< Matendo 1 >
1 Kitabu cha zamani nilikiandika, Theofilo, nikisema yote Yesu aliyoanza kufanya na kufundisha,
Katika kitabu changu cha kwanza nilikuandikia, mpendwa Theofilo, kuhusu mambo yote Yesu aliyofanya na kufundisha tangu mwanzo,
2 mpaka siku ambayo Yeye alipokelewa juu. Hii ilikuwa baada ya kutoa amri kupitia Roho Mtakatifu kwa mitume aliokuwa amewachagua.
hadi siku ile alipochukuliwa kwenda mbinguni, baada ya kuwapa maagizo kupitia kwa Roho Mtakatifu wale mitume aliowachagua.
3 Baada ya mateso yake, Yeye alionekana kwao akiwa hai pia na vithibitisho vingi vikishuhudia. Kwa siku arobaini alijidhihirisha kwao, na alizungumza kuhusu ufalme wa Mungu.
Baada ya mateso yake, alijionyesha kwao na kuwathibitishia kwa njia nyingi kwamba yeye yu hai. Katika muda wa siku arobaini baada ya kufufuka kwake aliwatokea na kunena kuhusu Ufalme wa Mungu.
4 Alipokuwa akikutana pamoja nao, aliwaamuru wasiondoke Yerusalemu, lakini wasubiri kwa ajili ya ahadi ya Baba, ambayo, alisema, “Mlisikia kutoka kwangu
Wakati mmoja alipokuwa pamoja nao, aliwapa amri hii, “Msitoke Yerusalemu, bali ingojeni ahadi ya Baba, ambayo mmenisikia nikisema habari zake.
5 kwamba Yohana alibatiza kabisa kwa maji, lakini mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu katika siku hizi chache.”
Yohana aliwabatiza kwa maji, lakini baada ya siku chache mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu.”
6 Na walipokuwa wamekutanika pamoja walimuuliza, “Bwana, hivi huu ndio muda utakaowarudishia Israeli ufalme?”
Mitume walipokuwa wamekusanyika pamoja, wakamuuliza Yesu, “Bwana, je, huu ndio wakati wa kuwarudishia Israeli ufalme?”
7 Yeye akawaambia, “Siyo sawa kwenu kujua wakati au majira ambayo Baba amekusudia kwa mamlaka yake mwenyewe.”
Yesu akawaambia, “Si juu yenu kujua nyakati na majira ambayo Baba ameyaweka katika mamlaka yake mwenyewe.
8 Lakini mtapokea nguvu, wakati Roho Mtakatifu atakapokuja juu yenu, na ninyi mtakuwa mashahidi wangu kote katika Yerusalemu na Uyahudi yote na Samaria mpaka mwisho wa nchi.”
Lakini mtapokea nguvu akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu, nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, Uyahudi kote na Samaria, hadi miisho ya dunia.”
9 Bwana Yesu alipokwisha yasema haya, wakiwa wanatazama juu, Yeye aliinuliwa juu, na wingu likamfunika wasimwone kwa macho yao.
Baada ya kusema mambo haya, walipokuwa wanatazama, akachukuliwa juu mbinguni mbele ya macho yao na wingu likampokea wasimwone tena.
10 Wakati wanatazama mbinguni kwa makini akienda, ghafla, watu wawili walisimama katikati yao wamevaa mavazi meupe.
Walipokuwa bado wakikaza macho yao kuelekea juu alipokuwa akienda zake Mbinguni, tazama ghafula, wanaume wawili waliovaa mavazi meupe wakasimama karibu nao,
11 Walisema, “Enyi watu wa Galilaya, kwa nini mnasimama hapa mkitazama mbinguni?” Huyu Yesu aliyepaa juu mbinguni atarudi kwa namna ile ile kama mlivyomuona akienda mbinguni.
wakasema, “Enyi watu wa Galilaya, mbona mnasimama mkitazama juu angani? Huyu Yesu aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda Mbinguni, atarudi tena jinsi iyo hiyo mlivyomwona akienda zake Mbinguni.”
12 Ndipo wakarudi Yerusalemu kutoka kwenye mlima wa mizeituni, ambao uko karibu na Yerusalemu, mwendo wa siku ya Sabato.
Ndipo waliporudi Yerusalemu kutoka Mlima wa Mizeituni, uliokuwa karibu na Yerusalemu, umbali wa mwendo wa Sabato kutoka mjini.
13 Walipofika walikwenda ghorofani walikokuwa wakikaa. Nao ni Petro, Yohana, Yakobo, Andrea, Filipo, Thomaso, Batholomayo, Mathayo, Yakobo Mwana wa Alfayo, Simoni Zelote na Yuda Mwana wa Yakobo.
Walipowasili mjini Yerusalemu, walikwenda ghorofani kwenye chumba walichokuwa wakiishi. Wale waliokuwepo walikuwa: Petro, Yohana, Yakobo, Andrea, Filipo, Tomaso, Bartholomayo, Mathayo, Yakobo mwana wa Alfayo, Simoni Zelote na Yuda mwana wa Yakobo.
14 Wote waliungana kama mtu mmoja, kwa juhudi walikuwa wakiendelea katika maombi. Pamoja na hao walikuwepo wanawake, Mariamu Mama yake Yesu, na kaka zake.
Hawa wote waliungana pamoja katika maombi. Pamoja nao walikuwepo wanawake kadha, na Maria mama yake Yesu, pamoja na ndugu zake Yesu.
15 Katika siku zile Petro alisimama katikati ya ndugu, kama watu 120, akasema,
Katika siku hizo Petro akasimama katikati ya waumini (jumla yao wote walikuwa watu wapatao 120), akasema,
16 Ndugu, ilikuwa lazima kwamba maandiko yatimizwe, ambapo zamani Roho Mtakatifu alisema kwa kinywa cha Daudi kuhusiana na Yuda, ambaye aliwaelekeza wale waliomkamata Yesu.
“Ndugu zangu, ilibidi Andiko litimie ambalo Roho Mtakatifu alitabiri kupitia kwa Daudi kumhusu Yuda aliyewaongoza wale waliomkamata Yesu.
17 Kwa kuwa yeye alikuwa mmoja wetu na alipokea fungu lake la faida katika hii huduma.”
Yuda alikuwa mmoja wetu, kwa maana na yeye alichaguliwa ashiriki katika huduma hii.”
18 (Sasa mtu huyu alinunua eneo kwa kile alichokipokea kwa uovu wake na hapo alianguka akitanguliza kichwa, mwili ukapasuka na matumbo yake yote yakawa wazi yakamwagika.
(Basi Yuda alinunua shamba kwa zile fedha za uovu alizopata; akiwa huko shambani akaanguka, akapasuka na matumbo yote yakatoka nje.
19 Wote walioishi Yerusalemu walisikia kuhusu hili, hivyo eneo hilo wakaliita kwa lugha yao “Akeldama” hilo ni “shamba la damu.”)
Kila mtu Yerusalemu akasikia habari hizi, kwa hiyo wakapaita mahali hapo kwa lugha yao, Akeldama, yaani Shamba la Damu).
20 “Kwenye kitabu cha Zaburi imeandikwa, 'Ngoja eneo lake liwe hame na isiruhusiwe hata mmoja kuishi pale;' na, 'Ruhusu mtu mwingine achukue nafasi yake ya uongozi.'
“Kama vile ilivyoandikwa katika kitabu cha Zaburi, “‘Mahali pake na pawe ukiwa, wala asiwepo yeyote atakayeishi humo,’ na, “‘Mtu mwingine aichukue nafasi yake ya uongozi.’
21 Hiyo ni muhimu, kwa hiyo, mmoja wa wanaume ambao waliambatana nasi wakati Bwana Yesu alipotoka na kuingia kati yetu,
Kwa hiyo inatubidi tumchague mtu mwingine miongoni mwa wale ambao wamekuwa pamoja nasi wakati wote Bwana Yesu alipoingia na kutoka katikati yenu,
22 kuanzia kwenye ubatizo wa Yohana mpaka siku ile alipotwaliwa juu, lazima awe shahidi wa ufufuo pamoja nasi.
kuanzia ubatizo wa Yohana mpaka siku aliyochukuliwa kutoka kwetu kwenda Mbinguni. Kwa kuwa mmoja wao inabidi awe shahidi pamoja nasi wa ufufuo wake.”
23 “Wakaweka mbele wanaume wawili, Yusufu aitwaye Barnaba, ambaye pia aliitwa Yusto na Mathia.
Wakapendekeza majina ya watu wawili: Yosefu, aitwaye Barsaba (ambaye pia alijulikana kama Yusto) na Mathiya.
24 Wao waliomba wakisema, “Wewe, Bwana, ujuaye mioyo ya watu wote, hivyo weka wazi yupi kati ya wawili hawa ambaye umemchagua
Kisha wakaomba, wakasema, “Bwana, wewe waujua moyo wa kila mtu. Tuonyeshe ni yupi kati ya hawa wawili uliyemchagua
25 kuchukua nafasi katika huduma na utume, ambapo Yuda alitenda uovu na kwenda mahali pake.”
ili achukue nafasi ya huduma ya utume ambayo Yuda aliiacha ili aende mahali pake mwenyewe.”
26 Wakapiga kura kwa ajili yao, na kura ikamwangukia Mathia ambaye alihesabiwa pamoja na wale mitume kumi na moja.
Kisha wakawapigia kura, nayo kura ikamwangukia Mathiya, naye akaongezwa kwenye wale mitume kumi na mmoja.