< 2 Samweli 8 >
1 ikawa baada ya haya Daudi aliwashambulia Wafilisti na kuwashinda. Hivyo Daudi akaichukua Gathi na vijiji vyake kutoka katika mamlaka ya wafilisti.
Baada ya muda, Daudi akawashinda Wafilisti na kuwatiisha, naye akautwaa Metheg-Amma kutoka mikononi mwa Wafilisti.
2 Kisha akaishinda Moabu na akawapima watu wake kwa mstari kwa kuwafanya walale chini juu ya ardhi. Alipima mistari miwili ya kuua, na mstari mmoja kamili kuwahifadhi hai. Hivyo Wamoabu wakawa watumishi wa Daudi na wakaanza kumlipa kodi.
Pia Daudi akawashinda Wamoabu. Akawafanya walale chini kwa mstari akawapima kwa urefu wa kamba. Kila alipopima urefu wa hiyo kamba mara mbili hilo kundi waliuawa na alipopima mara ya tatu aliwaacha hai. Kwa hiyo Wamoabu wakawa chini ya Daudi nao wakamletea kodi.
3 Kisha Daudi akamshinda Hadadezeri mwana wa Rehobu, mfalme wa Soba, Hadadezeri aliposafiri kuurudisha ufalme wake katika mto Frati.
Zaidi ya hayo, Daudi akapigana na Hadadezeri mwana wa Rehobu, mfalme wa Soba, alipokwenda kurudisha tena utawala wake kwenye eneo la Mto Frati.
4 Daudi aliteka magari 1, 700 ya farasi na askari ishirini elfu waendao kwa miguu. Daudi akawakata miguu farasi wa magari, lakini akahifadhi wakutosha magari mia moja.
Daudi akateka magari yake ya vita 1,000, askari wapanda farasi 7,000 na askari 20,000 watembeao kwa miguu. Daudi akawakata wale farasi wote wakokotao magari mishipa ya miguu, isipokuwa farasi 100 hakuwakata.
5 Wakati Washami wa Dameski walipokuja kumsaidia Hadadeziri mfalme wa Soba, Daudi akaua katika Washami watu ishirini na mbili elfu.
Waaramu wa Dameski walipokuja kumsaidia Hadadezeri mfalme wa Soba, Daudi akawashambulia na kuwaua 22,000 miongoni mwao.
6 Daudi akaweka ngome huko Shamu ya Dameski, na Washami wakawa watumishi wake na wakaleta kodi. Yahwe akampa Daudi ushindi kila alikokwenda.
Daudi akaweka askari walinzi katika ufalme wa Waaramu huko Dameski, nao Waaramu wakawa watumwa wake na kumlipa ushuru. Bwana akampa Daudi ushindi kote alipokwenda.
7 Daudi akachukua ngao za dhahabu walizokuwa nazo watumishi wa Hadadezeri naye akazileta Yerusalemu.
Daudi akazitwaa ngao za dhahabu zilizokuwa za maafisa wa Hadadezeri na kuzileta Yerusalemu.
8 Mfalme Daudi akachukua shaba nyingi kutoka Beta na Berosai, miji ya Hadadezeri.
Kutoka miji ya Beta na Berothai, iliyokuwa miji ya Hadadezeri, Mfalme Daudi akatwaa shaba nyingi sana.
9 Wakati Tou, mfalme wa Hamathi, aliposikia kwamba Daudi amelishinda jeshi lote la Hadadezeri,
Tou, mfalme wa Hamathi, aliposikia kwamba Daudi amelishinda jeshi lote la Hadadezeri,
10 Tou akamtuma Hadoramu mwanawe kwa mfalme Daudi kumpa salamu na kumbariki, kwa kuwa Daudi alikuwa amepigana na Hadadezeri na kumshinda, maana Hadadezeri alikuwa amepiga vita dhidi ya Tou. Hadoramu akaja pamoja na vitu vya fedha, dhahabu, na shaba.
akamtuma mwanawe Yoramu kwa Mfalme Daudi kumsalimu na kumpongeza kwa ushindi wake katika vita dhidi ya Hadadezeri, kwa kuwa Hadadezeri alikuwa amepigana vita na Tou. Yoramu akamletea Daudi vyombo vya fedha, dhahabu na shaba.
11 Mfalme Daudi akaviweka wakfu vitu hivi kwa ajili ya Yahwe, pamoja na fedha na dhahabu kutoka katika mataifa yote aliyokuwa ameyashinda-
Mfalme Daudi akaviweka vifaa hivi wakfu kwa Bwana, kama vile alivyokuwa amefanya kwa fedha na dhahabu kutoka kwa mataifa yote aliyokuwa ameyashinda:
12 kutoka Shamu, Moabu, Waamoni, Wafilist, Waamaleki, pamoja na nyara zote alizoziteka kutoka kwa Hadadezeri mwana wa Rehobu, mfalme wa Soba.
yaani Edomu, Moabu, Waamoni, Wafilisti na Waamaleki. Pia akaweka wakfu nyara alizoteka kutoka kwa Hadadezeri mwana wa Rehobu, mfalme wa Soba.
13 Jina la Daudi likajulikana sana alipowashinda washami katika bonde la Chumvi, pamoja na watu wao wapatao elfu kumi na nane.
Naye Daudi akapata sifa baada ya kurudi kutoka kuwaua Waedomu 18,000 katika Bonde la Chumvi.
14 Akaweka ngome katika Edomu yote, na Waedomu wote wakawa watumishi wake. Yahwe akampa Daudi ushindi kila alipokwenda.
Akaweka kambi za askari walinzi katika Edomu yote, nao Waedomu wakawa chini ya Daudi. Bwana alimpatia Daudi ushindi kila alipokwenda.
15 Daudi akatawala juu ya Israeli yote, naye akatenda kwa haki na usawa kwa watu wote.
Daudi akatawala Israeli yote, akitenda lililo haki na sawa kwa watu wake wote.
16 Yoabu mwana wa Seruya alikuwa mkuu wa jeshi, na Yehoshafati mwana wa Ahiludi alikuwa mwenye kuandika taarifa.
Yoabu mwana wa Seruya alikuwa jemadari wa jeshi; Yehoshafati mwana wa Ahiludi alikuwa mweka kumbukumbu;
17 Sadoki mwana wa Ahitubu na Ahimeleki mwana wa Abiathari walikuwa makuhani, na Seraya alikuwa mwandishi.
Sadoki mwana wa Ahitubu na Ahimeleki mwana wa Abiathari walikuwa makuhani; Seraya alikuwa mwandishi;
18 Benaya mwana wa Yehoyada alikuwa juu ya Wakerethi na Wapelethi, na wana wa Daudi walikuwa washauri wa mfalme.
Benaya mwana wa Yehoyada alikuwa msimamizi wa Wakerethi na Wapelethi; nao wana wa Daudi walikuwa washauri wa mfalme.