< 2 Timotheo 4 >
1 Ninakupa agizo hili lenye uzito mbele za Mungu na Kristo Yesu, atakaye wahukumu walio hai na wafu, na kwa sababu ya kufunuliwa kwake na Ufalme wake:
2 Hubiri Neno. Uwe tayari kwa wakati ufaao na usiofaa. Waambie watu dhambi zao, kemea, himiza, kwa uvumilivu wote na mafundisho.
3 Kwa maana wakati utakuja ambao watu hawatachukuliana na mafundisho ya kweli. Badala yake, watajitafutia walimu wa kufundisha kulingana na tamaa zao. kwa njia hii masikio yao yatakuwa yametekenywa.
4 Wataacha kusikiliza mafundisho ya kweli, na kugeukia hadithi.
5 Lakini wewe uwe mwaminifu katika mambo yote, vumilia magumu, fanya kazi ya mwinjilisti; timiza huduma yako.
6 Kwa maana mimi tayari nimekwisha kumiminwa. Muda wa kuondoka kwangu umewadia.
7 Nimeshindana katika haki, Mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda.
8 Taji ya haki imewekwa kwa ajili yangu, ambayo Bwana, anayehukumu kwa haki, atanipa siku ile. Na siyo kwangu tu bali pia kwa wote wanaongojea kwa shauku kuonekana kwake.
9 Jitahidi kuja kwagu haraka.
10 Kwa kuwa Dema ameniacha. Anaupenda ulimwengu wa sasa na amekwenda Thesalonike, Kreseni alikwenda Galatia, na Tito alikwenda Dalmatia. (aiōn )
11 Luka tu ndiye yuko pamoja nami. Umchukue Marko uje naye kwani yeye ni muhimu kwangu katika huduma.
12 Nimemtuma Tikiko Efeso.
13 Lile joho ambalo nililiacha Troa kwa Karpo, utakapokuja lilete, pamoja na vile vitabu hasa vile vya ngozi.
14 Alekizanda mfua chuma alinitendea maovu mengi. Bwana atamlipa kulingana na matendo yake.
15 Nawe pia jihadhari naye, kwani aliyapinga sana maneno yetu.
16 Katika utetezi wangu wa kwanza, hakuna mtu yeyote aliyesimama pamoja nami, badala yake, kila mmoja aliniacha. Mungu asiwahesabie hatia.
17 Lakini Bwana alisimama pamoja nami, akanitia nguvu ili kwamba kupitia kwangu, neno linenwe kwa ukamilifu na mataifa wapate kusikia. Niliokolewa katika kinywa cha Simba.
18 Bwana ataniepusha na matendo yote maovu na kuniokoa kwa ajili ya ufalme wake wa mbinguni. Utukufu uwe kwake milele na milele. Amen (aiōn )
19 Msalimie Priska, Akila na nyumba ya Onesiforo.
20 Erasto alibaki huko Korintho, lakini Trifimo nilimuacha Mileto akiwa mgonjwa.
21 Fanya hima uje kabla ya kipindi cha baridi. Eubulo anakusalimu, pia Pude, Lino, Claudia na ndugu wote.
22 Mungu awe pamoja na roho yako, Neema iwe nawe.