< Matendo 25 >

1 Ndipo Festo alipoingia katika jimbo hilo na baada ya siku tatu alienda toka Kaisaria hadi Yerusalemu.
Siku tatu baada ya Festo kuwasili Kaisaria kuchukua wajibu wake mpya, alipanda kwenda Yerusalemu,
2 Kuhani mkuu na Wayahudi mashuhuri walileta shutuma dhidi ya Paulo kwa Festo, na walizungumza kwa nguvu kwa Festo.
ambako viongozi wa makuhani na viongozi wa Wayahudi walikuja mbele yake na kuleta mashtaka yao dhidi ya Paulo.
3 Na walimwomba Festo fadhili juu ya habari za Paulo apate kumwita Yerusalemu ili waweze kumwua njiani.
Wakamsihi sana Festo, kama upendeleo kwao, aamuru Paulo ahamishiwe Yerusalemu, kwa kuwa walikuwa wanaandaa kumvizia ili wamuue akiwa njiani.
4 Lakini Festo alijibu kwamba Paulo alikuwa mfungwa katika Kaisaria, na kwamba yeye mwenyewe atarudi huko haraka.
Festo akawajibu, “Paulo amezuiliwa huko Kaisaria, nami mwenyewe ninakwenda huko hivi karibuni.
5 Alisema “Kwa hiyo, wale ambao wanaweza, wanaweza kwenda huko na sisi. Kama kuna kitu kibaya kwa mtu huyu, mnapaswa kumshtaki.”
Baadhi ya viongozi wenu wafuatane nami na kutoa mashtaka dhidi ya mtu huyo huko, kama amekosa jambo lolote.”
6 Baada ya kukaa siku nane au kumi zaidi, akarudi Kaisaria. Na siku iliyofuata akakaa katika kiti cha hukumu na kuamuru Paulo aletwe kwake.
Baada ya Festo kukaa miongoni mwao kwa karibu siku nane au kumi, akashuka kwenda Kaisaria na siku iliyofuata akaitisha mahakama, akaketi penye kiti chake cha hukumu, akaamuru Paulo aletwe mbele yake.
7 Alipofika, Wayahudi kutoka Yerusalemu wakasimama karibu, Wakatoa mashtaka mengi mazito ambayo hawakuweza kuyathibitisha.
Paulo alipotokea, wale Wayahudi waliokuwa wameteremka toka Yerusalemu wakasimama wakiwa wamemzunguka, wakileta mashtaka mengi mazito dhidi yake ambayo hawakuweza kuyathibitisha.
8 Paulo alijitetea na kusema, 'Si dhidi ya jina la Wayahudi, si juu ya hekalu, na si juu ya Kaisari, nimefanya mabaya.'
Ndipo Paulo akajitetea, akasema, “Mimi sikufanya jambo lolote kinyume cha sheria ya Wayahudi au dhidi ya Hekalu au kinyume cha Kaisari.”
9 Lakini Festo alitaka kujipendekeza kwa Wayahudi, na hivyo akamjibu Paulo kwa kusema, 'Je, unataka kwenda Yerusalemu na kuhukumiwa na mimi kuhusu mambo haya huko?'
Festo, akitaka kuwapendeza Wayahudi, akamuuliza Paulo, “Je, ungependa kwenda Yerusalemu na kukabili mashtaka mbele yangu huko?”
10 Paulo alisema, 'ninasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Kaisari ambapo napaswa kuhukumiwa. Sijawakosea Wayahudi, kama wewe ujuavyo vema.
Paulo akasema, “Mimi sasa nimesimama mbele ya mahakama ya Kaisari, ambako ndiko ninakostahili kushtakiwa. Kama vile wewe mwenyewe ujuavyo vyema kabisa sijawatendea Wayahudi kosa lolote.
11 Ikiwa nimekosa na kama nimefanya kinachostahili kifo, sikatai kufa. Lakini kama shutuma zao si kitu, hakuna mtu anaweza kunikabidhi kwao. Ninamwomba Kaisari. '
Basi kama mimi nina hatia ya kutenda kosa lolote linalostahili kifo, sikatai kufa. Lakini kama mashtaka yaliyoletwa dhidi yangu na hawa Wayahudi si kweli, hakuna yeyote aliye na haki ya kunikabidhi mikononi mwao. Naomba rufaa kwa Kaisari!”
12 Baada ya Festo kuongea na baraza akajibu, “unamwomba Kaisari; utaenda kwa Kaisari.”
Baada ya Festo kufanya shauri pamoja na baraza lake, akatangaza, “Wewe umeomba rufaa kwa Kaisari, nako kwa Kaisari utakwenda!”
13 Baada ya siku kadhaa, mfalme Agripa na Bernike walifika Kaisaria kufanya ziara rasmi kwa Festo.
Baada ya siku kadhaa Mfalme Agripa na Bernike wakapanda kuja Kaisaria kumsalimu Festo.
14 Baada ya kukaa hapo kwa siku nyingi, Festo aliwasilisha kesi ya Paulo kwa mfalme; Akasema, 'Mtu mmoja aliachwa hapa na Feliki kama mfungwa.
Kwa kuwa walikuwa wakae huko Kaisaria kwa siku nyingi, Festo alijadili shauri la Paulo na mfalme, akisema, “Kuna mtu mmoja hapa ambaye Feliksi alimwacha gerezani.
15 Nilipokuwa Yerusalemu makuhani wakuu na wazee wa Wayahudi walileta mashtaka juu ya mtu huyu kwangu, nao waliuliza juu ya hukumu dhidi yake.
Nilipokuwa huko Yerusalemu, viongozi wa makuhani na wazee wa Wayahudi walinijulisha habari zake na wakaomba hukumu dhidi yake.
16 Kwa hili mimi niliwajibu kwamba si desturi ya Waroma kumtoa mtu kwa upendeleo badala yake, mtuhumiwa anapaswa kuwa na nafasi ya kuwakabili washitaki wake na kujitetea dhidi ya tuhuma hizo.
“Lakini mimi nikawaambia kwamba si desturi ya Kirumi kumtoa mtu yeyote auawe kabla mshtakiwa kuonana uso kwa uso na washtaki wake, naye awe amepewa nafasi ya kujitetea kuhusu mashtaka anayoshutumiwa.
17 Kwa hiyo, walipokuja pamoja hapa, sikuweza kusubiri, lakini siku iliyofuata niliketi katika kiti cha hukumu na kuamuru mtu huyo aletwe ndani.
Hivyo walipokutana hapa, sikukawia, kesho yake niliitisha baraza, nikaketi penye kiti changu cha hukumu, nikaagiza huyo mtu aletwe.
18 Wakati washitaki waliposimama na kumshtaki, nilifikiri kwamba hakuna mashtaka makubwa yaliyoletwa dhidi yake.
Washtaki wake waliposimama, hawakushtaki kwa uhalifu wowote niliokuwa ninatarajia.
19 Badala yake, walikuwa na mabishano fulani pamoja naye kuhusu dini yao na kuhusu Yesu ambaye alikuwa amekufa, lakini Paulo anadai kuwa yu hai.
Badala yake walikuwa na vipengele fulani vya kutokukubaliana naye kuhusu dini yao na juu ya mtu mmoja aitwaye Yesu, ambaye alikufa, lakini yeye Paulo alidai kwamba yu hai.
20 Nilikuwa nimefumbwa jinsi ya kuchunguza suala hili, na nikamwuliza kama angeenda Yerusalemu kuhukumiwa kuhusu mambo haya.
Kwa kuwa sikujua jinsi ya kupeleleza jambo hili, nilimuuliza kama angependa kwenda Yerusalemu na kuhojiwa huko kuhusu mashtaka haya.
21 Lakini Paulo alipoitwa awekwe chini ya ulinzi kwa ajili ya uamuzi wa Mfalme, niliamuru awekwe hata nitakapompeleka kwa Kaisari. '
Lakini Paulo alipoomba afadhiliwe ili rufaa yake isikilizwe na Mfalme Agusto, nilimwamuru alindwe mpaka nitakapoweza kumpeleka kwa Kaisari.”
22 Agripa alizungumza na Festo, “ningependa pia kumsikiliza mtu huyu.” “Festo, akasema, “kesho utamsikiliza.”
Ndipo Agripa akamwambia Festo, “Ningependa kumsikiliza mtu huyo mimi mwenyewe.” Yeye akajibu, “Kesho utamsikia.”
23 Hivyo kesho yake, Agripa na Bernike walifika na sherehe nyingi; walifika katika ukumbi na maafisa wa kijeshi, na watu mashuhuri wa mji. Na Festo alipotoa amri, Paulo aliletwa kwao.
Siku iliyofuata Agripa na Bernike walifika kwa fahari kubwa wakaingia katika ukumbi wa mahakama, pamoja na majemadari wa jeshi na watu mashuhuri wa mji. Ndipo kwa amri ya Festo, Paulo akaletwa ndani.
24 Festo akasema, “Mfalme Agripa, na watu wote ambao wapo hapa pamoja nasi, mnamwona mtu huyu; jumuiya yote ya Wayahudi huko Yerusalemu na hapa pia wametaka niwashauri, na wao wakapiga kelele kwangu kwamba asiishi.
Festo akasema, “Mfalme Agripa, nanyi nyote mlio hapa pamoja nasi, mnamwona mtu huyu! Jumuiya yote ya Kiyahudi wamenilalamikia kuhusu mtu huyu huko Yerusalemu na hapa Kaisaria, wakipiga kelele kwamba haimpasi kuendelea kuishi.
25 Naliona kwamba hakufanya lolote linalostahili kifo; lakini kwa sababu amemwita Mfalme, niliamua kumpeleka kwake.
Sikuona kwamba ametenda jambo lolote linalostahili kifo, ila kwa kuwa alikuwa ameomba rufaa yake kwa mfalme, niliamua kumpeleka Rumi.
26 Lakini sina kitu dhahiri cha kuandika kwa Mfalme. Kwa sababu hii, nimemleta kwako, hasa kwako wewe, Mfalme Agripa, ili nipate kuwa na kitu cha kuandika kuhusu kesi.
Lakini mimi sina kitu maalum cha kumwandikia Bwana Mtukufu kumhusu mtu huyu. Kwa hiyo nimemleta mbele yenu ninyi nyote, hasa mbele yako, Mfalme Agripa, ili kutokana na matokeo ya uchunguzi huu, niweze kupata kitu cha kuandika.
27 kwa kuwa naona haina maana kumpeleka mfungwa na bila kuonyesha mashitaka yanayomkabili.
Kwa kuwa naona hakuna sababu ya kumpeleka mfungwa bila kuainisha mashtaka dhidi yake.”

< Matendo 25 >