< Matendo 23 >

1 Paulo akawaangalia moja kwa moja watu wa baraza na kusema, “Ndugu zangu, nimeishi mbele za Mungu kwa dhamira nzuri hadi hivi leo.”
Paulo akawakazia macho wale wajumbe wa baraza, akasema, “Ndugu zangu, nimetimiza wajibu wangu kwa Mungu kwa dhamiri safi kabisa hadi leo.”
2 Kuhani mkuu Anania akawaamuru wale waliosimama karibu naye wampige kinywa chake.
Kwa ajili ya jambo hili kuhani mkuu Anania akaamuru wale waliokuwa karibu na Paulo wampige kofi kinywani.
3 Ndipo Paulo akamwambia, “Mungu atakupiga wewe, ukuta uliopakwa chokaa. Umekaa ukinihukumu kwa sheria, nawe unaamuru nipigwe kinyume cha sheria?”
Ndipo Paulo akamwambia, “Mungu atakupiga wewe, ewe ukuta uliopakwa chokaa! Wewe umeketi hapo ili kunihukumu kwa mujibu wa sheria, lakini wewe mwenyewe unakiuka sheria kwa kuamuru kwamba nipigwe kinyume cha sheria!”
4 Wale waliokuwa wamesimama karibu naye wakasema, “Hivi ndivyo unavyomtukana kuhani mkuu wa Mungu?”
Wale watu waliokuwa wamesimama karibu na Paulo wakamwambia, “Je, wewe wathubutu kumtukana kuhani mkuu wa Mungu?”
5 Paulo akasema, “ndugu zangu, mimi sikujua kwamba huyu ni kuhani mkuu. Kwa kuwa imeandikwa, hutazungumza vibaya juu ya mtawala wa watu wako.”
Paulo akajibu, “Ndugu zangu, sikujua kwamba yeye alikuwa kuhani mkuu. Kwa maana imeandikwa, ‘Usimnenee mabaya kiongozi wa watu wako.’”
6 Paulo alipoona ya kwamba upande mmoja wa baraza ni Masadukayo na wengine Mafarisayo, akapaza sauti na kusema, “ndugu zangu, mimi ni Mfarisayo, mwana wa Mfarisayo. Ni kwa sababu hii nategemea kwa ujasiri ufufuo wa wafu ninao hukumiwa nao.”
Paulo alipotambua ya kuwa baadhi yao walikuwa Masadukayo na wengine ni Mafarisayo, akapaza sauti kwenye baraza, “Ndugu zangu, mimi ni Farisayo, mwana Farisayo. Hapa nimeshtakiwa kuhusu tumaini langu katika ufufuo wa wafu.”
7 Alipoyasema haya, malumbano makubwa yakatokea baina ya Mafarisayo na Masadukayo, na mkutano ukagawanyika.
Aliposema haya, farakano likaanza kati ya Mafarisayo na Masadukayo na baraza lote likagawanyika.
8 Kwani Masadukayo husema hakuna ufufuo, malaika wala hakuna roho, ila Mafarisayo husema haya yote yapo.
(Kwa maana Masadukayo wanasema kwamba hakuna ufufuo, wala hakuna malaika au roho, lakini Mafarisayo wanaamini haya yote.)
9 Ghasia kubwa ikatokea na baadhi ya waandishi waliokuwa upande wa Mafarisayo wakasimama na kujadili, wakisema, “hatujaona chochote kibaya dhidi ya mtu huyu. Vipi kama roho au malaika ameongea na yeye?”
Kukawa na ghasia kubwa, nao baadhi ya walimu wa sheria ambao ni Mafarisayo, wakasimama wakapinga kwa nguvu wakisema, “Hatuoni kosa lolote la mtu huyu! Huenda ikawa roho au malaika amezungumza naye”
10 Wakati kulitokea hoja kubwa, mkuu wa majeshi aliogopa kwamba Paulo angeraruliwa vipande vipande na wao, hivyo akaamuru wanajeshi washuke chini na kumchukua kwa nguvu kutoka kwa wajumbe wa baraza, na kumleta katika ngome.
Ugomvi ukawa mkubwa kiasi kwamba yule jemadari akahofu kuwa wangemrarua Paulo vipande vipande, akaamuru vikosi vya askari vishuke na kumwondoa Paulo katikati yao kwa nguvu na kumleta ndani ya ngome ya jeshi.
11 Usiku uliofuata Bwana alisimama karibu naye na kusema, “Usiogope, kwa kuwa umenishuhudia katika Yerusalemu, hivyo utatoa ushahidi pia katika Roma.”
Usiku uliofuata, Bwana akasimama karibu naye akamwambia, “Jipe moyo! Kama vile ulivyonishuhudia hapa Yerusalemu, hivyo imekupasa kunishuhudia huko Rumi pia.”
12 Kulipokucha, baadhi ya Wayahudi walifanya agano na kuita laana juu yao wenyewe: walisema ya kwamba hawatakula wala kunywa chochote mpaka watakapomuua Paulo.
Kulipopambazuka Wayahudi wakafanya shauri pamoja na kujifunga kwa kiapo kwamba hawatakula wala kunywa mpaka wawe wamemuua Paulo.
13 Kulikuwa na watu zaidi ya arobaini ambao walifanya njama hii.
Waliofanya mpango huo walikuwa zaidi ya watu arobaini.
14 wakaenda kwa wakuu wa makuhani na wazee na kusema, “Tumejiweka wenyewe kwenye laana kuu, tusile chochote hadi tutakapomwua Paulo.
Wakawaendea viongozi wa makuhani na wazee na kusema, “Tumejifunga pamoja kwa kiapo kwamba hatutakula wala kunywa mpaka tuwe tumemuua Paulo.
15 Hivyo sasa, baraza limwambie jemadari mkuu amlete kwenu, kana kwamba mnaamua kesi yake kwa usahihi. Kwetu sisi tuko tayari kumwua kabla hajaja hapa.”
Hivyo basi, wewe pamoja na baraza, inawapasa mkamjulishe jemadari ili amteremshe Paulo kwenu, mjifanye kama mnataka kufanya uchunguzi wa kina zaidi wa shauri lake. Nasi tuko tayari kumuua kabla hajafika hapa.”
16 Lakini mtoto wa dada yake na Paulo akasikia kwamba kulikuwa na njama, akaenda akaingia ndani ya ngome na kumwambia Paulo.
Lakini mtoto wa dada yake Paulo aliposikia juu ya shauri hilo baya, alikwenda kule kwenye ngome ya askari na kumweleza Paulo.
17 Paulo akamwita akida mmoja akasema, “Mchukue kijana huyu kwa jemadari; maana ana neno la kumwambia.”
Ndipo Paulo akamwita mmoja wa viongozi wa askari, akamwambia, “Mpeleke huyu kijana kwa jemadari, analo jambo la kumweleza.”
18 Basi akida akamchukua yule kijana akampeleka kwa jemedari mkuu akamwambia, “Paulo yule mfungwa aliniita akataka nikuletee kijana huyu kwako. Ana neno la kukuambia.”
Hivyo yule kiongozi wa askari akampeleka yule kijana kwa jemadari, akamwambia, “Paulo yule mfungwa aliniita na kuniomba nimlete huyu kijana kwako, kwa sababu ana neno la kukueleza.”
19 Yule jemadari mkuu akamshika kwa mkono akajitenga naye kando, na akamwuliza, “Ni kitu gani unachotaka kuniambia?”
Yule jemadari akamshika yule kijana mkono, akampeleka kando na kumuuliza, “Unataka kuniambia nini?”
20 Kijana yule akasema, “Wayahudi wamepatana kukuomba umlete Paulo kesho kwenye baraza kana kwamba wanataka kupata habari zake kwa usahili zaidi.
Yule kijana akasema, “Wayahudi wamekubaliana wakuombe umpeleke Paulo kwenye baraza lao kesho kwa kisingizio kwamba wanataka kufanya uchunguzi wa kina wa shauri lake.
21 Basi wewe usikubali kwa maana watu zaidi ya arobaini wanamvizia. Wamejifunga kwa laana, wasile wala wasinywe hata watakapomwua. Hata sasa wako tayari, wakisubiria kibali toka kwako.”
Lakini usishawishiwe nao kwa maana zaidi ya watu arobaini wanamvizia. Wamejifunga kwa kiapo kwamba hawatakula wala kunywa mpaka wawe wamemuua Paulo. Sasa wako tayari, wanangoja idhini yako kwa ajili ya ombi lao.”
22 Basi yule jemadari mkuu akamwacha kijana aende zake, baada ya kumwagiza “usimwambie mtu yeyote ya kwamba umeniarifu haya.”
Yule jemadari akamruhusu yule kijana aende na akamwonya, akisema, “Usimwambie mtu yeyote kwamba umenieleza habari hizi.”
23 Akawaita maakida wawili akasema watayarisheni askari mia mbili kwenda Kaisaria na askari wapanda farasi sabini, na wenye mikuki mia mbili, mtaondoka zamu ya tatu ya usiku.
Kisha yule jemadari akawaita viongozi wake wawili wa askari akawaambia, “Jiandaeni kuondoka saa tatu usiku huu kuelekea Kaisaria pamoja na askari 200, wapanda farasi sabini na watu 200 wenye mikuki.
24 Akawaambia kuweka wanyama tayari ambaye Paulo atamtumia na kumchukua salama kwa Feliki Gavana.
Pia tayarisheni na farasi watakaotumiwa na Paulo, mkampeleke salama kwa mtawala Feliksi.”
25 Akaandika barua kwa namna hii,
Kisha akaandika barua kwa Feliksi kama ifuatavyo:
26 Klaudio Lisia kwa Liwali mtukufu Feliki, salamu.
Klaudio Lisia, Kwa Mtawala, Mtukufu Feliksi: Salamu.
27 Mtu huyu alikamatwa na wayahudi wakawa karibu kumwua, ndipo nikaenda pamoja na kikosi cha askari nikamwokoa, nilipopata habari ya kuwa yeye ni raia wa kirumi.
Mtu huyu alikamatwa na Wayahudi wakakaribia kumuua, lakini nikaja na vikosi vyangu vya askari nikamwokoa, kwa kuwa nilipata habari kwamba yeye ni raiya wa Rumi.
28 Nilitaka kujua kwa nini wamemshtaki, hivyo nikampeleka kwenye baraza.
Nilitaka kujua kwa nini walikuwa wanamshutumu, hivyo nikamleta mbele ya baraza lao.
29 Nikaona kwamba alikuwa ameshitakiwa kwa ajili ya maswali ya sheria yao, wala hakushitakiwa neno lolote la kustahili kuuawa wala kufungwa.
Ndipo nikaona kuwa alikuwa anashutumiwa kwa mambo yanayohusu sheria yao, lakini hakuwa ameshtakiwa kwa jambo lolote linalostahili kifo au kifungo.
30 Kisha ikajulikana kwangu kwamba kuna njama dhidi yake, hivyo kwa haraka nikamtuma kwako, na kuwaagiza wanaomshitaki pia walete mashitaka dhidi yake mbele yako. Wakaagana.”
Nilipoarifiwa kuwa kulikuwa na shauri baya dhidi ya mtu huyu, nilimtuma kwako mara moja. Niliwaagiza washtaki wake pia waeleze mashtaka yao dhidi yake mbele yako.
31 Basi wale askari wakatii amri: wakamchukua Paulo wakampeleka hata Antipatri usiku.
Hivyo askari, kwa kufuata maelekezo waliyopewa, wakamchukua Paulo wakati wa usiku na kumleta mpaka Antipatri.
32 Siku iliyofuata, maaskari wengi wakawaacha wale wapanda farasi waende pamoja naye, nao wakarudi zao ngomeni.
Kesho yake wakawaacha wale wapanda farasi waendelee na safari wakiwa na Paulo, wao wakarudi kwenye ngome ya askari.
33 Na wapanda farasi walipofika Kaisaria, na kumpa liwali ile barua, wakamweka Paulo mbele yake.
Askari walipofika Kaisaria, walimpa mtawala ile barua, na kumkabidhi Paulo kwake.
34 Naye liwali alipoisoma barua, alimuuliza Paulo alitokea jimbo gani; alipojua ya kwamba ni mtu wa Kilikia,
Mtawala alipokwisha kuisoma ile barua alimuuliza Paulo alikuwa mtu wa jimbo gani. Alipojua kuwa anatoka Kilikia,
35 akasema, “Nitakusikia wewe watakapo kuja wale waliokushitaki,” akaamuru awekwe katika ikulu ya Herode.
alisema, “Nitasikiliza shauri lako washtaki wako watakapofika hapa.” Kisha akaamuru Paulo awekwe chini ya ulinzi kwenye jumba la kifalme la Herode.

< Matendo 23 >