< Amosi 5 >
1 Sikilizeni hili neno ambalo nisemalo kama maombelezo juu yenu, nyumba ya Israeli.
2 Bikira wa Israeli ameanguka; hatoinuka tena; ametoroka kwenye nchi yake, hakuna mtu wa kumwinua.
3 Kwa kuwa hivi ndivyo Yahwe asemavyo: “Mji ambao umetoka nje kwa elfu watabaki mia, na walioenda nje mia watabaki kumi wa mali ya nyumba ya Israeli.”
4 Kwa kuwa hivi ndivyo Yahwe asemavyo kwa nyumba ya Israeli: “Nitafuteni na mtaishi!
5 Msimtafute Betheli; wala kuingia Gilgali; msisafiri kwenda Bersheba. Kwa kuwa Gilgali watakwenda utumwani hakika, na Betheli haitakuwa kitu.
6 Mtafuteni Yahwe mtaishi, au atawaka kama moto kwenye nyumba ya Yusufu. Utateketeza, na hakutakuwa na mtu hata mmoja kuuzima katika Betheli.
7 Wale watu wageuzao haki kuwa jambo chungu na kuiangusha haki chini!”
8 Mungu aliiumba Pleidezi na Orioni; amebadilisha giza kuwa asubuhu; hufanya siku kuwa giza na usiku na kuita maji ya bahari; yeye huyamwaga juu ya uso wa dunia. Yahwe ndilo jina lake!
9 Yeye huleta uharibifu wa ghafla juu ya waliohodari ili kwamba uharibifu uje juu ya ngome.
10 Wanamchukia kila awasahihishaye katika lango la mji, nao humchukia sana yeyote asemaye ukweli.
11 Kwa sababu mnamkanyaga chini maskini na kuchukua sehemu ya ngano kutoka kwake- ingawa mmejenga nyumba za mawe yaliyochongwa, hamtaishi kwenye nyumba hizo. Mmependezwa na mashamba ya mizabibu, lakini hamtakunywa mvinyo wake.
12 Kwa kuwa najua ni jinsi gani mlivyo na makosa mengi na jinsi dhambi zenu zilivyo kubwa- ninyi mnaowaonea wenye haki, chukueni rushwa, na kuwageuza wahitaji kwenye lango la mji.
13 Kwa hiyo kila mtu mwenye busara atanyamaza kimya kwenye wakati kama huo, kwa kuwa ni wakati wa uovu.
14 Tafuteni mazuri na sio mabaya, ili kwamba mpate kuishi. Hivyo Yahwe, Mungu wa majeshi, atakuwa na ninyi tayari, kama msemavyo yeye ndiye.
15 Chukieni uovu, imarisheni haki katika lango la mji. Huenda Yahwe, Mungu wa majeshi, atawafadhili mabaki ya Yusufu.
16 Kwa hiyo, hivi ndivyo Yahwe asemavyo, Mungu wa majeshi, Bwana, “Kutakuwa na maombolezo kwenye miraba yote, na watasema kwenye mitaa yote, 'Ole! Ole!' Watawaita wakulima kuomboleza na walio hodari wa kulia na kuomboleza.
17 Katika mashamba yote ya mizabibu kutakuwa na kilio, kwa kuwa nitapita katikati yako,” asema Yahwe.
18 Ole wenu ninyi mnaoitamani siku ya Yahwe! Kwa nini mnaitamani? Itakuwa giza na sio nuru,
19 kama wakati mtu anamkimbia simba na kukutana na dubu, au aliingia katika nyumba na kuweka mkono wake kwenye ukuta na kung'atwa na nyoka.
20 Je siku ya Yahwe itakuwa giza na sio nuru? Huzuni na sio furaha?
21 “Nachukia, nazidharau sikukuu zenu, naichukia mikutano yenu ya dini.
22 Hata kama mnanitolea sadaka ya kuteketeza na sadaka za unga, sintozipokea, wala kuzitazama kwenye sadaka za ushirika wa wanyama walionona.
23 Niondoleeni kelele za nyimbo zenu; sintosikiliza sauti za vinubi vyenu.
24 Badala yake, acheni haki itiririke kama maji, na haki kama mkondo utiririkao siku zote.
25 Je mmeniletea dhambihu na sadaka za kuteketeza jangwani kwa mda wa miaka arobaini?
26 Mtamwinua Sikuthi kama mfalme wenu, na Kiuni, nyota yenu ya miungu-ambayo mmeifanya kwa ajili yenu wenyewe.
27 Kwa hiyo nitawahamisha upande wa pili wa Damaskasi,” asema Yahwe, ambaye jina lake ni Mungu wa majeshi.