauri langu: Acha dhambi zako kwa kutenda yaliyo haki, ukaache uovu wako, na uwe na huruma kwa walioonewa. Hivyo itawezekana baada ya hayo, mafanikio yako yakaendelea.”
28 Vitu hivi vyote vilitokea kwa mfalme Nebukadneza.
Haya yote yalimpata Mfalme Nebukadneza.
29 Baada ya miezi wa kumi na miwili alipokuwa akitembea juu ya dari la ikulu ya kifalme katika Babeli,
Miezi kumi na miwili baadaye, mfalme alipokuwa akitembea juu ya paa la jumba la kifalme la Babeli,
30 na alisema, “Je hii si Babeli kuu, ambayo nimeijenga kwa ajili ya makao yangu ya kifalme, kwa ajili ya utukufu wa enzi yangu?”
alisema, “Je, huu si Babeli mji mkuu nilioujenga kama makao ya kifalme, kwa uwezo wangu mkubwa, na kwa ajili ya utukufu wa enzi yangu?”
31 Wakati maneno yakali katika midomo ya mfalme, sauti ilisikika kutoka mbinguni: “Mfalme Nebukadneza, imetangazwa kwako kwamba ufalme huu umeondolewa kutoka kwako.
Maneno hayo yalikuwa bado katika midomo yake wakati sauti ilipokuja kutoka mbinguni, ikisema, “Mfalme Nebukadneza, hiki ndicho kilichoamriwa kwa ajili yako: Mamlaka yako ya ufalme yameondolewa kutoka kwako.
32 Utafukuziwa mbali kutoka miongoni mwa watu, na makao yao yatakuwa pamoja na wanyama wa mwitu katika mashamba. Utafanywa kulamajani kama ng'ombe. Miaka saba itapita mpaka pale utakapokiri kwamba Mungu Aliye Juu anatawala juu ya falme za watu na humpa falme mtu yeyote amtakaye.”
Utafukuzwa mbali na wanadamu, ukaishi pamoja na wanyama pori, na utakula manyasi kama ngʼombe. Nyakati saba zitapita juu yako, mpaka utakapokubali kuwa Yeye Aliye Juu Sana ndiye anayetawala juu ya falme za wanadamu, naye humtawaza yeyote amtakaye.”
33 Agizo hili kinyume na Nebukadneza lilitekelezwa ghafla. Aliondolewa miongoni mwa watu. Alikula majani kama ng'ombe, na mwili wake ulilowa kwa umande wa kutoka mbinguni. Nywele zake zilirefuka kama manyoa ya tai, na makucha yake yalikuwa kama makucha ya ndege.
Papo hapo yale yaliyokuwa yamesemwa kuhusu Nebukadneza yakatimia. Alifukuzwa mbali na wanadamu, akala majani kama ngʼombe. Mwili wake uliloweshwa kwa umande wa mbinguni mpaka nywele zake zikakua kama manyoya ya tai na kucha zake kama makucha ya ndege.
34 Na katika mwisho wa siku, mimi, Nebukadneza niliinua macho yangu kuelekea mbinguni, utimamu wa akili nilirudishiwa. “Nilimsifu Mungu Aliye Juu sana, na nilimheshimu na kumtukuza yeye aishiye milele. Kwa kuwa utawala wake ni wa milele, na ufalme wake unadumu katoka katika vizazi vyote hadi vizazi vyote.
Mwisho wa huo wakati, mimi Nebukadneza, niliinua macho yangu kuelekea mbinguni, nazo fahamu zangu zikanirudia. Ndipo nikamsifu Yeye Aliye Juu Sana, nikamheshimu na kumhimidi yeye aishiye milele. Utawala wake ni utawala wa milele; ufalme wake hudumu kutoka kizazi na kizazi.
35 Wenyeji wote wa duniani huhesabiwa na yeye kuwa bure; hufanya lolote limpendezalo miongoni mwa jeshi la mbinguni na wakazi wa dunia. Hakuna hata mmoja awezaye kumzuia au kumpa changamoto. Hakuna hata mmoja awezaye kumwambia, “Mbona umefanya hivi?”
Mataifa yote ya dunia yanahesabiwa kuwa si kitu. Hufanya kama atakavyo kwa majeshi ya mbinguni, na kwa mataifa ya dunia. Hakuna anayeweza kuuzuia mkono wake au kumwambia, “Umefanya nini wewe?”
36 Kwa wakati ule ule utimamu wa akili zangu uliponirudia, utukufu wangu na fahari yangu ilinirudia kwa ajili ya utukufu wa ufalme wangu. Washauri wangu na watu wenye heshima walitafuta msaada wangu. Nilirudishwa kwenye kiti changu cha enzi, na nilipewa ukuu zaidi.
Wakati huo huo fahamu zangu ziliponirudia, nikarudishiwa heshima yangu na fahari yangu kwa ajili ya utukufu wa ufalme wangu. Washauri wangu na wakuu wangu walikuja kunitafuta, nami nikarudishwa kwenye kiti changu cha ufalme hata nikawa mkuu kuliko mwanzoni.
37 Sasa basi, mimi Nebukadneza, ninamsifu, ninamtukuza na kumheshimu mfalme wa mbinguni, kwa kuwa matendo yake yote ni ya haki, na njia zake ni za adili. Anaweza kuwashusha wale wanaotembea katika kiburi chao wenyewe.
Basi mimi, Nebukadneza, humhimidi, na humtukuza na kumsifu Mfalme wa mbinguni, kwa sababu kila kitu afanyacho ni haki, na njia zake zote ni adili. Nao waendao kwa kiburi anaweza kuwashusha.

< Danieli 4 >