< Matendo 9 >
1 Lakini Sauli, aliendelea kusema vitisho hata vya kifo kwa wanafunzi wa Bwana, alikwenda kwa kuhani mkuu
2 na kumwomba barua kwa ajili ya masinagogi huko Dameski, ili kwamba akimpata mtu aliye katika Njia ile, awe mwanaume au mwanamke, awafunge na kuwaleta Yerusalemu.
3 Hata alipokuwa akisafiri, ilitokea kwamba alipokaribia Dameski, ghafla ikamwangaza kotekote nuru kutoka mbinguni,'
4 naye akaanguka chini na akasikia sauti ikimwambia,”Sauli, Sauli, mbona wanitesa mimi?”
5 Sauli akajibu, U nani wewe Bwana? Bwana akasema, “Mimi ndiye Yesu unayeniudhi;
6 Lakini inuka, ingia mjini, nawe utaambiwa yakupasayo kutenda
7 Wale watu waliosafiri pamoja na Sauli wakatulia kimya, wakisikiliza sauti, wasione mtu.
8 Sauli akainuka katika nchi na alipofungua macho yake, hakuweza kuona kitu, wakamshika mkono wakamleta mpaka Dameski.
9 Kwa siku tatu haoni, hali, wala hanywi.
10 Basi palikuwapo mwanafunzi Dameski jina lake Anania, Bwana alisema naye katika maono, “Anania.” Na akasema, “Tazama, nipo hapa, Bwana.
11 “Bwana akamwambia, “Inuka uenda zako katika mtaa uitwao Nyofu, na katika nyumba ya Yuda na ukaulize mtu kutoka Tarso aitwaye Sauli; maana angali anaomba;
12 na alimwona katika maono mtu jina lake Anania akiingia na kumwekea mikono juu yake ili kwamba apate kuona.
13 Lakini Anania akajibu, “Bwana, nimesikia habari za mtu huyu kwa watu wengi, kwa kiasi gani alivyowatendea mabaya watakatifu wa huko Yerusalemu;
14 Hapa ana mamlaka kutoka kwa kuhani mkuu kumkamata kila mmoja anayeliitia jina lako.
15 Lakini Bwana akamwambia, “Nenda, kwa maana yeye ni chombo teule kwangu, alichukue jina langu mbele ya Mataifa na wafalme na wana wa Israeli.
16 Maana nitawaonesha yalivyo mengi yatakayompasa kuteswa kwa ajili ya jina langu”.
17 Anania akaenda, akaingia mle nyumbani; Akamwekea mikono akasema, Ndugu Sauli, Bwana Yesu, aliyekutokea katika njia ulipokuwa unakuja, amenituma upate kuona tena na ujazwe Roho Mtakatifu.
18 Ghafla vikaanguka machoni pake vitu kama magamba, akapata kuona, akasimama, akabatizwa; akala chakula na kupata nguvu.
19 Akakaa pamoja na wanafunzi huko Dameski kwa siku nyingi.
20 Wakati huo huo akamtangaza Yesu katika masinagogi, akisema kwamba yeye ni Mwana wa Mungu.
21 Na wote waliosikia walishangaa na kusema, “Siyo mtu huyu aliyewaharibu wote walioita Jina hili huko Yerusalemu? Na hapa alikuja kwa kusudi la kuwafunga na kuwapeleka kwa makuhani.”
22 Lakini Sauli aliwezeshwa kuhubiri na kuwafanya Wayahudi waliokaa Dameski wachanganyikiwe na kuthibitisha ya kuwa huyu ndiye Kristo.
23 Baada ya siku nyingi, Wayahudi wakafanya shauri pamoja ili wamuue.
24 Lakini mpango wao ukajulikana na Sauli. Wakamvizia mlangoni mchana na usiku wapate kumuua.
25 Lakini wanafunzi wake wakamchukua usiku wakamshusha kupitia ukutani, wakamtelemsha chini katika kapu.
26 Na Sauli alipofika Yerusalemu, alijaribu kujiunga na wanafunzi lakini walikuwa wakimuogopa, wasisadiki kuwa yeye ni mwanafunzi.
27 Lakini Barnaba akamchukua na kumpeleka kwa mitume, Na akawaeleza jinsi Sauli alivyomuona Bwana njiani na Bwana alivyosema nae, na jinsi Sauli alivyohubiri kwa ujasiri kwa jina la Yesu huko Dameski.
28 Alikutana nao walipoingia na kutoka Yerusalemu. Akanena kwa ujasiri kwa jina la Bwana Yesu,
29 akihojiana na Wayahudi wa Kiyunani lakini wakijaribu mara kwa mara kumuua.
30 Wakati ndugu walipojua jambo hilo, wakamchukua mpaka Kaisaria, na wampeleke aende Tarso.
31 Basi kanisa lote katika Uyahudi, Galilaya na Samaria, lilikuwa na amani, na likajengwa, na kutembea katika hofu ya Bwana na faraja ya Roho Mtakatifu, kanisa likakua kwa kuongezeka idadi.
32 Kisha ilitokea Petro alipokuwa akizungukazunguka pande zote za mkoa, akawateremkia waumini waishio katika mji wa Lida.
33 Akamuona huko mtu mmoja jina lake Ainea, mtu huyo amekuwa kitandani miaka minane; maana alikuwa amepooza.
34 Petro akamwambia, “Ainea, Yesu Kristo akuponye; Amka na ujitandikia kitanda chako,” Mara akaamka.
35 Na watu wote waliokaa Lida na Sharoni walipomuona mtu huyo, walimgeukia Bwana.
36 Palikuwa na mwanafunzi Yafa aitwaye Tabitha, ambalo lilitafsiriwa kama “Dorcas” Huyu mwanamke alijaa kazi njema na matendo ya rehema aliyoyafanya kwa maskini.
37 Ilitokea katika siku hizo aliugua na akafa; walipomsafisha, walimpandisha chumba cha juu na kumlaza.
38 Kwa vile Lida ilikuwa karibu na Yafa, na wanafunzi walisikia kwamba Petro alikuwa huko, waliwatuma watu wawili kwake, wakimsihi, “Njoo kwetu bila kuchelewa”.
39 Petro akaamka na akaondoka pamoja nao. Alipofika, walimleta katika chumba cha juu. Na wajane wote walisimama karibu naye wakilia, wakimwonyesha koti na nguo ambazo Dorcas aliwashonea wakati akiwa pamoja nao.
40 Petro akawatoa wote nje ya chumba, akapiga magoti akaomba, kisha akaugekia mwili, akasema, “Tabitha, amka”. Akafungua macho yake na alipomwona Petro akakaa chini.
41 Kisha Petro akampa mkono wake akamwinua, na alipowaita waamini na wajane, akawakabidhi kwao akiwa hai
42 Jambo hili likajulikana Yafa yote, na watu wengi wakamwamini Bwana.
43 Ilitokea Petro akakaa siku nyingi Yafa pamoja na mtu aitwaye Simoni, mtengeneza ngozi.