< Wakolosai 3 >
1 Ikiwa tena Mungu amewafufua pamoja na Kristo, yatafuteni mambo ya juu ambako Kristo anakaa mkono wa kuume wa Mungu.
2 Fikirini kuhusu mambo ya juu, sio kuhusu mambo ya duniani.
3 Kwa kuwa mmekufa, na maisha yenu yamefichwa pamoja na Kristo katika Mungu.
4 Wakati Kristo atakapoonekana, ambaye ni maisha yenu, ndipo nanyi pia mtaonekana naye katika utukufu.
5 Kwa hiyo yafisheni mambo yaliyo katika nchi yaani, zinaa, uchafu, shauku mbaya, nia mbaya, na tamaa, ambayo ni ibada ya sanamu.
6 Ni kwa ajili ya mambo haya ghadhabu ya Mungu inakuja juu ya wana wasio tii.
7 Ni kwa ajili ya mambo haya ninyi pia mlitembea kwayo mlipoishi kati yao.
8 Lakini sasa ni lazima myaondoe mambo haya yote. Yaani, ghadhabu, hasira, nia mbaya, matusi, na maneno machafu yatokayo vinywani mwenu.
9 Msidanganyane ninyi kwa ninyi, kwa kuwa mmeuvua utu wenu wa kale na matendo yake.
10 Mmevaa utu mpya, ambao unafanywa upya katika maarifa kutokana mfano wa yule aliye muumba.
11 Katika maarifa haya, hakuna Myunani na Myahudi, kutahiriwa na kutokutahiriwa, msomi, asiye msomi, mtumwa, asiye mtumwa, lakini badala yake Kristo ni mambo yote katika yote.
12 Kama wateule wa Mungu, watakatifu na wapendwao, jivikeni utu wema, ukarimu, unyenyekevu, upole na uvumilivu.
13 Chukulianeni ninyi kwa ninyi. Hurumianeni kila mtu na mwenzake. Kama mtu analalamiko dhidi ya mwingine, amsamehe kwa jinsi ilele ambayo Bwana alivyo wasamehe ninyi.
14 Zaidi ya mambo haya yote, muwe na upendo, ambao ndio kigezo cha ukamilifu.
15 Amani ya Kristo na iwaongoze mioyoni mwenu. Ilikuwa ni kwa ajili ya amani hii kwamba mliitiwa katika mwili mmoja. Iweni na shukrani.
16 Na Neno la Kristo likae ndani yenu kwa utajiri. Kwa hekima yote, fundishaneni na kushauriana ninyi kwa ninyi kwa Zaburi, nyimbo, na nyimbo za rohoni. Imbeni kwa shukrani mioyo yenu kwa Mungu.
17 Na chochote mfanyacho, katika maneno au katika matendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu. Mpeni shukrani Mungu baba kupitia Yeye.
18 Wake, wanyenyekeeni waume zenu, kama ipendezavyo katika Bwana.
19 Nanyi waume, wapendeni wake zenu, na msiwe wakali dhidi yao.
20 Watoto, watiini wazazi wenu katika mambo yote, maana ndivyo impendezavyo Bwana.
21 Akina baba msiwachokoze watoto wenu, ili kwamba wasije wakakata tamaa.
22 Watumwa, watiini mabwana zenu katika mwili kwa mambo yote, sio kwa huduma ya macho kama watu wa kufurahisha tu, bali kwa moyo wa kweli. Mwogopeni Mungu.
23 Chochote mfanyacho, fanyeni kutoka nafsini mwenu kama kwa Bwana na si kama kwa wanadamu.
24 Mnajua ya kwamba mtapokea tuzo ya umilkaji kutoka kwa Bwana. Ni Kristo Bwana mnayemtumikia.
25 Kwa sababu yeyote atendaye yasiyo haki atapokea hukumu kwa matendo yasiyo haki aliyoyafanya, na hakuna upendeleo.