< Matendo 4 >
1 Wakati Petro na Yohana walipokuwa wakizungumza na watu, makuhani na mlinzi wa hekalu na masadukayo waliwaendea.
2 Walikuwa wameudhika sana kwa sababu Petro na Yohana walikuwa wanawafundisha watu kuhusu Yesu na kutangaza juu ya kufufuka kwake kutoka kwa wafu.
3 Waliwakamata na kuwaweka gerezani hadi asubuhi iliyofuata, kwani tayari ilikuwa jioni.
4 Lakini watu wengi waliokuwa wamesikia ujumbe waliamini; na idadi ya wanaume waliokuwa wameamini walikadiliwa kuwa elfu tano.
5 Hata ilipofika asubuhi siku iliyofuata, kwamba wakuu wao, wazee na waandishi, kwa pamoja walikusanyika Yerusalemu.
6 Anasi kuhani mkuu alikuwepo, na Kayafa, na Yohana, na Iskanda, na wote waliokuwa ni ndugu wa kuhani mkuu.
7 Walipokuwa wamewaweka Petro na Yohana katikati yao, waliwauliza, “Kwa uwezo gani, au kwa jina gani mmefanya hili?”
8 Kisha, Petro, akiwa amejaa Roho Mtakatifu, akawaambia, “Ninyi wakuu wa watu, na wazee,
9 kama sisi siku ya leo tunahojiwa kuhusu tendo jema lililofanywa kwa mtu huyu mgonjwa - kwa namna gani mtu huyu alifanywa mzima?
10 Hebu lijulikane hilo kwenu na kwa watu wote katika Israel, kwamba kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, ambaye mlimsulibisha, ambaye Mungu alimfufua kutoka kwa wafu, ni kwa njia yake kwamba mtu huyu anasimama hapa mbele yenu akiwa mwenye afya.
11 Yesu Kristo ni jiwe ambalo ninyi wajenzi mlilidharau, lakini ambalo limefanywa kuwa jiwe kuu la pembeni.
12 Hakuna wokovu katika mtu mwingine awaye yote. Kwa maana hakuna jina jingine chini ya mbingu walilopewa watu, ambalo kwa hilo tunaweza kuokolewa.”
13 Sasa walipoona ujasiri wa Petro na Yohana, na wakagundua kwamba walikuwa ni watu wakawaida wasio na elimu, walishangaa, wakafahamu kwamba Petro na Yohana wamekuwa pamoja na Yesu.
14 Kwa sababu walimwona yule mtu aliyeponywa amesimama pamoja nao, hawakuwa na kitu cha kusema dhidi ya hili.
15 Lakini walipokuwa wamekwisha kuwaamuru mitume waondoke mbele ya mkutano wa baraza, walizungumza wao kwa wao.
16 Walisema, tutawafanyaje watu hawa? Ni kweli kwamba muujiza wa ajabu umefanyika kupitia wao unajulikana na kila mmoja anayeishi Yerusalemu; hatuwezi kulikataa hilo.
17 Lakini, ili kwamba jambo hili lisienee miongoni mwa watu, hebu tuwaonye wasinene tena kwa mtu yeyote kwa jina hili.
18 Waliwaita Petro na Yohana ndani na kuwaamuru kamwe wasinene wala kufundisha kwa jina la Yesu.
19 Lakini Petro na Yohana walijibu na kuwaambia, “Kama ni sahihi machoni pa Mungu kuwatii ninyi kuliko Mungu, hukumuni wenyewe.
20 Maana sisi hatuwezi kuacha kuyanena mambo ambayo tumeyaona na kuyasikia.”
21 Baada ya kuwaonya sana Petro na Yohana, waliwaacha waende. Hawakuweza kupata sababu yoyote ya kuwaadhibu, kwa sababu watu wote walikuwa wakimsifu Mungu kwa kile kilichokuwa kimetendeka.
22 Mtu aliyekuwa amepokea muujiza wa uponyaji alipata kuwa na umri zaidi ya miaka arobaini.
23 Baada ya kuwaacha huru, Petro na Yohana walikuja kwa watu wao na kuwataarifu yote ambayo makuhani wakuu na wazee walikuwa wamewaambia.
24 Walipoyasikia, walipaza sauti zao kwa pamoja kwa Mungu na kusema, “Bwana, wewe uliyeumba mbingu na dunia na bahari na kila kitu ndani yake,
25 wewe ambaye, kwa Roho Mtakatifu, kwa kinywa cha baba yetu Daudi, mtumishi wako, ulisema, “Kwanini watu wa mataifa wamefanya ghasia, na watu wametafakari mambo yasiyofaa?
26 Wafalme wa dunia wamejipanga pamoja, na watawala wamekusanyika kwa pamoja dhidi ya Bwana na dhidi ya masihi wake.”
27 Ni hakika, wote Herode na Pontio Pilato, pamoja na watu wa mataifa na watu wa Israeli, walikusanyika kwa pamoja katika mji huu dhidi ya mtumishi wako mtakatifu Yesu, ambaye ulimpaka mafuta.
28 Walikusanyika kwa pamoja kufanya yote ambayo mkono wako na mapenzi yako yaliyaamuru tangu awali kabla hayajatokea.
29 Sasa, Bwana, yaangalie matisho yao, na ukawajaalie watumishi wako kulinena neno lako kwa ujasiri wote. Ili
30 kwamba unaponyosha mkono wako kuponya, ishara na maajabu viweze kutokea kupitia jina la mtumishi wako mtakatifu Yesu.”
31 Walipomaliza kuomba, eneo ambalo walikusanyika kwa pamoja likatikiswa, na wote wakajazwa na Roho Mtakatifu, na walinena neno la Mungu kwa ujasili.
32 Idadi kubwa ya wale walioamini walikuwa na moyo mmoja na roho moja: na hakuna hata mmoja wao aliyesema kwamba chochote alichomiliki kilikuwa cha kwake mwenyewe; badala yake walikuwa na vitu vyote shirika.
33 Kwa nguvu kubwa mitume walikuwa wakiutangaza ushuhuda wao kuhusu ufufuo wa Bwana Yesu, na neema kubwa ilikuwa juu yao wote.
34 Hapakuwa na mtu yeyote miongoni mwao aliyepungukiwa na mahitaji, kwa sababu watu wote waliokuwa na hati za viwanja au nyumba, waliviuza na kuleta pesa ya vitu waliyokuwa wameuza
35 na kuviweka chini ya miguu ya mitume. Na mgawanyo ulifanywa kwa kila muumini, kulingana na kila mmoja alivyokuwa na hitaji.
36 Yusufu, mlawi, mtu kutoka Kipro, alipewa jina la Barnabasi na mitume (hiyo ikitafasiriwa, ni mwana wa faraja).
37 Akiwa na shamba, aliliuza na akaleta fedha, akaziweka chini ya miguu ya mitume.