< 2 Wathesalonike 3 >

1 Na sasa, ndugu, tuombeeni, kwamba neno la Bwana liweze kuenea na kutukuzwa, kama ilivyo pia kwenu.
Hatimaye, ndugu, tuombeeni ili Neno la Bwana lipate kuenea kwa haraka na kuheshimiwa kila mahali, kama vile ilivyokuwa kwenu.
2 Ombeni kwamba tuweze kuokolewa kutoka katika uovu na watu waasi, kwa kuwa si wote wana imani.
Ombeni pia ili tupate kuokolewa kutokana na watu waovu na wabaya, kwa maana si wote wanaoamini.
3 Lakini Bwana ni mwaminifu, ambaye atawaimarisha ninyi na kuwalinda kutoka kwa yule mwovu.
Lakini Bwana ni mwaminifu, naye atawaimarisha ninyi na kuwalinda kutokana na yule mwovu.
4 Tunaujasiri katika Bwana kwa ajili yenu, kwamba mnatenda na mtaendelea kutenda mambo ambayo tunawaagiza.
Nasi tuna tumaini katika Bwana ya kuwa mnafanya na mtaendelea kufanya yale tuliyowaagiza.
5 Bwana aweze kuongoza mioyo yenu katika upendo na katika uvumilivu wa Kristo.
Bwana aiongoze mioyo yenu katika upendo wa Mungu na katika saburi ya Kristo.
6 Sasa tunawaagiza, ndugu, katika jina la Bwana Yesu Kristo, kwamba mwepuke kila ndugu ambaye anaishi maisha ya uvivu na siyo kwa kutokana na desturi ambazo mlipokea kutoka kwetu.
Ndugu, tunawaagiza katika Jina la Bwana Yesu Kristo, jitengeni na kila ndugu ambaye ni mvivu na ambaye haishi kufuatana na maagizo tuliyowapa.
7 Kwa kuwa ninyi wenyewe mnajua ni sawa kwenu kutuiga sisi. Hatukuishi miongoni mwenu kama wale ambao hawakuwa na nidhamu.
Maana ninyi wenyewe mnajua jinsi iwapasavyo kufuata mfano wetu. Sisi hatukuwa wavivu tulipokuwa pamoja nanyi,
8 Na hatukula chakula cha mtu yeyote bila kukilipia. Badala yake, tulifanya kazi usiku na mchana kwa kazi ngumu na kwa shida, ili tusiweze kuwa mzigo kwa yeyote katika ninyi.
wala hatukula chakula cha mtu yeyote pasipo kukilipia. Badala yake tulifanya kazi kwa bidii usiku na mchana, ili tusimlemee mtu yeyote miongoni mwenu.
9 Tulifanya hivi si kwa sababu hatuna mamlaka. Badala yake, tulifanya hivi ili tuwe mfano kwenu, ili kwamba mweze kutuiga sisi.
Tulifanya hivi, si kwa sababu hatukuwa na haki ya kupata msaada kama huo, bali ndio sisi wenyewe tuwe kielelezo.
10 Wakati tulipokuwa pamoja nanyi tuliwaagiza, “Ikiwa mmoja wenu hataki kufanya kazi, na asile.”
Kwa maana hata tulipokuwa pamoja nanyi, tuliwapa amri kwamba: “Mtu yeyote asiyetaka kufanya kazi, hata kula asile.”
11 Kwa kuwa tunasikia kwamba baadhi wanaenenda kwa uvivu miongoni mwenu. Hawafanyi kazi lakini badala yake ni watu wasio na utaratibu.
Kwa kuwa tunasikia kwamba baadhi ya watu miongoni mwenu ni wavivu. Hawafanyi kazi bali hujishughulisha na mambo ya wengine.
12 Sasa hao nao tunaagiza na kuwaasa katika Bwana Yesu Kristo, kwamba lazima wafanye kazi kwa utulivu na kula chakula chao wenyewe.
Basi watu kama hao tunawaagiza na kuwahimiza katika Bwana Yesu Kristo, kwamba wafanye kazi kwa utulivu kwa ajili ya chakula chao wenyewe.
13 Lakini ninyi, ndugu, msizimie roho katika kufanya yaliyo sahihi.
Kwa upande wenu, ndugu, ninyi kamwe msichoke katika kutenda mema.
14 Ikiwa mtu yeyote hataki kutii neno letu katika waraka huu, mwe makini naye na msiwe na ushirika pamoja naye, ili kwamba aweze kuaibika.
Ikiwa mtu yeyote hayatii maagizo yetu yaliyoko katika barua hii, mwangalieni sana mtu huyo. Msishirikiane naye, ili apate kuona aibu.
15 Msimchukulie kama adui, lakini mwonyeni kama ndugu.
Lakini msimhesabu kuwa adui, bali mwonyeni kama ndugu.
16 Bwana wa amani mwenyewe awape amani wakati wowote katika njia zote. Bwana awe nanyi nyote.
Basi, Bwana wa amani mwenyewe awapeni amani nyakati zote na kwa kila njia. Bwana awe nanyi nyote.
17 Hii ni salam yangu, Paulo, kwa mkono wangu mwenyewe, ambayo ni alama katika kila waraka. Hivi ndivyo niandikavyo.
Mimi, Paulo, ninaandika salamu hizi kwa mkono wangu mwenyewe. Hii ndio alama ya utambulisho katika barua zangu zote. Hivi ndivyo niandikavyo.
18 Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iweze kuwa nanyi nyote.
Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe nanyi nyote. Amen.

< 2 Wathesalonike 3 >