< 2 Timotheo 2 >
1 Kwa hiyo, wewe mwanangu, utiwe nguvu katika neema iliyondani ya Kristo Yesu.
2 Na mambo uliyoyasikia kwangu miongoni mwa mashahidi wengi, uyakabidhi kwa watu waaminifu ambao wataweza kuwafundisha wengine pia.
3 Shiriki mateso pamoja nami, kama askari mwema wa Kristo Yesu.
4 Hakuna askari atumikae wakati huo huo akijihusisha na shughuli za kawaida za maisha haya, ili kwamba ampendeze ofisa wake mkuu.
5 Pia kama mtu akishindana kama mwanariadha, hatapewa taji asiposhindana kwa kufuata kanuni.
6 Ni Muhimu kwamba mkulima mwenye bidii awe wa kwanza kupokea mgao wa mazao yake.
7 Tafakari kuhusu nisemacho, kwa maana Bwana atakupa uelewa katika mambo yote.
8 Mkumbuke Yesu Kristo, kutoka uzao wa Daudi, ambaye alifufuliwa kutoka kwa wafu. Hii ni kulingana na ujumbe wangu wa Injili,
9 ambao kwa sababu ya huo ninateswa hata kufungwa minyororo kama mhalifu. Lakini neno la Mungu halifungwi kwa minyororo.
10 Kwa hiyo, navumilia mambo yote kwa ajili ya wale ambao Mungu amekwishawachagua, ili kwamba nao pia waupate wokovu ulio katika Kristo Yesu pamoja na utukufu wa milele. (aiōnios )
11 Usemi huu ni wakuaminika: “Ikiwa tumekufa pamoja naye, tutaishi pamoja naye pia,
12 kama tukivumilia, tutatawala pamoja naye pia, kama tukimkana yeye, naye pia atatukana sisi.
13 kama hatutakuwa waaminifu, yeye atabaki kuwa mwaminifu, maana hawezi kujikana mwenyewe.”
14 Endelea kuwakumbusha juu ya mambo haya. Waonye mbele za Mungu waache kubishana kuhusu maneno. Kwa sababu hakuna manufaa katika jambo hili. Kutokana na hili kuna uharibifu kwa wale wanaosikiliza.
15 Fanya bidii kujionesha kuwa umekubalika kwa Mungu kama mtenda kazi asiye na sababu ya kulaumiwa. Litumie neno la kweli kwa usahihi.
16 Jiepushe na majadiliano ya kidunia, ambayo huongoza kwa zaidi na zaidi ya uasi.
17 Majadiliano yao yatasambaa kama donda ndugu. Miongoni mwao ni Himenayo na Fileto.
18 Hawa ni watu walioukosa ukweli. Wanasema ya kuwa ufufuo tayari umishatokea. Wanapindua imani ya baadhi ya watu.
19 Hata hivyo, msingi imara wa Mungu unasimama, wenye uandishi huu, “Bwana anawajua walio wake, na kila alitajaye jina la Bwana ni lazima ajitenge na udhalimu.”
20 Kwenye nyumba ya kitajiri, siyo kwamba vimo vyombo vya dhahabu na shaba tu. Pia kuna vyombo vya miti na udongo. Baadhi ya hivi ni kwa ajili ya matumizi ya heshima na baadhi yake ni kwa matumizi yasiyo ya heshima.
21 Ikiwa mtu atajitakasa mwenyewe kutoka kwenye matumizi yasiyo ya heshima, yeye ni chombo chenye kuheshimika. Ametengwa maalumu, mwenye manufaa kwa Bwana, na ameandaliwa kwa kila kazi njema.
22 Zikimbie tamaa za ujanani. Ukifuata haki, imani, upendo na amani pamoja na wale wamwitao Bwana kwa moyo safi.
23 Lakini ukatae upumbavu na maswali ya kipuuzi. Kwani unajua ya kuwa huzaa ugomvi.
24 Mtumishi wa Bwana hapaswi kugombana, badala yake inampasa kuwa mpole kwa watu wote, awezaye kufundisha, na mvumilivu.
25 Ni lazima awaelimishe kwa upole wale wampingao. Yamkini Mungu aweze kuwapatia toba kwa kuifahamu kweli.
26 Waweze kupata ufahamu tena na kuepuka mtego wa Shetani, baada ya kuwa wametekwa na yeye kwa ajili ya mapenzi yake.