< 2 Samweli 22 >

1 Daudi akamwimbia Yahwe maneno ya wimbo huu siku ile Yahwe alipomwokoa katika mkono wa adui zake wote na katika mkono wa Sauli.
Daudi alimwimbia Bwana maneno ya wimbo huu wakati Bwana alipomwokoa mikononi mwa adui zake wote, na pia mkononi mwa Sauli.
2 Akaomba hivi, “Yahwe ni mwamba wangu, ngome yangu, aliyeniokoa.
Akasema: “Bwana ni mwamba wangu, ngome yangu na mwokozi wangu,
3 Mungu ni mwamba wangu. Yeye ni kimbilio langu. Ngao yangu, pembe ya wokovu wangu, ngome yangu na kimbilio langu, aniokoaye na mabaya yote.
Mungu wangu ni mwamba wangu, ambaye kwake ninakimbilia, ngao yangu na pembe ya wokovu wangu. Yeye ni ngome yangu, kimbilio langu na mwokozi wangu, huniokoa kutoka kwa watu wenye jeuri.
4 Nitamwita Yahwe, astahiliye kutukuzwa, nami nitaokolewa kutoka kwa adui zangu.
Ninamwita Bwana, anayestahili kusifiwa, nami ninaokolewa kutoka kwa adui zangu.
5 Maana mawimbi ya mauti yalinizunguka, mafuriko ya maji ya uharibifu yakanishinda.
“Mawimbi ya mauti yalinizunguka, mafuriko ya maangamizi yalinilemea.
6 Vifungo vya kuzimu vilinizunguka; kamba za mauti zikaninasa. (Sheol h7585)
Kamba za kuzimu zilinizunguka, mitego ya mauti ilinikabili. (Sheol h7585)
7 Katika shida yangu nalimwita Yahwe; nilimwita Mungu wangu; akaisikia sauti yangu katika hekalu lake, na kilio changu cha msaada kikafika masikioni mwake.
Katika shida yangu nalimwita Bwana, nilimlilia Mungu wangu. Kutoka Hekaluni mwake alisikia sauti yangu, kilio changu kikafika masikioni mwake.
8 Ndipo nchi ilipotikisika na kutetemeka. Misingi ya mbingu ikatetemeka na kutikiswa, kwa kuwa Mungu alikasirika.
“Dunia ilitetemeka na kutikisika, misingi ya mbingu ikatikisika, vilitetemeka kwa sababu alikuwa amekasirika.
9 Moshi ukatoka katika pua yake, na miale ya moto ikatoka katika kinywa chake. Makaa yakawashwa nayo.
Moshi ukapanda kutoka puani mwake, moto uteketezao ukatoka kinywani mwake, makaa ya moto yawakayo yakatoka ndani mwake.
10 Alizifungua mbingu akashuka, na giza totoro lilikuwa chini ya miguu yake.
Akazipasua mbingu akashuka chini, mawingu meusi yalikuwa chini ya miguu yake.
11 Alipanda juu ya kerubi na kuruka. Alionekana katika mawingu ya upepo.
Alipanda juu ya kerubi akaruka, akapaa juu kwa mbawa za upepo.
12 Naye akalifanya giza kuwa hema kumzunguka, akakusanya mawingu makubwa ya mvua angani.
Alifanya giza hema lake la kujifunika: mawingu meusi ya mvua ya angani.
13 Makaa ya moto yalidondoka mbele zake kutoka katika radi.
Kutokana na mwanga wa uwepo wake mawingu yalisogea, ikanyesha mvua ya mawe na umeme wa radi.
14 Yahwe alishuka kutoka katika mbingu. Aliyejuu alipiga kelele.
Bwana alinguruma kutoka mbinguni, sauti ya Aliye Juu Sana ilisikika.
15 Alipiga mishale na kuwatawanya adui zake—miale ya radi na kuwasambaratisha.
Aliipiga mishale na kutawanya adui, umeme wa radi na kuwafukuza.
16 Kisha njia za maji zikaonekana; misingi ya dunia ikawa wazi katika kilio cha vita ya Yahweh, katika sauti za pumzi ya pua zake.
Mabonde ya bahari yalifunuliwa, na misingi ya dunia ikawa wazi kwa kukaripia kwake Bwana, kwa uvumi wa pumzi kutoka puani mwake.
17 Kutoka juu alifika chini; akanishikilia! Aliniondoa katika vilindi vya maji.
“Alinyoosha mkono kutoka juu na kunishika; alinitoa kutoka kilindi cha maji makuu.
18 Aliniokoa kutoka kwa adui zangu wenye nguvu, kwao walionichukia, kwa maana walikuwa na nguvu sana kwangu.
Aliniokoa kutoka adui wangu mwenye nguvu nyingi, kutoka adui zangu waliokuwa na nguvu nyingi kuliko mimi.
19 Walikuja kinyume changu siku ya shida yangu, lakini Yahwe alikuwa msaada wangu.
Walinikabili siku ya msiba wangu, lakini Bwana alikuwa msaada wangu.
20 Pia aliniweka mahali panapo nafasi. Aliniokoa kwa kuwa alipendezwa nami.
Alinileta nje mahali penye nafasi tele, akaniokoa kwa kuwa alipendezwa nami.
21 Yahwe amenituza kwa kipimo cha haki yangu; amenirejesha kwa kiwango cha usafi wa mikono yangu.
“Bwana alinitendea sawasawa na uadilifu wangu; sawasawa na usafi wa mikono yangu amenilipa.
22 Kwa maana nimezishika njia za Yahwe na sijafanya uovu kwa kugeuka kutoka kwa Mungu.
Kwa maana nimezishika njia za Bwana; sijatenda ubaya nikamwacha Mungu wangu.
23 Kwa kuwa maagizo yake yote ya haki yamekuwa mbele yangu; kwa kuwa sheria zake, sikujiepusha nazo.
Sheria zake zote zi mbele yangu, wala sijayaacha maagizo yake.
24 Nimekuwa bila hatia mbele zake pia, na nimejiepusha na dhambi.
Nimekuwa sina hatia mbele zake, nami nimejilinda nisitende dhambi.
25 Kwa hiyo Yahwe amenirejesha kwa kiasi cha uadilifu wangu, kwa kipimo cha usafi wangu mbele zake.
Bwana amenilipa sawasawa na uadilifu wangu, sawasawa na usafi wangu machoni pake.
26 Kwa mwaminifu, unajionesha kuwa mwaminifu; kwake asiye na hatia; unajionesha kuwa hauna hatia.
“Kwa yeye aliye mwaminifu unajionyesha kuwa mwaminifu, kwa asiye na hatia unajionyesha kutokuwa na hatia,
27 Kwa usafi unajionesha kuwa msafi, lakini kwa wakaidi unajionesha kuwa mkaidi.
kwa aliye mtakatifu unajionyesha kuwa mtakatifu, lakini kwa aliyepotoka unajionyesha kuwa mkaidi.
28 Unaokoa walioteswa, lakini macho yako ni kinyume cha wenye kiburi, unawashusha chini.
Wewe huwaokoa wanyenyekevu, lakini macho yako ni juu ya wenye kiburi ili uwashushe.
29 Kwa maana wewe ni taa yangu, Yahwe. Yahwe huangaza katika giza langu.
Wewe ni taa yangu, Ee Bwana. Bwana hulifanya giza langu kuwa mwanga.
30 Maana kwa ajili yake ninaweza kupita vipingamizi; kwa msaada wa Mungu wangu naweza kuruka juu ya ukuta.
Kwa msaada wako naweza kushinda jeshi, nikiwa pamoja na Mungu wangu nitaweza kuruka ukuta.
31 Maana njia za Mungu ni kamilifu. Neno la Yahwe ni safi. Yeye ni ngao yao wanaomkimbilia.
“Kuhusu Mungu, njia yake ni kamilifu; neno la Bwana halina dosari. Yeye ni ngao kwa wote wanaokimbilia kwake.
32 Maana ni nani aliye Mungu isipokuwa Yahwe? Na ni nani aliyemwamba isipokuwa Mungu?
Kwa maana ni nani aliye Mungu zaidi ya Bwana? Ni nani aliye Mwamba isipokuwa Mungu wetu?
33 Mungu ni kimbilio langu, na umwongoza katika njia yake mtu asiye na hatia.
Mungu ndiye anivikaye nguvu na kufanya njia yangu kuwa kamilifu.
34 Huifanya myepesi miguu yangu kama kurungu na kuniweka katika vilima virefu.
Huifanya miguu yangu kama miguu ya kulungu, huniwezesha kusimama mahali palipo juu.
35 Huifundisha mikono yangu kwa vita, na viganja vyangu kupinda upinde wa shaba.
Huifundisha mikono yangu kupigana vita; mikono yangu inaweza kupinda upinde wa shaba.
36 Umenipa ngao ya wokovu wako, na matakwa yako yamenifanya mkuu.
Hunipa ngao yako ya ushindi, unajishusha chini ili kuniinua.
37 Umeitengenezea miguu yangu nafasi chini yangu, hivyo miguu yangu haikujikwaa.
Huyapanua mapito yangu, ili miguu yangu isiteleze.
38 Niliwafuatia adui zangu na kuwaangamiza. Sikurudi nyuma hadi walipoangamizwa.
“Niliwafuatia adui zangu na nikawaseta, sikurudi nyuma mpaka walipoangamizwa.
39 Niliwararua na kuwasambaratisha; hawawezi kuinuka. Wameanguka chini ya miguu yangu.
Niliwaseta kabisa, nao hawakuweza kuinuka tena; walianguka chini ya miguu yangu.
40 Unaweka nguvu ndani yangu kama mkanda kwa vita; unawaweka chini yangu wanaoinuka kinyume changu.
Ulinivika nguvu kwa ajili ya kupigana vita; uliwafanya adui zangu wasujudu miguuni pangu.
41 Ulinipa migongo ya shingo za adui zangu; niliwaangamiza kabisa wale wanaonichukia.
Uliwafanya adui zangu wageuke na kukimbia, nami nikawaangamiza adui zangu.
42 Walilia kwa msaada, lakini hakuna aliyewaokoa; walimlilia Yahwe, lakini hakuwajibu.
Walipiga yowe, lakini hapakuwepo na yeyote wa kuwaokoa; walimlilia Bwana, lakini hakuwajibu.
43 Niliwaponda katika vipande kama mavumbi juu ya ardhi, niliwakanyaga kama matope mitaani.
Niliwaponda kama mavumbi ya nchi; niliwaponda na kuwakanyaga kama tope barabarani.
44 Umeniokoa pia kutoka katika mashutumu ya watu wangu. Umeniweka kama kichwa cha mataifa. Watu nisiowajua wananitumikia.
“Umeniokoa kutokana na mashambulizi ya watu wangu; umenihifadhi mimi kama kiongozi wa mataifa. Watu ambao sikuwajua wananitumikia,
45 Wageni walishurutishwa kuniinamia. Mara waliposikia kuhusu mimi, walinitii.
nao wageni huja wakininyenyekea, mara wanisikiapo, hunitii.
46 Wageni walikuja wakitetemeka kutoka katika ngome zao.
Wote wanalegea, wanatoka katika ngome zao wakitetemeka.
47 Yahwe anaishi! Mwamba wangu atukuzwe. Mungu na ainuliwe, mwamba wa wokovu wangu.
“Bwana yu hai! Sifa ni kwa Mwamba wangu! Atukuzwe Mungu, Mwamba, Mwokozi wangu!
48 Huyu ndiye Mungu anilipiaye kisasi, awawekaye watu chini yangu.
Yeye ndiye Mungu anilipiziaye kisasi, ayawekaye mataifa chini yangu,
49 Uniweka huru mbali na adui zangu. Hakika, uliniinua juu yao walioinuka kinyume changu. Uliniokoa kutoka kwa watu wenye ghasia.
aniwekaye huru toka kwa adui zangu. Uliniinua juu ya adui zangu; uliniokoa toka kwa watu wajeuri.
50 Kwa hiyo nitakushukuru, Yahwe, kati ya mataifa; nitaliimbia sifa jina lako.
Kwa hiyo nitakusifu, Ee Bwana, katikati ya mataifa; nitaliimbia sifa jina lako.
51 Mungu hutoa ushindi mkuu kwa mfalme wake, na uonesha uaminifu wake wa kiagano kwa mtiwa mafuta wake, kwa Daudi na uzao wake daima.”
Humpa mfalme wake ushindi mkuu; huonyesha fadhili zake kwa mpakwa mafuta wake, kwa Daudi na wazao wake milele.”

< 2 Samweli 22 >