< Wakolosai 2 >
1 Kwa kuwa nataka mfahamu jinsi ambavyo nimekuwa na taabu nyingi kwa ajili yenu, kwa wote walioko Laodikia na kwa wote ambao hawajaona uso wangu katika mwili.
2 Nafanya kazi ili kwamba mioyo yao iweze kufarijiwa kwa kuletwa pamoja katika upendo na katika utajiri wote wa wingi wa uhakika kamili wa maarifa, katika kuijua siri ya kweli ya Mungu, ambaye ni Kristo.
3 Katika Yeye hazina zote za hekima na maarifa zimefichwa.
4 Nasema hivi ili kwamba mtu yeyote asije akawafanyia hila kwa hotuba yenye ushawishi.
5 Na ingawa sipo pamoja nanyi katika mwili, lakini nipo nanyi katika roho. Ninafurahi kuona utaratibu wenu mzuri na nguvu ya imani yenu katika Kristo.
6 Kama mlivyompokea Kristo Bwana, tembeeni katika yeye.
7 Mwimarishwe katika yeye, mjengwe katika yeye, mwimarishwe katika imani kama tu mlivyofundishwa, na kufungwa katika shukrani nyingi.
8 Angalieni ya kwamba mtu yeyote asiwanase kwa falsafa na maneno matupu ya udanganyifu kulingana na mapokeo ya wanadamu, kulingana na kanuni za kidunia, na sio kulingana na Kristo.
9 Kwa kuwa katika yeye ukamilifu wote wa Mungu unaishi katika mwili.
10 Nanyi mmejazwa katika yeye. Yeye ni kichwa cha kila uweza na mamlaka.
11 Katika yeye pia mlitahiriwa kwa tohara isiyofanywa na wanadamu katika kuondolewa mwili wa nyama, lakini ni katika tohara ya Kristo.
12 Mlizikwa pamoja naye katika ubatizo. Na kwa njia ya imani katika yeye mlifufuliwa kwa uweza wa Mungu, aliyemfufua kutoka kwa wafu.
13 Na mlipokuwa mmekufa katika makosa yenu na kutokutahiriwa kwa miili yenu, aliwafanya hai pamoja naye na kutusamehe makosa yetu yote.
14 Alifuta kumbukumbu ya madeni iliyoandikwa, na taratibu zilizokuwa kinyume nasi. Aliiondoa yote na kuigongomea msalabani.
15 Aliziondoa nguvu na mamlaka. Aliyaweka wazi na kuyafanya kuwa sherehe ya ushidi kwa njia ya msalaba wake.
16 Kwa hiyo, mtu yeyote asiwahukumu ninyi katika kula au katika kunywa, au kuhusu siku ya sikukuu au mwezi mpya, au siku za Sabato.
17 Hivi ni vivuli vya mambo yajayo, lakini kiini ni Kristo.
18 Mtu awaye yote asinyang'anywe tuzo yake kwa kutamani unyenyekevu na kwa kuabudu malaika. Mtu wa jinsi hiyo huingia katika mambo aliyoyaona na kushawishiwa na mawazo yake ya kimwili.
19 Yeye hakishikilii kichwa. Ni kutoka katika kichwa kwamba mwili wote kupitia viungo vyake na mifupa huungwa na kushikamanishwa kwa pamoja; na hukua kwa ukuaji utolewao na Mungu.
20 Ikiwa mlikufa pamoja na Kristo kwa tabia za dunia, mbona mnaishi kama mnawajibika kwa dunia:
21 “Msishike, wala kuonja, wala kugusa”?
22 Haya yote yameamuriwa kwa ajili ya uharibifu ujao na matumizi, kutokana na maelekezo na mafundisho ya wanadamu.
23 Sheria hizi zina hekima ya dini zilizotengenezwa kwa ubinafsi na unyenyekevu na mateso ya mwili. Lakini hazina thamani dhidi ya tamaa za mwili.