< Matendo 17 >
1 Na walipopita katika miji ya Amfipoli na Apolonia, walikuja mpaka mji wa Thesalonike ambao kulikuwa na sinagogi la Wayahudi.
2 Kama ilivyo kawaida ya Paulo, alienda kwao, na kwa muda wa siku tatu za Sabato alijadiliana nao juu ya maandiko.
3 Alikuwa akiwafungulia maandiko na kuwaeleza kuwa, ilimpasa Kristo ateseke na kisha kufufuka tena kutoka kwa wafu. Aliwaambia, “Huyu Yesu ninayewaambia habari zake ndiye Kristo”
4 Baadhi ya Wayahudi walishawishika na kuungana na Paulo na Sila, pamoja na Wagiriki wachamungu, akinamama wengi waongofu na kundi kubwa la watu.
5 Lakini baadhi ya Wayahudi wasioamini, waliojawa na wivu, walienda sokoni na kuwachukuwa baadhi ya watu waovu, wakakusanya umati wa watu pamoja, na kusababisha ghasia mjini, kisha wakaivamia nyumba ya Jason, wakitaka kuwakamata Paulo na Sila ilikuwaleta mbele za watu.
6 Lakini walipowakosa, walimkamata Yasoni na baadhi ya ndugu wengine na kuwapeleka mbele ya maofisa wa mji, wakipiga kelele, “Hawa wanaume walioupindua ulimwengu wamefika mpaka huku pia,
7 Wanaume hawa waliokaribishwa na Yasoni wanaihalifu sheria ya Kaisari, wanasema kuna mfalme mwingine anayeitwa Yesu”
8 Umati na maofisa wa mji waliposikia mambo hayo, waliingiwa na wasiwasi.
9 Baada ya kuwa wamekwisha kuchukua fedha ya thamani ya ulinzi kutoka kwa Yason na wengine, waliwaachia waende.
10 Usiku ule ndugu walimtuma Paulo na Sila Beroya. Na walipofika kule walikwenda katika sinagogi la Wayahudi.
11 Watu wale walikuwa wenye werevu mkubwa kuliko wale watu wa Thesalonike, kwa sababu walikuwa na utayari wa kulipokea neno kwa akili zao, na kuchunguza maandiko kila siku ili kuona kama maneno yaliyonenwa ndivyo yalivyo.
12 Kwa hiyo wengi wao waliamini, wakiwemo wanawake wenye ushawishi mkubwa wa Kigiriki na wanaume wengi.
13 Lakini Wayahudi wa Thesalonike walipogundua kwamba Paulo anatangaza neno la Mungu huko Beroya, walienda huko na kuchochea na kisha kuanzisha ghasia kwa watu.
14 Kwa haraka, ndugu wakampeleka Paulo kwa njia ya ziwa, lakini Sila na Timotheo wakabaki pale.
15 Wale ndugu waliompeleka Paulo walienda naye hadi Athene, walipomwacha Paulo huko, walipokea maagizo kutoka kwake kuwa, Sila na Timotheo waje kwake kwa haraka iwezeanavyo.
16 Na wakati akiwasubiri huko Athene, roho yake ilikasirishwa ndani yake kwa jinsi alivyouona mji ulivyojaa sanamu nyingi.
17 Hivyo akajadiliana katika sinagogi na wayahudi wale waliomcha Mungu na kwa wale wote aliokutana nao kila siku sokoni.
18 Lakini baathi ya Wanafalsafa wa Waepikureo na Wastoiko wakamkabili. Na wengine wakasema, “Ni nini anachokisema huyu mwongeaji mchanga? Wengine wakasema, “inaonekana anahubiri habari ya mungu mgeni,” kwasababu anahubiri habari ya Yesu na ufufuo.
19 Wakamchukua Paulo na kumleta Areopago, wakisema, “Twaweza kujua haya mafundisho mapya unayoyaongea?
20 Kwasababu unaleta mambo mapya katika masikio yetu. Kwahivyo tunataka kujua haya mambo yana maana gani?”
21 (Na watu wote wa Athene pamoja na wageni waliopo kwao, hutumia muda wao aidha katika kuongea na kusikiliza juu ya jambo jipya.)
22 Kwa hiyo Paulo akasimama katikati ya watu wa Areopago na kusema, “Enyi watu wa Athene, naona kuwa ninyi ni watu wa dini kwa kila namna,
23 Kwani katika kupita kwangu na kuangalia vitu vyenu vya kuabudu, nimeona maneno yalioandikwa kwenye moja ya madhabahu yenu, ikisema “KWA MUNGU ASIYEJULIKANA”. Hivyo basi, huyo mnayemwabudu pasipokujua, ndiye ninayewajulisha ninyi.
24 Mungu aliyeumba dunia na kila kitu kilichoko ndani, kwa kuwa ni Bwana wa mbingu na nchi, hawezi kukaa katika mahekalu yaliyotengenezwa na mikono.
25 Na pia hatumikiwi na mikono ya wanadamu kana kwamba anahitaji kitu kwao, kwani yeye mwenyewe huwapa watu uzima na pumzi na vitu vingine vyote.
26 Kupitia mtu mmoja, alifanya mataifa yote ya watu waishio juu ya uso wa dunia, na akawawekea nyakati na mipaka katika maeneo wanaoishi.
27 Kwa hiyo, wanatakiwa kumtafuta Mungu, na yamkini wamfikie na kumpata, na kwa uhakika hayupo mbali na kila mmoja wetu.
28 Kwake tunaishi, tunatembea na kuwa na uzima wetu, kama vile mtunzi wenu mmoja wa shairi aliposema 'tu wazaliwa wake.'
29 Kwa hiyo, ikiwa sisi ni wazaliwa wa Mungu, hatupaswi kufikiri kuwa uungu ni kama dhahabu, au shaba, au mawe, sanamu iliyochongwa kwa ustadi na mawazo ya watu.
30 Kwa hiyo, Mungu alinyamazia nyakati zile za ujinga, lakini sasa anaamuru watu wote kila mahali wapate kutubu.
31 Hii ni kwa sababu ameweka siku atakayo ihukumu dunia kwa haki kwa mtu ambaye alimchagua. Mungu alitoa uhakika wa mtu huyu kwa kila mtu pale alipomfufua katoka kwa wafu.
32 Na watu wa Athene waliposikia habari ya kufufuliwa kwa wafu, baadhi yao wakamdhihaki Paulo, ila wengine wakasema “Tutakusikiliza tena kwa habari ya jambo hili”
33 Baada ya hapo, Paulo akawaacha.
34 Lakini baadhi ya watu waliungana naye wakaamini, akiwemo Dionisio Mwareopago, na Mwanamke anaitwa Damari na wengine pamoja nao.