< 2 Wathesalonike 3 >
1 Na sasa, ndugu, tuombeeni, kwamba neno la Bwana liweze kuenea na kutukuzwa, kama ilivyo pia kwenu.
2 Ombeni kwamba tuweze kuokolewa kutoka katika uovu na watu waasi, kwa kuwa si wote wana imani.
3 Lakini Bwana ni mwaminifu, ambaye atawaimarisha ninyi na kuwalinda kutoka kwa yule mwovu.
4 Tunaujasiri katika Bwana kwa ajili yenu, kwamba mnatenda na mtaendelea kutenda mambo ambayo tunawaagiza.
5 Bwana aweze kuongoza mioyo yenu katika upendo na katika uvumilivu wa Kristo.
6 Sasa tunawaagiza, ndugu, katika jina la Bwana Yesu Kristo, kwamba mwepuke kila ndugu ambaye anaishi maisha ya uvivu na siyo kwa kutokana na desturi ambazo mlipokea kutoka kwetu.
7 Kwa kuwa ninyi wenyewe mnajua ni sawa kwenu kutuiga sisi. Hatukuishi miongoni mwenu kama wale ambao hawakuwa na nidhamu.
8 Na hatukula chakula cha mtu yeyote bila kukilipia. Badala yake, tulifanya kazi usiku na mchana kwa kazi ngumu na kwa shida, ili tusiweze kuwa mzigo kwa yeyote katika ninyi.
9 Tulifanya hivi si kwa sababu hatuna mamlaka. Badala yake, tulifanya hivi ili tuwe mfano kwenu, ili kwamba mweze kutuiga sisi.
10 Wakati tulipokuwa pamoja nanyi tuliwaagiza, “Ikiwa mmoja wenu hataki kufanya kazi, na asile.”
11 Kwa kuwa tunasikia kwamba baadhi wanaenenda kwa uvivu miongoni mwenu. Hawafanyi kazi lakini badala yake ni watu wasio na utaratibu.
12 Sasa hao nao tunaagiza na kuwaasa katika Bwana Yesu Kristo, kwamba lazima wafanye kazi kwa utulivu na kula chakula chao wenyewe.
13 Lakini ninyi, ndugu, msizimie roho katika kufanya yaliyo sahihi.
14 Ikiwa mtu yeyote hataki kutii neno letu katika waraka huu, mwe makini naye na msiwe na ushirika pamoja naye, ili kwamba aweze kuaibika.
15 Msimchukulie kama adui, lakini mwonyeni kama ndugu.
16 Bwana wa amani mwenyewe awape amani wakati wowote katika njia zote. Bwana awe nanyi nyote.
17 Hii ni salam yangu, Paulo, kwa mkono wangu mwenyewe, ambayo ni alama katika kila waraka. Hivi ndivyo niandikavyo.
18 Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iweze kuwa nanyi nyote.