< 2 Samweli 9 >
1 Daudi akasema, “Je kuna yeyote aliyesalia wa familia ya Sauli ambaye naweza kumwonyesha kwa fadhiri kwa ajili ya Yonathani?
2 Alikuwepo mtumishi katika familia ya Sauli jina lake Siba, akaitwa kwa Daudi. Mfalme akamuuliza, “Je wewe ndiye Siba?” Akajibu, “Mimi ni mtumishi wako, ndiye.”
3 Hivyo mfalme akasema, “Je hakuna aliyesalia wa familia ya Sauli ambaye naweza kumuonesha wema wa Mungu?” Siba akamjibu mfalme, “Yonathani ana mwana, ambaye ni mlemavu wa miguu.
4 Mfalme akamwambia, “Yupo wapi?” Siba akamjibu mfalme, “Tazama, yupo katika nyumba ya Makiri mwana wa Amieli huko Lo Debari.
5 Ndipo mfalme Daudi akatuma watu na kumtoa katika nyumba ya Makiri mwana wa Amieli huko Lo Debari.
6 Hivyo Mefiboshethi mwana wa Yonathani mwana wa Sauli, akaja kwa Daudi naye akainama uso wake hadi katika sakafu kwa kumheshimu Daudi. Daudi akasema, “Mefiboshethi.” Naye akajibu, “Angalia, mimi ni mtumishi wako!
7 Daudi akamwambia, “Usiogope, maana hakika nitakufadhiri kwa ajili ya Yonathani baba yako, nami nitakurudishia ardhi yote ya Sauli babu yako, nawe utakula katika meza yangu daima.”
8 Mefiboshethi akainama na kusema, “Mtumishi wako ni nani, hata ukamwangalia kwa fadhiri mbwa mfu kama nilivyo?”
9 Kisha mfalme akamwita Siba, mtumishi wa Sauli, na kumwambia, “Yote yaliyo ya Sauli na familia yake nimempa mjukuu wa bwana wako.
10 Wewe, wanao, na watumishi wako mtalima mashamba kwa ajili yake nanyi mtavuna mazao ili kwamba mjukuu wa bwana wako apate chakula. Kwa maana Mefiboshethi, mjukuu wa bwana wako, atakula katika meza yangu daima.” Basi Siba alikuwa na wana kumi na watano na watumishi ishirini.
11 Kisha Siba akamwambia mfalme, “Mtumishi wako atafanya yote ambayo bwana wangu mfalme amemwamuru mtumishi wake.” Mfalme akaongeza kusema, kwa Mefiboshethi yeye atakula katika meza yangu, kama mmojawapo ya wana wa mfalme.”
12 Mefiboshethi alikuwa na mwana mdogo jina lake Mika. Na wote waliokuwa wanaishi katika nyumba ya Siba walikuwa watumishi wa Mefiboshethi.
13 Hivyo Mefiboshethi akaishi Yerusalemu, naye akala chakula cha daima katika meza ya mfalme, japokuwa alikuwa mlemavu wa miguu yote.