< 2 Wathesalonike 1 >

1 Paulo, Silwano, na Timotheo, kwa kanisa la Wathesalonike katika Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo.
Paulo, Silvano na Timotheo: Kwa kanisa la Wathesalonike mlio katika Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo:
2 Neema na iwe kwenu na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo.
Neema na amani itokayo kwa Mungu Baba na Bwana Yesu Kristo iwe nanyi.
3 Imetupasa sisi kumshukuru Mungu siku zote kwa ajili yenu, ndugu. Maana hivi ndivyo itupasavyo, kwa kuwa imani yenu inakua sana, na upendo wenu kwa kila mtu uongezeke mwingi.
Ndugu, imetubidi kumshukuru Mungu kwa ajili yenu siku zote, kama ulivyo wajibu wetu, kwa sababu imani yenu inakua zaidi na zaidi na upendo wa kila mmoja wenu alio nao kwa mwenzake unazidi kuongezeka.
4 Hivyo sisi wenyewe tunaongea kwa fahari juu yenu katika makanisa ya Mungu. Tunazungumza habari ya saburi yenu na imani mliyo nayo katika mateso yote. Tunaongea kwa habari ya mateso mnayostahimili.
Ndiyo sababu miongoni mwa makanisa ya Mungu, tunajivuna kuhusu saburi yenu na imani mliyo nayo katika mateso yote na dhiki mnazostahimili.
5 Hii ndiyo ishara ya hukumu ya haki ya Mungu. Matokeo ya haya ni kuwa ninyi mhesabiwe kuwa mwastahili kuuingia ufalme wa Mungu ambao kwa ajili yake mnateswa.
Haya yote ni uthibitisho kwamba hukumu ya Mungu ni ya haki, na kwa sababu hiyo ninyi mtahesabiwa kwamba mnastahili kuwa wa Ufalme wa Mungu, mnaoteswa kwa ajili wake.
6 Kwa kuwa ni haki kwa Mungu kuwalipa mateso wale wawatesao ninyi,
Mungu ni mwenye haki: yeye atawalipa mateso wale wawatesao ninyi
7 na kuwapa raha ninyi mteswao pamoja nasi. Atafanya hivi wakati wa kufunuliwa kwake Bwana Yesu kutoka mbinguni pamoja na malaika wa uweza wake.
na kuwapa ninyi mnaoteseka raha pamoja na sisi, wakati Bwana Yesu atakapodhihirishwa kutoka mbinguni katika mwali wa moto pamoja na malaika wake wenye nguvu.
8 Katika mwali wa moto atawalipiza kisasi wao wasiomjua Mungu na wao wasioitii injili ya Bwana wetu Yesu.
Atawaadhibu wale wasiomjua Mungu na ambao hawakuitii Injili ya Bwana wetu Yesu.
9 Watateseka kwa maangamizi ya milele wakiwa wametengwa na uwepo wa Bwana na utukufu wa nguvu zake. (aiōnios g166)
Wataadhibiwa kwa uangamivu wa milele na kutengwa na uso wa Bwana na utukufu wa uweza wake, (aiōnios g166)
10 Atafanya wakati atakapokuja ili kutukuzwa na watu wake na kustaajabishwa na wote walioamini. Kwa sababu ushuhuda wetu kwenu ulisadikiwa kwenu.
siku hiyo atakapokuja kutukuzwa katika watakatifu wake na kustaajabiwa miongoni mwa wote walioamini. Ninyi pia mtakuwa miongoni mwa hawa kwa sababu mliamini ushuhuda wetu kwenu.
11 Kwa sababu hii twawaombea ninyi siku zote. Twaomba kwamba Mungu wetu awahesabu kuwa mlistahili kuitwa. Twaomba kwamba apate kutimiza kila haja ya wema na kila kazi ya imani kwa nguvu.
Kwa sababu hii, tunawaombea ninyi bila kukoma, ili Mungu apate kuwahesabu kuwa mnastahili wito wake na kwamba kwa uwezo wake apate kutimiza kila kusudi lenu jema na kila tendo linaloongozwa na imani yenu.
12 Tunaomba mambo haya ili mpate kulitukuza jina la Bwana Yesu. Tunaomba kwamba mpate kutukuzwa naye, kwa sababu ya neema ya Mungu na ya Bwana Yesu Kristo.
Tunaomba hivi ili Jina la Bwana wetu Yesu lipate kutukuzwa ndani yenu, nanyi ndani yake, kulingana na neema ya Mungu wetu na Bwana Yesu Kristo.

< 2 Wathesalonike 1 >