< 2 Samweli 3 >
1 Kulikuwa na vita ya mda mrefu kati ya nyumba ya Sauli na nyumba ya Daudi. Daudi akaendelea kupata nguvu zaidi, lakini nyumba ya Sauli iliendelea kudhoofika na kuthoofika.
Vita kati ya nyumba ya Sauli na nyumba ya Daudi vilidumu kwa muda mrefu. Daudi akaendelea kuwa imara zaidi na zaidi, wakati nyumba ya Sauli iliendelea kudhoofika zaidi na zaidi.
2 Wana wakazaliwa kwa Daudi huko Hebron. Mzaliwa wake wa kwanza alikuwa Amnoni, kwa Ahinoamu wa Yezreeli.
Wana walizaliwa kwa Daudi huko Hebroni: Mzaliwa wake wa kwanza alikuwa Amnoni mwana wa Ahinoamu wa Yezreeli;
3 Mwanawe wa pili, Kileabu, alizaliwa kwa Abigaili, mjane wa Nabali wa Karmeli. Wa tatu, Absalomu, alikuwa mwana wa Maaka, binti Talmai, mfalme wa Geshuri.
mzaliwa wake wa pili alikuwa Danieli mwana wa Abigaili, mjane wa Nabali wa Karmeli; wa tatu, Absalomu mwana wa Maaka, binti Talmai mfalme wa Geshuri;
4 Mwana wa nne wa Daudi, Adoniya, alikuwa mwana wa Hagithi. Mwanawe wa tano alikuwa Shefatia mwana wa Abitali,
wa nne, Adoniya mwana wa Hagithi; wa tano, Shefatia mwana wa Abitali;
5 na wa sita, Ithreamu, alikuwa mwana wa Egla mkewe Daudi. Hawa wote walizaliwa kwa Daudi huko Hebroni.
wa sita, Ithreamu mwana wa Egla, mkewe Daudi. Hawa ndio waliozaliwa kwa Daudi huko Hebroni.
6 Ikawa wakati wa vita kati ya nyumba ya Sauli na nyumba ya Daudi Abneri akajifanya mwenye nguvu katika nyumba ya Sauli.
Wakati wa vita kati ya nyumba ya Sauli na nyumba ya Daudi, Abneri alikuwa anajiimarisha katika nafasi yake kwenye nyumba ya Sauli.
7 Sauli alikuwa na suria jina lake Rispa, binti Aiya. Ishboshethi akamuuliza Abneri, “Kwa nini umelala na suria wa baba yangu?”
Basi Sauli alikuwa amekuwa na suria, jina lake Rispa binti wa Aiya. Naye Ish-Boshethi akamwambia Abneri, “Kwa nini umekutana kimwili na suria wa baba yangu?”
8 Hata ikawa Abneri akakasirika sana kutokana na maneno ya Ishboshethi naye akasema, “Je mimi ni kichwa cha mbwa wa Yuda? Ninaonesha uaminifu kwa nyumba ya Sauli, baba yako, kwa jamaa yake, na rafiki zake, kwa kutokukuweka katika mkono wa Daudi. Na bado leo unanishutumu kuhusu mwanamke.
Abneri akakasirika sana kwa sababu ya kile Ish-Boshethi alichosema, naye akamjibu, “Je, mimi ni kichwa cha mbwa, kwa upande wa Yuda? Siku hii ya leo mimi ni mtiifu kwa nyumba ya baba yako Sauli, kwa jamaa yake na rafiki zake. Sijakukabidhi kwa Daudi, lakini bado unanilaumu kwa kosa la kuhusika na huyu mwanamke!
9 Mungu na anifanyie hivyo, Abneri, na kuzidi, ikiwa sitafanya kwa Daudi kama Yahwe alivyomwapia,
Mungu na amshughulikie Abneri, tena kwa ukali, ikiwa sitafanya kwa ajili ya Daudi kile Bwana alichomwahidi kwa kiapo,
10 kuuhamisha ufalme kutoka nyumba ya Sauli na kukisimika kiti cha enzi cha Daudi juu ya Israeli na juu ya Yuda, kutoka Dani hadi Beersheba.”
na kuuhamisha ufalme kutoka kwenye nyumba ya Sauli na kuimarisha kiti cha ufalme cha Daudi juu ya Israeli na Yuda kuanzia Dani mpaka Beer-Sheba.”
11 Ishboshethi hakuweza kumjibu Abneri neno tena, kwani alimuogopa.
Ish-Boshethi hakuthubutu kusema neno jingine kwa Abneri, kwa sababu alimwogopa Abneri.
12 Kisha Abneri akatuma wajumbe kwa Daudi kusema, “Nchi hii ni ya nani? Fanya agano nami, nawe utaona kwamba mkono wangu uko nawe, kuiIeta Israeli yote kwako.”
Ndipo Abneri akatuma wajumbe kwa niaba yake kwa Daudi, kumwambia, “Nchi hii ni ya nani? Fanya mapatano na mimi, nami nitakusaidia kuiweka Israeli yote juu yako.”
13 Daudi akajibu, “Vema, nitafanya agano nawe. Lakini neno moja ninalolitaka kutoka kwako ni kwamba hautauona uso wangu usipomuleta kwanza Mikali, binti Sauli, unapokuja kuonana nami.”
Daudi akasema, “Vyema, nitafanya mapatano nawe. Lakini nahitaji jambo moja kwako: Usije mbele yangu mpaka umemleta Mikali binti Sauli wakati utakapokuja kuniona.”
14 Kisha Daudi akatuma wajumbe kwa Ishboshethi, mwana wa Sauli, kusema, “Nipe Mikali, mke wangu niliyetoa kwa ajili yake govi mia moja za Wafilisti.”
Kisha Daudi akapeleka wajumbe kwa Ish-Boshethi mwana wa Sauli, kudai, “Nipe Mikali mke wangu, ambaye nilimposa mwenyewe kwa mahari ya magovi 100 ya Wafilisti.”
15 Hivyo Ishboshethi akatuma kwa Mikali na kumchukua kutoka kwa mme wake, Paltieli mwana wa Laishi.
Kwa hiyo Ish-Boshethi akatoa amri kwamba Mikali achukuliwe kutoka kwa Paltieli mumewe, mwana wa Laishi.
16 Mme wake akafuatana naye, huku akilia, akaendelea hadi Bahurimu. Kisha Abneri akamwambia, “basi sasa rudi nyumbani.” Hivyo akarudi.
Hata hivyo, mumewe alikwenda pamoja naye, akilia nyuma ya mkewe njia yote hadi Bahurimu. Ndipo Abneri akamwambia Paltieli, “Rudi nyumbani!” Kwa hiyo akarudi.
17 Abneri akaongea na wazee wa Israeli kusema, “Zamani mlitaka Daudi awe mfalme wenu.
Abneri akafanya shauri pamoja na wazee wa Israeli, akasema, “Muda mrefu mmetaka kumfanya Daudi mfalme wenu.
18 Basi sasa fanyeni hivyo. Kwa maana Yahwe alisema kuhusu Daudi kusema, “Kwa mkono wa Daudi mtumishi wangu nitawaokoa watu wangu Israeli kutoka katika mkono wa Wafilisti na kutoka katika mkono wa adui zao wote.”
Sasa fanyeni hivyo! Kwa maana Bwana alimwahidi Daudi akisema, ‘Kwa kupitia Daudi mtumishi wangu nitawaokoa watu wangu Israeli kutoka mikononi mwa Wafilisti na kutoka mikononi mwa adui zako wote.’”
19 Pia Abneri akasema na watu wa Benjamini ana kwa ana. Kisha Abneri akaenda kuongea na Daudi huko Hebroni akaeleza kila jambo ambalo Israeli na nyumba yote ya Benjamini walitamani kulitimiza.
Pia Abneri mwenyewe akazungumza na kabila la Benyamini. Kisha akaenda mpaka Hebroni kumwambia Daudi kila kitu ambacho Israeli na nyumba yote ya Benyamini walichotaka kufanya.
20 Wakati Abneri na watu ishirini kati ya watu wake walifika Hebroni kumuona Daudi, Daudi akaandaa sherehe kwa ajili yao.
Wakati Abneri aliyekuwa na watu ishirini pamoja naye, alipokuja kwa Daudi huko Hebroni, Daudi akamwandalia karamu pamoja na watu wake.
21 Abneri akamweleza Daudi, “Nitainuka na kukukusanyia Israeli wote, bwana wangu mfalme, ili kwamba wafanye agano nawe, kwamba utawale juu ya yote unayotaka.” Hivyo Daudi akamruhusu Abneri kuondoka, Abneri akaondoka kwa amani.
Ndipo Abneri akamwambia Daudi, “Niache niende mara moja nikakusanye Israeli yote kwa ajili ya mfalme bwana wangu, ili waweze kufanya mapatano na wewe, ili kwamba uweze kutawala juu ya yote yale ambayo moyo wako unaonea shauku.” Basi Daudi akamuaga Abneri, naye akaenda kwa amani.
22 Kisha askari wa Daudi na Yoabu wakarudi kutoka katika kuteka nyara na wakaja na nyara nyingi. Lakini Abneri hakuwepo Hebroni pamoja na Daudi. Daudi alikuwa amemruhusu kuondoka, na alikuwa ameondoka kwa amani.
Wakati huo huo, watu wa Daudi na Yoabu walirudi kutoka kwenye kushambulia, nao wakarudi na nyara nyingi mno. Lakini Abneri hakuwa tena pamoja na Daudi huko Hebroni, kwa sababu Daudi alikuwa amemruhusu aende zake, naye akaenda kwa amani.
23 Wakati Yoabu na Jeshi lote walipofika, Yoabu aliambiwa, “Abneri mwana wa Neri alikuja kwa mfalme, na mfalme amemruhusu kuondoka, naye Abneri ameondoka kwa amani.”
Yoabu na askari wote aliokuwa nao walipowasili, aliambiwa kwamba Abneri mwana wa Neri alikuwa amekuja kwa mfalme na kwamba mfalme alikuwa amemruhusu aende zake, na kwamba alikwisha ondoka kwa amani.
24 Kisha Yoabu akaja kwa mfalme na kusema, “Umefanya nini? Tazama, Abneri alikuja kwako! Kwa nini umemruhusu kuondoka, naye amenda?
Basi Yoabu alikwenda kwa mfalme na kumwambia, “Ni nini hiki ulichofanya? Tazama, Abneri alikuja kwako. Kwa nini ukamwacha aende? Sasa amekwenda!
25 Haujui kwamba Abneri mwana wa Neri alikuja kukudanganya na kupeleleza hali yako na kuangalia kila unalofanya?”
Wajua Abneri mwana wa Neri alikuja kukudanganya na kuchunguza nyendo zako na kupata kila kitu unachokifanya.”
26 Yoabu alipoondoka kwa Daudi, alituma wajumbe kumfuatia Abneri, nao wakamrudisha kutoka katika kisima cha Sirah, lakini Daudi hakulijua hili.
Ndipo Yoabu akamwacha Daudi na kutuma wajumbe wamfuate Abneri, nao wakamrudisha kutoka kisima cha Sira. Lakini Daudi hakufahamu jambo hili.
27 Abneri aliporudi Hebroni, Yoabu alimchukua kando kati ya lango ili aongee naye faraghani. Hapohapo Yoabu alimchoka tumboni na kumuua. Hivyo, akalipa kisasi cha damu ya Asaheli nduguye.
Basi Abneri aliporudi Hebroni, Yoabu akamchukua kando ndani ya lango, kama vile kuzungumza naye faraghani. Ili kulipiza kisasi damu ya nduguye Asaheli, Yoabu akamchoma mkuki tumboni palepale, naye akafa.
28 Daudi alipolisikia jambo hili akasema, “Mimi na ufalme wangu hatuna hatia mbele za Yahwe daima, kuhusiana na damu ya Abneri mwana wa Neri.
Baadaye, Daudi aliposikia kuhusu jambo hili, akasema, “Mimi na ufalme wangu kamwe hatuna hatia mbele za Bwana kuhusu damu ya Abneri mwana wa Neri.
29 Hatia ya damu ya Abneri na iwe juu ya Yoabu na nyumba yote ya baba yake. Na asikosekane katika familia ya Yoabu mtu mwenye vidonda, au mwenye ukoma, au kirema atembeaye kwa fimbo au aliyeuawa kwa upanga au mwenye kukosa chakula.”
Damu yake na iwe juu ya kichwa cha Yoabu na juu ya nyumba yote ya baba yake! Kamwe asikosekane yeyote katika nyumba ya Yoabu mwenye kidonda chenye usaha, au ukoma au mwenye kuegemea fimbo au aangukaye kwa upanga au kupungukiwa na chakula.”
30 Hivyo Yoabu na Abishai nduguye wakamwua Abneri, kwa sababu alimwua Asaheli ndugu yao vitani huko Gibeoni.
(Yoabu na Abishai ndugu yake walimuua Abneri kwa sababu alikuwa amemuua Asaheli ndugu yao katika vita huko Gibeoni.)
31 Daudi akamwambia Yoabu na wote waliokuwa pamoja naye, “Rarueni mavazi yenu, jivikeni nguo za magunia, na muomboleze mbele ya mwili wa Abneri.” Na mfalme Daudi akaufuata mwili wa Abneri wakati wa mazishi.
Kisha Daudi akamwambia Yoabu na watu wote aliokuwa pamoja nao, “Rarueni nguo zenu na mvae nguo za gunia na mtembee mkiomboleza mbele ya Abneri.” Mfalme Daudi mwenyewe akatembea nyuma ya jeneza.
32 Wakamzika Abneri huko Hebroni. Mfalme akalia kwa sauti katika kaburi la Abneri, na watu wote pia wakalia.
Wakamzika Abneri huko Hebroni, naye mfalme akalia kwa sauti kwenye kaburi la Abneri. Pia watu wote wakalia.
33 Mfalme akamwombolea Abneri naye akaimbo, “Je ilipasa Abneri afe kama afavyo mpumbavu?
Mfalme akaimba ombolezo hili kwa ajili ya Abneri: “Je, ilipasa Abneri afe kama afavyo mpumbavu?
34 Mikono yako haikufungwa. Miguu yako hakuwa imefungwa minyororo. Kama mtu aangukavyo mbele ya wana wa uovu, ndivyo ulivyoanguka.” Watu wote wakamlilia zaidi.
Mikono yako haikufungwa, miguu yako haikufungwa pingu. Ulianguka kama yeye aangukaye mbele ya watu waovu.” Nao watu wote wakamlilia tena.
35 Watu wote wakaja kumtaka Daudi ale wakati kungali mchana, lakini Daudi akaapa, “Mungu na anifanyie hivyo, na kuzidi, ikiwa nitaonja mkate au chochote kabla jua halijazama.”
Kisha watu wote wakaja kumsihi Daudi ale chochote kulipokuwa kungali bado mchana; lakini Daudi akaapa, akisema, “Mungu na anishughulikie, tena kwa ukali, kama nikionja mkate au kitu kingine chochote kabla ya jua kutua!”
36 Watu wote wakaiona huzuni ya Daudi, na ikawapendeza, hivyo kila alichokifanya mfalme kikawapendeza.
Watu wote wakaona hilo nao ikawapendeza; naam, kila kitu mfalme alichofanya kiliwapendeza.
37 Hivyo watu wote na Israeli wote wakatambua siku hiyo kwamba haikuwa nia ya mfalme Abneri mwana wa Neri afe.
Kwa hiyo siku ile watu wote na Israeli yote wakajua kwamba mfalme hakushiriki katika mauaji ya Abneri mwana wa Neri.
38 Mfalme akawaambia watumishi wake, “je hamjui kuwa mtu mkuu ameanguka leo hii katika Israeli?
Kisha mfalme akawaambia watu wake, “Je, hamfahamu kwamba mkuu na mtu mashuhuri ameanguka katika Israeli leo?
39 Nami leo nimedhoofika, japokuwa nimetiwa mafuta kuwa mfalme. Watu hawa, wana wa Seruya ni hatari sana kwangu. Yahwe na amrudishie mwovu kwa kumlipa kwa ajili ya uovu wake kama anavyostahili.
Nami leo ingawa ni mfalme mpakwa mafuta, mimi ni dhaifu, nao hawa wana wa Seruya wananizidi nguvu. Bwana na amlipize mtenda maovu sawasawa na matendo yake maovu!”